· Unaitwa Pocket Law; Hautumii mtandao kuupakua
· Mtendaji Mkuu asema ni mageuzi mengine ya kitehama mahakamani
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 30 Januari, 2024 amezindua mfumo maalum wa Sheria Mfukoni (Pocket Law) unaomwezesha mtumiaji kupata taarifa mbalimbali za kisheria mahali popote alipo bila kutumia mtandao.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa kabla ya kuzindua mfumo huo, ambao unaweza kupakuliwa kupitia TanzLii, Prof. Ole Gabriel amesema uwepo wa Pocket Law ni mwendelezo wa mageuzi mkubwa ya kitehama yanayotokea mahakamani.
“Kwa sasa tuna mifumo takribani 17 inayofanyakazi ndani ya Mahakama ambayo imeunganishwa pamoja ili kumrahisishia mwananchi kupata haki kwa haraka na kwa gharama nafuu au bila gharama yoyote,” amesema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mahakama kupata rasilimali zilizofanikisha mageuzi hayo.
Kadhalika, ameushukuru Uongozi wa Mahakama chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuipeleka Mahakama kwenye ngazi ya mahakama mtandao ili kuondoa mchakato mrefu wa mwananchi kupata haki.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ametoa angalizo kuwa Mahakama inaweza kufanya hayo yote, lakini jukumu lake la kutoa haki halitabaki kuwa jepesi bila mwananchi kubadilisha fikra.
Hivyo amewaomba wananchi kutamba jitihada zinazofanywa na Serikali na Mahakama katika kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha mchakato wa utoaji haki kwa kutumia njia za kidijiti.
Amesema lengo kuu ni kuwafanya wote kwa pamoja kuboresha mifumo ya utoaji haki ili kukuza uchumi, kwani pale ambapo haki inapatikana kirahisi pia ina mchango mkubwa katika uchumi, hivyo kuiwezesha Tanzania kuendelea kubaki kuwa Nchi ya uchumi wa kati na hata kupanda kuwa na uchumi wa juu.
“Tutatumia fursa hii ambayo Serikali imetupa kuhakikusha wananchi wanapata haki zao kwa wakati na wapate taarifa ambazo wanazihitaji kwa haraka,” Prof. Ole Gabriel amesmea.
Amewahimiza Watumishi wa Mahakama kuendelea kuchangamkia fursa kama hizo ambazo zinakwenda kuifanya Mahakama ya Tanzania kuwa tofauti na Mahakama zingine, siyo tu katika Ukanda wa Afrika Mashariki bali pia Bara la Afrika na Dunia nzima kwa ujumla.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema kuwa na mfumo huu ni jambo moja, lakini kutuumia ni jambo muhimu zaidi, hivyo akawaomba wale wote wanaohusika kuendelea kuutumia ili uweze kuleta matunda chanya yaliyokuwa yamekusudiwa.
“Mfumo wa TanzLii unatembelewa kwa asilimia 82.4 duniani ukilinganisha na mifumo mingine na Nchi inayofuata ambayo ni kubwa kiuchumi ina asilimia 2.7, hivyo, unaweza kuona jinsi gani mfumo wetu wa Tanzania umeiacha mbali sana mifumo mingine,” amebainisha.
Prof. Ole Gabriel amewaomba wadau wengine wa utoaji haki, kama Polisi, Magereza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Msajili Mkuu, Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine kuendelea kushirikiana.
“Ahadi yangu kama Mtendaji Mkuu wa Mahakama ni kwamba tutatoa ushirikiano wetu wote. Milango yetu ipo wazi kwa wadau wote katika mnyororo wa utoaji haki ambao wanatamani kuboresha huduma zao tuweze kufanya maamuzi kwa haraka ili mwanachi wa kawaida kule kijijini aweze kupata haki kwa urahisi,” amesema.
Awali katika maelezo yake ya utangulizi, Mratibu wa TanzLii, Mhe. Kifungu Mrisho Kariho amesema kuwa Sheria ya Mfukoni ni mpango wa kimapinduzi ambao unafafanua upya upatikanaji wa maarifa ya kisheria na utaalamu.
Amesema kuwa mfumo huo ambao hautumii mtandao utasaidia upatikanaji wa maamuzi ya Mahakama na Sheria kutoka TanzLII nje ya mtandao. TanzLII ilianza 2018 na kuna takriban maamuzi 49,000 ya Mahakama yaliyopakiwa kwenye mfumo na hufikiwa bila gharama yoyote.
“Katika siku zijazo, tutaunganisha ADCM, e-Library na TanzLII. Sheria ya Mfukoni itaruhusu upatikanaji wa sheria na maamuzi ya Mahakama kwa urahisi kutoka TanzLII na bila gharama yoyote kwa Majaji, Mahakimu na wadau hata pale wanapokuwa hawana mtandao na katika maeneo ya kazi ambayo ni mbali na miji,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taarifa za Kisheria Afrika (AfricanLII), Bi Mariya Badeva alieleza kuwa uzinduzi wa Sheria Mfukoni unaendana na dhamira ya sekta ya haki ya Tanzania ya kufanya sheria ipatikane kwa urahisi.
Alieleza kuwa Sheria ya Mfuko ni sehemu muhimu ya juhudi hizo, ikitoa suluhisho la kidijitali ambalo hurahisisha upatikanaji wa rasilimali za kisheria kwa Watanzania wote.
“Nataka kutambua maono ya uongozi wa washirika wetu, Mahakama ya Tanzania, kwa kutambua thamani ya ubunifu huu. Ushirikiano wao ni muhimu katika kuendeleza mpango huu…
“Katika siku zijazo, tunatarajia kukuza ushirikiano katika maeneo mengine ya sekta ya haki na kusambaza zana hii muhimu ya utafiti wa kisheria kwa kila mtu anayesaidia raia wa Tanzania katika masuala yao ya kisheria,” amesema.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuliwa na Bw. Muhamet Brahimi na wawakilishi wote kutoka GIZ Regional Programme- Shirika la Ujerumani kuhusu Utawala wa Sheria na Mahakama Barani Afrika, Morina Chindia kutoka LawAfrica, sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wadau wengine wa Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni