Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani
Wananchi wa Wilaya ya Kibaha wajitokeza kutembelea banda la Mahakama kujionea shughuli za kimahakama katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza jana tarehe 24 Januari, 2024.
Wakati maonesho hayo yakiendelea Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai walionekana katika banda hilo wakikaribisha wageni waliotembelea banda hilo na kujionea shughuli mbalimbali za Mahakama.
Baadhi ya wananchi waliofika katika banda la Mahakama wametoa maoni yao kuhusu huduma za Mahakama na pia wamesema huduma hii iendelee ili watu waweze kujifunza zaidi maana wao wamejifunza vitu vingi kupitia maonesho hayo.
Wananachi waliotembelea leo katika banda la Mahakama ya Hakimu Mkazi wameweza kujifunza taratibu za kufungua kesi za mirathi ambapo Mhe. Honorina Kambadu ambaye ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mailimoja aliwaelewesha wananchi hao kuhusu viambatanisho katika kufungua kesi hizo kuanzia ngazi ya Mahakama ya mwanzo mpaka Mahakama kuu.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Mahakama wamekua na maoni tofauti tofauti ikiwemo kuongeza vituo vya maonesho kama vile Mahakama zote za Mwanzo ziwe na mabanda maeneo ya sokoni na shuleni, ambapo watu wengi wanapatikana katika shughuli zao ili kuwarahisishia.
Maswali mengi yaliyoulizwa yalikua yanahusu ardhi, jinai na mirathi, kutokana na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa; Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai” wananchi wamekua na maswali kuhusu muda ambao mtuhumiwa anaweza kukaa ndani (lock up) ndipo adhaminiwe.
Akijibu swali hilo Mhe. Kambadu alisema mshtakiwa anatakiwa kukaa chini ya ulinzi wa Polisi ndani ya saa 24 ndio apewe dhamana kama kosa lake linadhaminika.
Kadhalika, kwa upande wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi wananchi wameitikia wito na kufika katika maonesho hayo ambapo wamekua na maswali mengi. Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa yalihusu uendeshaji wa kesi katika na Mahakama, na kama mtu yoyote anaweza kuingia na kusikiliza shauri na pia waliuliza shauri gani ambazo mtuhumiwa haruhusiwi kudhaminiwa.
Akijibu maswali hayo Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Sharifa Mtumuyu alisema shauri linalomuhusu mtoto au shauri la ndoa hawaruhusiwi watu wasiohusika kusikiliza, pia katika mashauri ya jinai, mauaji, uhaini hayana dhamana na kuna baadhi ya kesi pia zenye dhamana lakini kutokana na sababu mbalimbali dhamana zinaweza kufungwa.
Jana ilikuwa siku ya kwanza ya maonesho ya Wiki ya Sheria ambapo maonesho hayo yanafanyika nchi nzima ambapo kwa upande wa Mkoa wa Pwani maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha na Mahakama ya Mwanzo Mlandizi.
Baadhi ya wananchi wa Kibaha wakisikiliza maelezo kutoka katika banda la Mahakama ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mhe. Honorina Kambadu na Msaidizi Wa Kumbukumbu, Bi. Tutindaga Mwankina (hawapo katika picha) wakitoa maelezo kwa wananchi hao.
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni