Alhamisi, 25 Januari 2024

WIKI YA SHERIA YAANZA MKOANI KAGERA

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Watanzania mkoani Kagera na maeneo ya jirani jana tarehe 24 Januari, 2024 wameanza kujitokeza katika Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria ili kupata elimu na ufafanuzi wa kisheria kwenye masuala kadhaa kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

Elimu hiyo inatolewa katika mabanda yaliyopo katika viwanja hivyo, kwa kushirikiana na wadau, wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Takukuru, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Ofisi ya Huduma kwa Jamii, Ustawi wa Jamii, Wakala wa Huduma za Misitu na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), wote kutoka Mkoa wa Kagera.

Kadhalika, elimu kama hiyo inaendelea kutolewa katika vituo vya Radio, Televisioni, Vyuoni, Mashuleni, Mialoni, Masokoni, Viwandani kwa lengo la kuelimisha wananchi.

Utoaji wa elimu hiyo unaongozwa na kauli mbiu Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu 2024 inayosema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa:Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa Haki Jinai.”

Mada mbalimabali zinatolewa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi zikiwemo: Sheria ya Mtoto, Mashauri ya Kujamiiana, Ukatili wa Kijinsia, Sheria za Kazi na Mahusiano ya Ajira, Sheria za Uvuvi, Muundo wa Mahakama, Sheria za Ardhi, Mabaraza ya Ardhi na Mamlaka zake, Ndoa na Talaka, Wosia na Taratibu zake, Rushwa na Uhujumu Uchumi.















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni