Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba imezindua rasmi Wiki ya Sheria kwa matembezi yaliyoongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Immaculata Banzi.
Matembezi hayo ambayo yalipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa yamefanyika jana tarehe 28 Januari, 2024 kuanzia Viwanja vya Jenerali Mayunga kuelekea kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba yakihusisha Viongozi wa Mahakama, wafanyakazi, wadau wa Mahakama na wananchi kwa ujumla.
Baada ya matembezi hayo kuwasili katika Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba Mhe. Banzi alimuongoza Mhe. Mwasa kutembelea mabanda yaliyoandaliwa na Mahakama kwa kushirikiana na Wadau na kujionea namna washiriki walivyojipanga katika zoezi la utoaji elimu.
Taasisi zilizotembelewa katika mabanda hayo ni Mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa, Chama cha Wanasheria Tanganyika Mkoa (TLS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Ofisi ya Huduma kwa Jamii Mkoa, Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa, Wakala wa Huduma za Misitu na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Banzi amewaalika wananchi wote kufika Mahakama Kuu Bukoba na kutembelea mabanda ambayo yameandaliwa ili kupata elimu mbalimbali ya kisheria.
Mhe. Banzi amesema, “Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mahakama kwa kushirikina na Wadau tumefanya zoezi la utoaji wa elimu kuanzia tarehe 24 Januari, 2024. Wananchi wameweza kufika na kufaidika na elimu iliyotolewa katika viwanja hivi vya Mahakama Kuu, Viwanja vya Lubale na Kemondo ambapo elimu ya Sheria imekuwa ikitolewa kila siku.”
Naye Mkuu wa Mkoa ameipongeza Mahakama kwa Kauli Mbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ambayo ni: “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa Haki Jinai.”
Mhe. Mwasa amesema: “Mheshimiwa Jaji Mfawidhi, umenitaarifu kuwa kwa sasa kwa hatua ya Mahakama Kuu, mtaanza mfumo wa usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia ya kunukuu usikilizwaji wa mashauri na kutafsiri kutoka kwenye sauti kwenda kwenye lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza [Translation and Transcription System (TTS)].
“… Mfumo huu una faida nyingi, mosi, Mashauri yatasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati na pili mfumo huo utaimarisha utunzaji na utasaidia upatikanaji wa kumbukumbu za Mahakama kwa wakati.”
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Immaculata Banzi akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua rasmi Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Kagera.
Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa akihutubia Wananchi na Wadau wa Mahakama katika Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba (kulia aliyevaa miwani), Mhe. Immaculata Banzi akiwaongoza Majaji na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Bukoba pamoja na wadau wengine wa Mahakama katika matembezi ya ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria mkoani Kagera.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa akipokea matembezi ya kuadhimisha ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Kagera.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Odira Amworo (kulia) na Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko (katikati) wakiwa katika matembezi ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria.
Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na Wadau wakiwa katika matembezi kuelekea katika Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu Iman Mzumbwe kutoka Songwe anaripoti kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe imezindua Wiki ya Sheria na kushuhudiwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Ufunguzi rasmi wa maadhimishao hayo ulifanyika katika Wilaya Mbozi mkoani Songwe katika mamlaka ya mji mdogo Mlowo huku wanacnhi wakijitiokeza kwa wingi kupata elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria.
Akizungumza katika hafla hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube aliwaomba wananchi katika Mkoa huo kutumia nafasi hiyo ili waweze kunufaika na elimu inayotolewa wakati wa Wiki ya Sheria katika Mahakama zote zilizopo.
Aliwapongeza Wadau wa Mahakama kutoka katika Taasisi zinazoshiriki katika utoaji elimu kwa wananchi na kuwaomba kuendeleza ushirikiano huo ili kupeleka elimu yenye tija kwa kwa manufaa ya ustawi wa Taifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe, Solomon Itunda aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utoaji haki kwa wakati kwa wananchi kupitia kesi mbalimbali zinazoletwa mahakamani na kuwasisitiza wananchi wa Mkoa wa Songwe kutopitwa na fursa hiyo ya utoaji elimu ya sheria kupitia mabanda mbalimbali yaliyopo katika eneo hilo.
Aidha, amezipongeza Taasisi zilizojitokeza ambazo ni Mamlaka Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Chama cha Mawakili Tanganyika, TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na Huduma za Uangalizi Kwa Jamii.
Watumishi pamoja na wadau wa Mahakama wameshiriki matembezi hayo ya kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyoanzia katika Mahakama ya Mwanzo Mlowo kuelekea katika stendi ya mabasi ya Mji Mdogo wa Mlowo na kupokelewa Mkuu wa Wilaya Songwe.
Watumishi na Wadau wa Mahakama Mkoa wa Songwe wakianza matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda akisaini kitabu cha wageni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube akifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati ufunguzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda akikagua mabanda ya watoa elimu katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria.
Sehemu ya Meza Kuu katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nalyelye wakishiriki katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria.
Watumishi wa Mahakama wakifuatilia mamboa mbalimbali katika maadhimisho hayo.
(Haberi sizi zimehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni