Jumatano, 7 Februari 2024

JAJI MKUU WA TANZANIA ASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA SHERIA ZANZIBAR

Na Mary Gwera-Mahakama, Zanzibar

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 07 Februari, 2024 ameungana na wananchi wa Zanzibar, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushiriki katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Visiwani humo. 

Mhe. Prof. Juma pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania alioambatana nao wameshiriki maadhimisho ya Siku hiyo katika Viwanja vya Mahkama Kuu ya Zanzibar iliyopo eneo la Tunguu Mkoa wa Kusini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameziagiza Taasisi za Sheria Visiwani humo kuhakikisha kuwa, mchakato wa utungaji Sheria ya kuundwa kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi unakamilika haraka iwezekanavyo.

“Katika salaam za Jaji Mkuu wa Zanzibar, ameeleza kuwa, agizo langu la kuundwa kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi limeanza kufanyiwa kazi na kwa sasa rasimu ya Sheria hiyo imeshaandaliwa, hivyo ni naagiza mchakato huo kukamilika mapema,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Katika hotuba yake, Rais Mwinyi amekiri kufurahishwa na Kauli Mbiu ya Siku ya Sheria isemayo ‘Mazingira bora ya kazi, maadili, uwazi na uweledi huashiriab upatikanaji wa haki, huvutia uwekezaji na ukuaji wa uchumi.’ 

“Nimefurahishwa sana na Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Sheria, hivyo tunapaswa kufahamu kuwa, kwa sasa nchini mwetu kumekuwa na ongezeko la wawekezaji ambao wanawekeza katika Sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa mahoteli, viwanda na kadhalika, utekelezaji wa mambo yote hayo lazima uende sambamba na mifumo mizuri ya upatikanaji wa haki itakayohakikisha kuwa, haki inapatikana kwa haraka na kwa uwazi, kwa urahisi na kwa ubora wa hali ya juu,” amesisitiza Rais Mwinyi.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inasisitiza kuhusu matumizi ya njia mbadala ya utatuzi wa migogoro (Alternative Dispute Resolution) kwa kuwa hurahisisha umalizikaji haraka wa mashauri pamoja na kuondoa uadui kwa wadaawa kwani humfanya kila mdaawa kuwa mshindi wa kesi (win-win situation).

 Akizungumza na wananchi kupitia maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Mwinyi amepongeza pia ushirikiano uliopo kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama Zanzibar. Amesema kitendo ya Jaji Mkuu wa Tanzania na ujumbe wake kufika Zanzibar na kuhudhuria maadhimisho hayo ni dalili tosha za kuimarika kwa ushirikiano.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa katika mwaka uliopita 2023, Mahkama ya Zanzibar iliendesha jumla ya mashauri 11,817 yaliendeshwa na Mahakama ambapo kati ya mashauri hayo, mashauri ya jinai yalikuwa 6,944 na mashauri ya madai yalikuwa 4,873.

“Mhe. Mgeni Rasmi katika kipindi hicho, mashauri 8,353 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi saw ana asilimia 70.7 ambapo mashauri yanayoendelea Mahkamani ni 3,464, aidha mchanganuo wote wa hali ya usikilizaji wa mashauri kwa Mahkama mbalimbali za Zanzibar umeelezwa kwa kina katika ripoti ya utendaji kazi,” amesema Jaji Mkuu huyo.

Hata hivyo, Mhe. Abdalla amesema kuwa, ufanisi katika shughuli za Mahkama na utoaji wa haki unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa fedha za kutosha, ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mahkama ilipangiwa kutumia jumla ya shilingi 12,911,500,000/- kwa kazi za kawaida na katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari 2024 imepanga kutumia jumla ya shilingi 8,835,663,000/- na hadi kufikia mwezi huu Mahkama imeingiziwa jumla shilingi 6,858,781,963 sawa na asilimia 77.6.
  
Katika kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya Mahkama yenye lengo la kuboresha huduma za utoaji haki, Mahkama ya Zanzibar imekamilisha kutayarisha Mpango Mkakati wa miaka mitano (2024/2025-2028/2029) ambao utakuwa muelekeo wa Mahkama hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Mhe. Abdalla ameeleza kuwa, kwa mwaka huu Mahkama ya Zanzibar imedhamiria kutia mkazo katika kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha ujenzi wa majengo saba (7) ya Mahkama ulioanza mwaka uliopita, kuendeleza ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa majukumu.

Vingine ni kuendelea kusimamia kwa ukamilifu nidhamu na maadili kwa watumishi wa Mahkama na Mawakili wa Kujitegemea, kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na kutolewa uamuzi, kuendelea na maboresho kwa kufanya kazi kwa uwazi na kutoa huduma bora kwa wananchi na mengine. 

Maadhimisho hayo yalipambwa kwa shamrashamra kadhaa ikiwemo igizo, mashahiri, kadhalika Rais Mwinyi pia amezindua Mpango Mkakati wa Mahkama ya Zanzibar. Vilevile, katika hafla hiyo Viongozi mbalimbali walipewa nafasi ya kuwasilisha salamu, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashtaka Visiwani humo.

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria maadhimisho hayo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.  Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda, Kaimu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na Wasaidizi wa Viongozi hao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) pamoja na Meza Kuu wakiimba wimbo wa Zanzibar kabla ya kuanza kwa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Visiwani humo leo tarehe 07 Februari, 2024 katika Viwanja vya Mahkama Kuu katika eneo la Tunguu Mkoa wa Kusini. Wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa tatu kulia Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa tatu kushoto ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid, wa kwanza kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman na wa pili kushoto ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Bi. Mariam Mwinyi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) na Viongozi wengine wakimsalimia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipowasili leo tarehe 07 Februari, 2024 katika Viwanja vya Mahkama Kuu Zanzibar kushiriki katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria visiwani humo. 
 Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (mbele) akiwaongoza Majaji kwenye maandamano ya Siku ya Sheria Visiwani humo. Nyuma yake ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifuatiwa na Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar.
 Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar na sehemu ya Watumishi wa Mahkama Zanzibar wakiwa kwenye hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria leo tarehe 07 Februari, 2024.
Viongozi kutoka Mahakama ya Tanzania wakiwa katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Msajili Mkuu ambaye pia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylvester Kainda, katikati ni Kaimu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza na kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.
Sehemu ya wananchi wakifuatilia yalikuwa yakijiri wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar leo tarehe 07 Februari, 2024 katika viwanja vya Mahkama Kuu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wananchi wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Visiwani humo.
 Jaji Mkuu wa Zanzibar akihutubia watumishi wa Mahkama na wananchi walioshiriki katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria visiwani humo.
Wananchi wakifuatilia yanayojiri wakati wa hafla ya Siku ya Sheria Zanzibar leo tarehe 07 Februari, 2024.
Viongozi mbalimbali wakiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar leo tarehe 07 Februari, 2024.
Majaji, Watumishi wa Mahkama Zanzibar pamoja na wageni waalikwa wakiwa katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria Visiwani humo leo tarehe 07 Februari, 2024.
Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahkama Kuu Zanzibar pamoja na Ma Kadhi.
Meza kuu katika picha ya pamoja na Mawaziri kutoka Wizara mbalimbali Visiwani Zanzibar.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania (waliosimama nyuma) na sehemu ya Majaji wastaafu.
Jaji Mkuu wa Zanzibar akikagua gwaride maalum kuashiria uzinduzi wa shughuli za Mahkama Zanzibar kwa mwaka huu 2024.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama, Zanzibar)























Hakuna maoni:

Chapisha Maoni