Na Amani Mtinangi- Mahakama Kuu Tabora
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi amewaongoza watumishi, wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama mkoani Tabora katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika Viwanja vya Mahakama hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Mambi ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo iliyofanyika jana tarehe 01 Februari, 2024, alisema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Tanzania inaipa Mahakama Mamlaka ya utoaji haki na Dira ya Mahakama inatambua kuwa haki inapaswa kutolewa kwa wakati na katika kutekeleza hilo Mahakama kwa kiasi kikubwa inategemea mifumo ya TEHAMA ambayo imesaidia kupunguza mashauri, kuokoa muda wa Mahakama, wananchi na wadau kwa kurahisisha utendaji kazi.
“Mahakama ya Tanzania ni chombo pekee chenye mamlaka ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba ya Katiba na kwa kiasi kikubwa inategemea mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi wake wa kila siku ambao imesaidia kupunguza mashauri, kuokoa muda wa Mahakama, wananchi na wadau kwa kurahisisha utendaji kazi,” alisema Jaji Mambi.
Katika Hotuba yake, Mwanasheria Mfawidhi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Idd Mgeni aliishukuru Mahakama kwa kuendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu na ushauri wa kisheria kupitia maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kuwasihi wadau wa Sheria kuendela kushirikiana kuelimisha umma.
“Kwa dhati tunapenda kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana kikamilifu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wadau kutoa ushauri kwa kisheria wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria. Ninawasishi wadau wengine wa Sheria kuendelea kushirikiana kutoa elimu kwa Umma.” alisema Wakili Mgeni.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. Batilda Buriani aliipongeza Mahakama kwa kazi nzuri ya kuonesha kwa vitendo haki ikitendeka bila kuchelewa na kusifu na usimamizi bora wa matumizi ya TEHAMA.
“Niwapongeza sana Mahakama kwa kufanya haki ikionekana kutendeka na kutochelewesha mashauri ya Madai kwa sasa Mahakama haicheleweshi hasa baada ya kuboresha na kusimamia matumizi ya TEHAMA,” alisema Mhe. Dkt. Buriani.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mkoani Tabora Wakili Kelvin Kayaga, alisema Chama hicho kitaendelea kutoa msaada wa kisheria kwa watu wote wasiojiweza kiuchumi na kuendelea kupokea mashauri yanayopangwa na Mahakama kwa ajili ya vikao vya Mahakama Kuu.
“Tutaendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiojiweza kiuchumi na kupokea mashauri kwa ajili ya vikao vya Mahakama Kuu kama jukumu mojawapo la Chama chetu,” alieleza Wakili Kayaga.
Baada ya maadhimisho hayo kuisha, Mahakama ilisikiliza shauri lake la kwanza katika kikao kilichohudhuriwa na Majaji wa Mahakama Kuu, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Waandishi wa Habari na wananchi kwa jumla.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akikagua gwaride la heshima jana tarehe 01 Februari, 2024 lililoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kuashiria uzinduzi wa mwaka mpya wa Mahakama.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu imeungana na Mahakama nyingine nchini kuiadhimishi Siku ya Sheria ambapo kwa Mkoa huo Mgeni Rasmi alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga aliyeambatana na Mgeni maalum ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Wadau kutoka Taasisi mbalimbali wakiwemo Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea ambao walipata wasaa wa kuwasilisha hotuba na salaam zao mbele ya Mgeni rasmi.
Katika hotuba yake Mgeni rasmi, Mhe. Mahumbuga alieleza mchakato wa haki jinai namna unavyofanya kazi ambapo alisema kuwa, “haki jinai hupitia hatua muhimu ambazo zinahusisha Mahakama na Wadau, hatua hizo ni pamoja na uchunguzi, upelelezi na kukamatwa kwa washukiwa unaofanywa na wachunguzi, wapelelezi na wakamataji ambapo wahusika wa mchakato huo wote ni Mahakama na wadau wake.”
Kwa upande wake Mgeni Maalum, Mhe. Simon Simalenga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliwapongeza watumishi wa Mahakama kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha mchakato mzima wa utaoji haki unafanyika. “Niwaombe wadau wa Mahakama mtende haki bila kumuonea mtu kwani itampendeza Mungu na wanadamu pia,” alisema Mhe. Simalenga.
Mhe. Simalenga alisema kuwa, pale watumishi wa Mahakama wanapotaka kutoa elimu kwa wananchi yupo tayari kutoa ushirikiano kwa asilimia 100 ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa aliwashukuru wadau kwa kujitoa kwao kuja kujumuika nao, na kusema kuwa, huo ni upendo na mshikamano wa dhati kwani wameacha majukumu yao na kuja kujumuika nao katika Siku hiyo muhimu.
Mhe. Simalenga aliwapongeza watumishi wa Mahakama kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha mchakato mzima wa utoaji haki unafanyika. “Niwaombe Wadau wa Mahakama mtende haki bila kumuonea mtu kwani itampendeza Mungu na wanadamu pia.” alisema Mhe. Simalenga.
Mgeni Rasmi ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, Watumishi na Wadau kutoka Taasisi mbalimbali walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 01 Februari, 2024.
Mgeni Rasmi akisoma hotuba mbele ya Viongozi, Watumishi wa Mahakama na Wadau waliohudhuria sherehe ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 01 Februari, 2024.
Mgeni Maalum akitoa salaam za Serikali mbele ya Watumishi wa Mahakama, Wadau na wananchi katika Siku ya kilele cha Sheria mkoani Simiyu.
Kwa upande wa MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI SINGIDA, Mwandishi wetu Eva Leshange anaripoti kwamba;
MKUU WA MKOA SINGIDA ASISITIZA WANANCHI KUFUATA SHERIA
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaasa wananchi wa Singida kufuata sheria mbalimbali za nchi ili kuepuka kukinzana nazo.
Mhe. Serukamba ambaye alikuwa Mgeni wa heshima katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika Mkoa huo jana tarehe 01 Februari, 2024 alisema kuwa, “ndugu wananchi hatuna budi kufuata kanuni na taratibu za sheria za nchi ili tusiingie matatani, tumieni majukwaa ya kisheria kufahamu sheria mbalimbali za nchi, kutokujua sheria hakukukingi na kutochukuliwa hatua.”
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuweka Haki kama kipaumbele muhimu cha Taifa kwani Taifa lisilo na Haki ni vigumu kupata maendeleo na Amani, pia amewataka wadau wote wanaoshirikiana na Mahakama kutekeleza wajibu wao kuepuka kuchelewesha Haki za wananchi.
Naye Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida, Bi. Mercy Ngowi katika taarifa yake ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuhakikisha inashughulikia changamoto mbalimbali za mifumo ya utoaji Haki Nchini.
Bi. Mercy ameipongeza pia, Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ambayo imekua chachu katika kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati.
Ameahidi Ofisi ya Mashtaka itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha na kuendesha kesi bila uoga wala upendeleo.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa kujitegema Bw. Cosmas Luambano katika taarifa yake amesisitiza kila mtu ana jukumu la kulinda haki ya mwenzake, ambapo amesema kwamba, kuwa katika Taasisi fulani au kuwa na mamlaka sio kigezo cha kuvunja sheria na kunyima haki za watu.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe Allu Nzowa amewashukuru wadau wa Haki Jinai mkoani Singida kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa.
Amesisitiza Wadau kuwekeza katika vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya TEHAMA ili mifumo baina ya Taasisi iweze kusomana.
"Wadau wa Mahakama, ninyi ni watu muhimu sana katika mnyororo wa utoaji haki ni vema kuboresha miundombinu ya TEHAMA katika Taasisi zenu ili kuendana na kasi ya Mahakama,” alisema Mhe. Nzowa.
Aidha aliongeza kwamba, wadau kutokuwa na mifumo jumuishi ya Haki jinai kutasababisha ucheleweshwaji wa Haki, wananchi watakosa muda wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi na kuongeza urasimu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni