Jumatatu, 29 Januari 2024

WIKI YA SHERIA YAWAIBUA WASOMI CHUO KIKUU CHA IRINGA

Na Lusako Mwang’onda-Mahakama KuuIringa

Katika kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini, Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Iringa (zamani Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa), kimeendesha mdahalo wa wazi kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao (cybercrimes). 

Mdahalo huo umefanyika chuoni hapo na kuhudhuriwa na Wanafunzi wote wanaosoma Sheria, huku Mgeni Rasmi akiwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta.

Akizungumza na umati wa Wanafunzi wakati wa ufunguzi wa Mdahalo huo, Jaji Mugeta aliwahimiza kujijengea tabia ya kupenda kuhudhuria midahalo ya namna hiyo ili kujiongezea maaarifa. 

“Midahalo ya kitaaluma ni sehemu muhimu ya kujifunza. Niwasihi msiache kuhudhuria. Niko tayari kuwaruhusu Majaji kuja kushiriki nanyi kama midahalo hii itafanyika kwa wingi na ubora zaidi,” alisema Jaji.

 Mdahalo huo ambao pia uliohudhuriwa na Majaji wengine wote wa Mahakama Kuu Kanda ya IringaMhe. Angaza Mwipopo, Mhe. Saidi Kalunde na Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika, uliongozwa na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sheria ya TEHAMA (LLM - ICT Law) kwa ushirikiano na Wahadhiri wao.

Pamoja na mambo mengine, mdahalo huo ulijikita katika kutoa elimu ya makosa ya mtandao na namna ya kujikinga dhidi ya uhalifu mtandaoni. Wawasilishaji walitoa wito kwa wasimamizi wa Sheria kuwalenga zaidi wanawake na watoto kwa madai kuwa ni waathirika wakubwa wa matumizi mabaya ya mtandao.

Baada ya mawasilisho ya Wanafunzi, Majaji nao walichangia hoja ambapo waliwasifu Wanafunzi kwa umahiri wao na kwa mahudhurio kiasi cha washiriki wengi kufuatilia mdahalo wakiwa nje ya ukumbi maarufu chuoni hapo uitwao “Science Block.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Kikuu Iringa, Mhadhiri wa Sheria, Bi. Halima Miigo alimuomba Jaji Mfawidhi na Majaji wenzake wasichoke kufika chuoni hapo na kutoa maoni yao juu ya kuboresha taaluma ya sheria ili iendane na uhalisia wa vitendo.

Wiki ya Sheria nchini ilianza tarehe 24 Januari, 2024 na inategemea kutamatika tarehe 30 Januari, 2024, ambapo ndani ya wiki hii Mahakama ipo katika utoaji wa elimu ya sheria bure kwa Wananchi.

Elimu hiyo inatoelewa katika maeneo mbalimbali ya wazi kama sokoni, stendi, mashuleni, vyuo vya kati na vyuo vikuu.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na umati wa Wanafunzi wa Sheria na Wafanyakazi mbalimbali wa Kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu cha Iringa wakati wa Mdahalo Maalumu wa Wiki ya Sheria nchini.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa Mhe. Dkt.  Eliamani Laltaika akitoa neno wakati wa mdahalo uliofanyika Chuo Kikuu cha Iringa katika kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa wakifuatilia wasilisho la Mada ya Sheria ya Mitandao kutoka kwa mmoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa. Kutoka kushoto ni Jaji Eliamani Laltaika, Jaji Angaza MwipopoJaji Mfawidhi Ilvin Mugeta na Jaji Saidi Kalunde.

Sehemu ya umati wa Wanafunzi na Wafanyakazi mbalimbali wa Kitivo cha Sheria (juu na chini) ikifuatilia kwa makini mdahalo huo katika kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini.


Mhadhiri wa Sheria, Bi. Halima Miigo akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo kwa uongozi wa Mahakama kwa kushiriki katika mdahalo huo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni