Jumanne, 6 Februari 2024

MAHAKAMA, POLISI WAWEKA MIKAKATI KURAHISISHA HAKI JINAI

Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya hivi karibuni alikutana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase na kuweka mikakati mbalimbali itakayo rahisisha utendaji kazi wa kila mmoja kuhakikisha upatikanaji haki jinai kwa wakati.

Katika kikao hicho kilichofanyika Ofisini kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Mtulya alilipongeza Jeshi la Polisi kwa utendaji wake mzuri kama wadau wakubwa wa haki jinai unaoisaidia Mahakama kufanya kazi kwa amani. 

Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa, Mahakama Kanda ya Musoma ilijiwekea mkakati wa Mahakama zake za Mwanzo kutovuka mwaka 2023 zikiwa na Mahabusu na jambo hilo limefanikiwa ili kuwapunguzia mzigo wadau wa Jeshi la Magereza.

Naye Kamanda Morcase aliipongeza Mahakama kwa utendaji kazi mzuri, ikiwemo usikilizaji wa mashauri kwa kazi nzuri uliopelekea kupungua kwa malalamiko, jambo lililosaidia wahalifu kupata haki zao kwa wakati, kupunguza mahabusu katika Magereza. 

Kupitia kikao hicho, Viongozi hao wawili waliweka mikakati mbalimbali ya kiutendaji kwa mwaka 2024 ili kuhakikisha vyombo vyote viwili vinaboresha zaidi mahusiano yao ili mwananchi aweze kupata haki yake kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Jaji Mfawidhi amefanya kikao cha tathmini ya Wiki ya Sheria pamoja na kutoa vyeti vya shukrani kwa Wadau walioshiriki katika maonesho na utoaji wa elimu kuanzia tarehe 24 hadi 30 Januari, 2024.

Wadau hao wameishukuru Mahakama kwa mwaliko katika utoaji wa elimu ambapo wananchi walifikiwa na kupewa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria. 

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) na viongozi wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Naibu Msajili, Salome Mshasha (wa pili kulia), Naibu Msajili, Mhe. Monica Ndyekobora (wa kwanza kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Bw. Festo Chonya (wa pili kushoto) wakiongea na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Salim Morcase (wa kwanza kulia) Ofisini kwa Jaji Mfawidhi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) na Viongozi wa Mahakama Kuu Musoma, Naibu Msajili, Mhe. Salome Mshasha (wa kwanza kushoto), Naibu Msajili, Mhe. Monica Ndyekobora (wa kwanza kulia) na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Festo Chonya (wa pili kushoto) wakiongea na Wadau (hawako pichani) walioshiriki katika maonesho ya Wiki ya Sheria na utoaji wa elimu katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akimkabidhi cheti cha shukrani ya ushiriki katika Wiki ya Sheria Wakili Godwilly Mweya kutoka Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS).


Wadau walioshiriki katika maonesho ya Wiki ya Sheria na utoaji wa elimu katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya katika kikao cha tathmini kilichofanyika uwanjani hapo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)




 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni