MAJAJI WATATU MAHAKAMA KUU WATEMBELEA MAONESHO WIKI YA SHERIA DODOMA
·Mtendaji Mahakama ya Rufani awa Kiongozi wa kwanza kufika Nyerere Square
·Wananchi nao waanza kujitokeza kupata elimu ya kisheria
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo leo tarehe 24 Januari, 2024 ametembelea mabanda ya maonesho ikiwa siku ya kwanza ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024 yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya ‘Nyerere Square’ jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Massabo ameambatana na Majaji wengine wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki na Mhe. Irene Msokwe kutembelea mabanda hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali.
Majaji hao kwa pamoja waliweza kukutana na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali kwenye mabanda yao kwa takribani masaa mawili. Wameonyesha kufurahishwa namna watumishi na wadau wa Mahakama walivyojipanga kuwahudumia wananchi.
Awali, Majaji hao walitanguliwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere, ambaye amekuwa wa kwanza kwa Viongozi wa juu wa Mahakama kutembelea mabanda hayo na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wake.
Sambamba na hilo, wananchi kutoka viunga mbalimbali jijini Dodoma na maeneo ya pembezoni wameanza kujitokeza kwenye maonesho hayo na kupata huduma za kimahakama na msaada wa kisheria bure.
Wananchi hao wameonekana wakihudumiwa kwa ukarimu na wadau huku wakitumia nafasi hiyo kuuliza maswali ili kupata uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria katika muktadha mzima wa utoaji wa haki nchini.
Ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria utakuwa tarehe 27 Januari, 2024 utakaofanyika kwa matembelezi maalum yatakayoanzia kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kutamatishwa katika Viwanja vya Nyerere Square. Mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo atakuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Wakati wa maonesho hayo, wadau mbalimbali watashirikiana na Mahakama katika zoezi la utoaji wa elimu na kutoa huduma mbalimbali za kimahakama. Miongoni mwa wadau hao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Elimu itakayotolewa inahusu taratibu za ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi, migogoro ya Kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.
Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo Jumuishi, watajifunza jinsi Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Januari, 2024 kuelekea kilele cha Siku ya Sheria tarehe 1 Februari, 2024 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu 2024 inasema, “"Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai."
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika Viwanja vya Nyerere Square muda mchache kabla ya kuanza kutembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria leo tarehe 24 Januari, 2024. Kutoka kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo, Mhe. Edwin Kakolaki na Mhe. Irene Msokwe. Picha tisa chini zinaonesha Majaji hao wakiwa kwenye mabanda mbalimbali.
Wananchi wakiwa katika banda la Jeshi la Polisi.
Wananchi wakipata maelezo kutoka kwenye Banda la Mahakama ya Afrika Mashariki. Picha chini wananchi wakiwa kwenye banda la Kituo hicho.
Wananchi wakiwa katika banda la Kumbukumbu na Nyaraka la Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni