Jumamosi, 27 Januari 2024

TUMIENI WIKI HII KUJENGA UELEWA KUHUSU SHUGHULI ZA MAHAKAMA: MHE. MKHOI

Na. Eunice Lugiana – Mahakama, Pwani

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani Mhe. Joyce Mkhoi ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kuitumia wiki hii ya sheria kupata elimu kuhusu shughuli za kimahakama na kupata ufafanuzi kwenye masuala ya kisheria hasa kwenye mambo mtambuka yanayo izunguka jamii hiyo.


Akitoa mada kwenye kipindi maalum cha wiki ya sheria katika Radio Chalinze FM jana tarehe 26 Januari, 2024 Mhe. Mkhoi alisema, katika kipindi hiki wananchi watapata elimu bure kutoka kwa Wanasheria Mahakimu na wadau mbalimbali wa haki pasipo malipo yoyote.


Akijibu swali lililoulizwa na mwandishi katika kipindi hicho alipotaka kujua makosa yapi yanatakiwa kudhaminika na je kama mtu anaweza kijidhamini mwenyewe Mhe. Mkhoi alisema, kuna makosa ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana na kuna makosa ambayo yana dhamana lakini Mahakama imejitahidi kuweka masharti rafiki ya dhamana kwa washtakiwa ambao makosa yao yana dhamana ili kupunguza msongamano magereza.


Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo Mhe. Samera Suleiman akifafanua kauli mbiu alisema, kutokana na mapungufu yaliyokuwepo katika sheria za jinai zimepelekea kuundwa kwa tume ya kuchukua maoni kuhusu haki jinai ili kuleta usawa katika utoaji haki.


“Mfumo jumuishi  wa haki jinai unahusisha wadau wote wa haki jinai ikiwemo Ofisi ya Mashtaka ya Taifa ambapo mpaka sasa kesi zote zinasajili kwa njia ya kielekroni na kusikilizwa kwa njia hiyo japo bado wadau wengine hajaungwa na mfumo huo jitihada zinaendele kuweka mfumo jumuishi kwa wadau wote wa haki jinai na mahakama”, alisema Mhe. Suleiman.


Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai akijibu swali na msikilizaji Bakari Bonge alipotaka kujua kama mke wake amegundua ana mtu mwingine akimuacha na yeye kuoa itakua kosa? Mhe. Lukumai alisema, ni vema kama wamekubalia kuachana wafuate utaratibu wa kufungua shauri la talaka waachane kisheria maana Mahakama ndiyo chombo pekee kilichopewa mamlaka kisheria ya kuvunja ndoa iwapo itathibitika ndoa hiyo haiwezi kurekebishika.


Katika kipindi hicho Mhe. Mkhoi aliambatana na Hakimu Mkazi Mfawidi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai na Hakimu Mkazi Mfawidi wa mahakama ya Wilaya Bagamoyo Mhe. Sameera Suleiman, kuelekea uzinduzi utakao fanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Mtongani Mlandizi katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na mgeni rasmi anatarajiwa kua Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon.

Waheshimiwa Mahakimu Wakiwa Studio Za Chalinze Fm Wakati Wa Kipindi Maalum (Katikati)  Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakam Ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani  Mhe. Joyce Mkhoi (Kulia) Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama Ya Wilaya Bagamoyo Mhe. Sameera Suleiman (Kushoto)  Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama Ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai 

Waheshimiwa Na Watangazaji Wa Radio Chalinze Fm Baada Ya Kipindi Maalum Kuelekea Uzinduzi Wa Wiki Ya Sheria (Katikati )Ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mhakama Ya Hakimu Mkazi Kibaha Mhe. Joyce Mkhoi, (Kutoka Kushoto )  Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakama Ya Wilaya Bagamoyo Mhe. Sameera Suleiman   Bi. Noela Mtavangu,  Bi. Flora Macha na kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha    Mhe. Emmael Lukumai.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni