Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson amezindua rasmi Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania unaolenga kurahisisha zaidi huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Tulia amezindua Mfumo huo leo tarehe 27 Januari, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria inayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
“Naipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa ya kuleta Mfumo huu, ambao naamini utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi,” amesema Spika wa Bunge.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Tulia ametoa rai kwa Wadau wengine wa Mahakama kuendana na kasi ya Mhimili huo ili kutokwamisha mchakato mzima wa utoaji haki.
‘‘Naamini kazi kubwa sasa, hasa wadau wa Mahakama ni utengenezaji wa mfumo hasa wa kitehama, utakaowasaidia wadau hawa kufungamanisha na kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai unaosomana, ili kubadilishana taarifa kuanzia hatua ya upelelezi, ufunguaji wa mashauri, msaada wa kisheria, uendeshaji wa mashtaka, kusikiliza mashauri na utoaji uamuzi,” amesisitiza Spika wa Bunge.
Ameongeza kwa kueleza kuwa kila Mdau anao wajibu wa kufanya uwekezaji kwenye eneo la miundombinu ya TEHAMA na usimikaji wa mifumo ya kidijitali, kuajiri Wataalamu wa TEHAMA na kuwaendeleza kwa mafunzo ili waweze kusimamia na kutoa msaada wa kiufundi.
Kadhalika amesema ni muhimu Wadau kuwapa Wataalam vifaa vya kisasa vya TEHAMA ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na kuongeza ushirikiano na Wadau wa Haki ili kuharakisha huduma ya Utoaji Haki.
Akizungumza wakati akimkaribisha Spika wa Bunge kuzzindua Mfumo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama ya Tanzania imewekeza nguvu katika matumizi ya TEHAMA ambapo ametaja Mifumo mbalimbali inayolenga kurahisisha huduma ya utoaji haki kwa wananchi mojawapo ikiwa ni Mfumo Mpya wa Kielektroniki wa Kuratibu Mashauri (e-CMS).
"Ikumbukwe kwamba wananchi kwa kitambo kirefu wamekuwa wakilalamika kuhusu kuchelewa kupatikana kwa mienendo ya mashauri yao na pia kuwepo kwa mapungufu katika mienendo ya mashauri yao na pia kuwepo kwa mapungufu katika mienendo ya mashauri, ili kuondokana na kadhia hiyo, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya ALMAWAVE ya Italia imejenga Mfumo unaotumia akili mnemba (Artificial Intelligence) kufundisha lugha ya Kiswahili na Kiingereza cha Kisheria mapungufu hayo," amesema Mhe. Prof. Juma.
Amebainisha faida za Mfumo huo kuwa ni pamoja na kuwapunguzia kazi Majaji na Mahakimu kazi kubwa waliyokuwa wanaifanya ya kuandika kwa mkono mienendo ya mashauri na hivyo kuwawezesha wananchi kupata haki kwa wakati.
Akitoa maelezo mafupi kuhusu mfumo TTS, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kwa sasa Mfumo huo tayari umefungwa katika Mahakama 11 na mpango uliopo ni kufunga katika Mahakama zote nchini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuja na Mfumo huu, ambao tulijifunza na kupata utaalam kutoka nchini Italia,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu amezialika Taasisi mbalimbali za Serikali zitakazoona zinahitaji kutumia Mfumo huo kuja Mahakama kujifunza jinsi unavyofanya kazi.
Amesema mpaka sasa tayari Wataalam kutoka Bunge la Tanzania na Mahakama ya Zanzibar wameshatembelea Mahakama kwa ajili ya kujifunza kuhusu Mfumo huo.
Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaendelea Nchi nzima hadi tarehe 30 Januari, 2024 na Kilele cha Siku ya Sheria kinatarajiwa kuwa tarehe 01 Februari, 2024 ambapo kwa upande wa Dodoma ambapo maadhimisho haya yanafanyika kitaifa Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni