Na Francisca Swai – Mahakama, Musoma
Mahakama ya Tanzania Kanda ya Musoma katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, imeendelea kuwafikia wananchi na wadau wa haki jinai kwa namna mbalimbali, ikiwemo utoaji wa elimu na misaada kwa makundi ya wahitaji.
Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake wametembelea na kutoa elimu kwa wafungwa na mahabusu wa Gereza la Musoma leo tarehe 29 Januari, 2024 pamoja na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika Gereza hilo.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tendo Jema, Mhe. Eugenia Rujwahuka, amesema Mahakama na wadau wake wameshirikiana kuleta mahitahi hayo muhimu ikiwemo Televisheni (TV) na king’amuzi kwa ajili ya gereza la wanawake.
Wadau hao ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, TIGO, Waandishi wa Habari, Wanasheria wa Kujitegemea na wafanyabiashara Musoma.
Naye Mfanyabiashara na Mlezi wa Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Mara, Bi. Joyce Sokombi amesema wao wameshirikiana na Mahakama katika tendo hilo jema la kibinadamu kwani mtu kuwa gerezani haimaanishi jamii imetenge.
‘‘Gerezani ni mahali pa kujirekebisha na mtu anapotoka kurudi kwenye jamii anakuwa amejifunza mambo mengi mazuri na kuwa raia mwema, hivyo ni wajibu wetu na ni utu kuwambuka wenzetu hawa,’’amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Musoma, SSP Jackson Murya ameshukuru Mahakama na wadau wake kwa misaada hiyo ya tendo jema kwani wanafungwa na mahabusu wanafarijika wanapoona jamii inawakumbuka, kuwatia moyo na kuwathamini.
“Kwa misaada hii wafungwa na mahabusu wanaguswa na watajirekebisha kwa kuona jamii inawakumbuka na kuwathamini,” amesema.
Nao wafungwa na mahabusu wa kike na kiume walioko katika Gereza Musoma wameishikuru Mahakama na wadau wake kwa kuwakumbuka kwa misaada hiyo.
Amesema misaada hiyo hasa televisheni (TV) na king'amuzi vitawawezesha kuendelea kujifunza na kupata habari za mambo mbalimbali yanayoendelea katika jamii na dunia kwa ujumla ambavyo vitawafanya waendelee kujiona sehemu ya jamii.
Naibu Msajili Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Salome Mshasha (katikati) akiwa pamoja na Mkuu wa Gereza Musoma, SSP Jackson Murya, Watumishi wa Mahakama, watumishi wa Magereza Musoma na Wadau wa Mahakama walioshiriki katika kukabidhi mahitaji ya wafungwa na mahabusu wa Gereza Musoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni