Jumanne, 6 Februari 2024

IRINGA MPYA CHINI YA JAJI MUGETA

Na LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama KuuIringa.

·      Ateua kamati tatu kusaidia utendaji

·      Ahimiza mazoezi kwa watumishi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta ameunda kamati tatu za kumsaidia katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kila siku na usimamizi wa shughuli zingine za kikanda ambazo zitakuwa zinaripoti kwake. 

Mhe. Mugeta amezitaja kamati hizo, ambazo amezitambulisha rasmi kwa watumishi wote wa Mahakama Kuu Iringa, ni Kamati ya Kusukuma Mashauri, Nidhamu na Malalamiko ambayo itaongozwa na Jaji Angaza Mwipopo.

Pia kuna Kamati ya Mazingira, Michezo na Huduma za Jamii itakayoongwa na Jaji Saidi Kalunde na Kamati ya Elimu na Mafunzo itakayoongozwa na Jaji Dkt. Eliamani Laltaika.

Akitangaza kuundwa kwa kamati hizo wakati wa kikao cha Watumishi kinachofanyika kila Ijumaa, Jaji Mfawidhi aliongeza kuwa Wasaidizi wa Kisheria wa Majaji husika watakuwa Makatibu wa Kamati hizo. 

Watumishi kwa upande wao wamemshukuru Mhe. Mugeta kwa ubunifu wa kuunda kamati hizo katika kuhakisha masuala ya msingi ya kanda hiyo yanakwenda mbele, huku wakipendekeza kuongezwa kwa wajumbe watatu katika kila kamati.

Katika hatua nyingine, Jaji Mugeta amewataka watumishi kujijengea tabia ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao. “Nawatia shime kila mmoja ajizoeze tabia ya kutembea walau hatua 4,000 kwa siku. Ukiweza kufikisha hatua 10,000 itakuwa bora zaidi,” amesema.

Jaji Mugeta ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukata keki kuashiria kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa mwezi Desemba na Januari kwa Watumishi wanaohudumu katika kanda hiyo

“Hapa wote tumekula sukari. Wataalam wa afya wanashauri kufanya mazoezi ili kuunguza sukari kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa. Mazoezi ndiyo njia pekee ya kuondoa hizi sukari tunazozipata kupitia keki hizi ambazo tumejiwekea utamaduni wa kuzila kila mwisho wa mwezi tukikumbuka kuzaliwa kwa ndugu zetu, alisisitiza.

Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa chini ya Jaji Mfawidhi umebuni utaratibu wa kuwa na keki ya pamoja kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya maadhimisho ya siku za kuzaliwa kwa watumishi wote katika kipindi husika. Hii ikiwa katika kuwaweka pamoja watumishi ili kujenga umoja, mshikamamo na upendo baina yana Viongozi.




Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta, akiwa pamoja na Majaji wote wa Mahakama Kuu Iringa, akizungumza na watumishi (hawapo pichani) nje ya jengo la Mahakama Kuu Iringa. Kushoto kwa Mhe. Mugeta ni Mhe. Angaza Mwipopo, Mhe. Said Kalunde na Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika.

Watumishi waliozaliwa mwezi Januari wakikata keki kwa pamoja katika kuadhimisha mwezi wao wa kuzaliwa.

Watumishi waliozaliwa mwezi Desemba wakikakata keti kwa pamoja katika kuadhimisha mwezi wao wa kuzaliwa.

Mmoja wa watumishi waliozaliwa mwezi Desemba, Bw. Dennis Kasigara ambaye ni Mlinzi akimlisha keki Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Angaza Mwipopo katika tafrija iliyofanyika nje ya jengo la Mahakama Kuu Iringa.

Watumishi wakilishana keki. Pichani (mbele) ni Mkaguzi wa Ndani wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bw. Dominic Ketsia akimlisha keki Kaimu Mtendaji wa Mahakakama Kuu Iringa, Bi. Dorisi Kisanga.

Watumishi wakilishana keki wakati wa hafla ya kuwapongeza wazaliwa wa mwezi Desemba na Januari mbele ya jengo la Mahakama Kuu Iringa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni