Ijumaa, 2 Februari 2024

YALIYOJIRI MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA KATIKA KANDA NA MIKOA

Jana tarehe 01 Februari, 2024 ilikuwa ni maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, maadhimisho hayo yalifanyika Kitaifa, katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Kadhalika maadhimisho ya Siku hiuyo yalifanyika nchi nzima ambapo Wawakilishi wetu wanatujuza yaliyojiri katika shamrashamra za kuadhimisha Siku hiyo;

Mwandishi wetu Seth Kazimoto kutoka MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA ARUSHA anaripoti kuwa; 

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imeungana na Mahakama nyingine nchini kuadhimisha Siku ya Sheria tarehe 01 Februari, 2024 katika eneo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC). 

Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga ambaye amewaasa wadau kuwatendea haki wananchi na kuleta ustawi wa jamii.

Akizungumza katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Mhe. Tiganga alisema kuwa, Mahakama na Wadau wametoa elimu kwa wananchi wapatao 194,405, ambapo wananchi 516 wamepatiwa msaada wa kisheria kupitia Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Wananchi 193,889 wamepatiwa elimu kwa kutembelea shule, Vyuo na Serikali za Mitaa. 

“Kwa kushirikiana na wadau, Mahakama imepiga hatua kubwa kumaliza mashauri kwa wakati na kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani. Ukaguzi wa hivi karibuni gerezani Arusha ulibaini kuwepo jumla ya wafungwa na mahabusu 704. Kati ya hao 492 sawa na asilimia 70 ni wafungwa na 212 sawa na asilimia 30 ni mahabusu,” alisema Mhe. Tiganga. 

Kadhalika, Jaji Mfawidhi ameongeza kuwa, uangaliwe uwezekano wa kuunganisha mifumo ya Wadau kama NIDA na ile ya Mahakama ili kuwe na urahisi wa kupata taarifa baina ya Taasisi moja na nyingine. Amesisitiza kuwa iwepo mifumo inayoshirikiana pamoja baina ya wadau bila kuingiliana katika majukumu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela ameishukuru Mahakama kwa kuweka utaratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambapo huwakutanisha wadau mbalimbali na kujadiliana kwa kina katika kuhakikisha kwamba shughuli ya utoaji haki inafanyika kwa ufanisi zaidi. 

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS) mkoani Arusha, Wakili Msomi Geoge Njooka pamoja na kuishukuru Mahakama mkoani humo, ameiomba Mahakama kufanya mafunzo zaidi kwa Mawakili wa Kujitegemea juu ya mifumo ya TEHAMA ya Mhimili huo ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila vikwazo.

Mhe. Tiganga amehitimisha kwa kuwashukuru wananchi na wadau waliohudhuria sherehe hizo kipekee Viongozi wa Dini mkoani Arusha kwa ushiriki wao katika masuala ya kimahakama hususani usuluhishi wa migogoro ya ndoa. Amewaomba wasichoke kuendelea kutoa ushirikiano huo pindi Mahakama inapowahitaji.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na watu na Taasisi mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wananchi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, TAKUKURU, Viongozi wa Dini, Mawakili wa Kujitegemea, Shule na Vyuo. Ushiriki wa wananchi na wadau ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya Mahakama na Wadau.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini jana tarehe 01 Februari, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 01 Februari, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela (katikati) na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo wanaosoma kozi ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini jana tarehe 01 Februari, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Fredrick Lukuna (kulia),  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya  Arusha, Mhe. Mariam Mchomba (kushoto)  na Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Leonard Maufi  (katikati)  wakisimamia shughuli za maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini zilizofanyika jana tarehe 01 Februari, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mkoa wa Arusha, Wakili Msomi George Njooka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 01 Februari, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa Mahakama waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania yaliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 01 Februari, 2024.                                                                                                                                       Kwa upande wa MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA, Mwandishi wetu Charles Ngusa, anaripoti kuwa,

Katika kuhitimisha kilele cha wiki ya Sheria nchini Mkoani Geita, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina amewashukuru wadau wote na wananchi kwa ujumla kwa namna walivyoitikia tangu siku ya kuanza kwa maonesho ya Wiki ya Sheria hadi kilele cha Siku ya Sheria, 2024.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama hiyo jana tarehe 01 Februari, 2024, Mhe. Mhina alisema wadau wamejitoa kwa kiasi kikubwa hivyo amewapongeza kwa ushirikiano wao.

Jaji Mfawidhi huyo pia amezungumzia ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Jumuishi (IJC) ambapo amesema kuwa ujenzi huu utakuwa kichocheo kikubwa sana katika mfumo wa upatikanaji wa haki kwa kuwa jengo hili litajumuisha ngazi zote za Mahakama kama vile Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Akielezea historia ya dhana ya Haki, Mhe. Mhina amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama mnamo mwaka 1920, Mahakama ilikuwa na Majaji wawili pekee wa Mahakama Kuu ambapo upatikanaji wa haki ulikuwa ni mgumu sana na watu walilazimika kusafiri umbali mrefu sana kuifuata haki tena kwa kutembea kwa miguu kwenda maeneo kama ya Mikoa ya Dodoma, Tabora na Kigoma. 

“Baada ya uhuru kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, Upatikanaji wa haki umeboreshwa zaidi kutokana na maboresho ya mifumo ya Mahakama ambayo mpaka sasa tunaendelea kuitumia na kuiboresha zaidi na zaidi,” alisema Jaji Mhina. 

Aidha, Jaji Mfawidhi amesisitiza kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa haki ambapo amesema ili mfumo wa upatikanaji wa haki uweze kutekelezwa kwa ufasaha, ni lazima wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa utoaji haki watekeleze wajibu wao kwa ufasaha pasiwe hata mmoja wao kulegalega.

Amewataja Wadau hao ambao ni pamoja na Ofisi ya Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Polisi, Magereza na Wadau wengine wote wanaohusika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela amesisitiza Wananchi na wadau kwa ujumla kuuheshimu Mhimili wa Mahakama.

“Mahakama ndicho chombo pekee chenye mamlaka kisheria juu ya utoaji haki  na wengine ni watekelezaji tu wa amri za Mahakama na hivyo tujitahidi kuheshimu hilo,” alisema Mhe. Shigela.

 Mkuu wa Mkoa huyo alisema wako baadhi wanakwamisha, wako baadhi wanataka kujadili uamuzi wa Mahakama, wako baadhi wanataka kutafsiri hukumu iliyotolewa na Mahakama, “nitumie nafasi hii kuwaelekeza watumishi wote wa Serikali  katika Mkoa huu wa Geita  kuanzia ngazi ya Kitongoji  mpaka kwangu Mkuu wa Mkoa  kuwa ni marufuku kuzuia utekelezaji wa tuzo zinazotolewa na Mahakama.”

Akisoma taarifa kwa niaba ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili wa Kujitegemea, Beatus Emmanuel ameishukuru Mahakama kwa kuendelea kuwatambua kama wadau muhimu katika mnyororo wa upatikanaji wa Haki. 

“Kama Chama cha Wanasheria, pamoja na jukumu lao kuu la kuwatetea wateja wao mbele ya Mahakama, wanalo pia jukumu kuu la kuwaelimisha wananchi juu ya kutambua haki zao kwani ndicho kichocheo kikubwa cha uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa urahisi, ni muhimu Mahakama zetu zikawezeshwa rasilimali na teknolojia bora na ya kisasa kwani inarahisisha kazi na kuboresha  mfumo wa uwazi na uwajibikaji,” alisema Wakili Emmanuel.

Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Geita, Bw. Godfrey Odupoy alisisitiza kuhusu ushirikiano ambapo alisema Mahakama pekee haiwezi kutekeleza jukumu lake la msingi la utoaji haki hivyo ni lazima wadau wote wa haki jinai washiriki ikiwemo Ofisi ya Mashtaka.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akiwasilisha hotuba yake wananchi na wadau wakati hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika jana tarehe 01 Februari, 2024 katika viwanja vya Mahakama hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akitoa salamu za Serikali mbele ya wananchi waliohudhuria katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria jana tarehe 01 Februari, 2024.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Geita, Bw.Godfrey Odupoy akiwasilisha hotuba wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Mwakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mkoani Geita, Wakili Beatus Emmanuel akisoma hotuba kwa niaba ya chama hicho.

Watumishi wa Mahakama wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Wadau na wananchi wakifuatilia hotuba wakati wa Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mwandishi wetu Aidan Robert anatujuza kuwa, 

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, ameongoza maandamano ya kitaluma katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria katika viwanja vya Mahakama hiyo, Jaji Rwizile amesema ametoa rai kwa wadau wa Mnyororo wa haki jinai kushirikiana na wananchi ili kuwahisha utoaji haki mahakamani.

“Utoaji haki huanzia pale tu taarifa inapotolewa kutoka kwa wananchi hata hivyo, wananchi wanawajibika kuusimamia mnyororo wa utoaji haki, katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8 na ibara ndogo ya 1 (a), inasema wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi,” kwahiyo wananchi hatupaswi kuvumilia vitendo viovu vinavyofanywa katika jamii yetu,” amesema Mhe. Rwizile.

Aidha, Jaji Rwizile aliendelea kusema kuwa, wananchi watoe taarifa maana wasipotoa taarifa watafanya mnyororo wa haki jinai kutofanya majukumu yake vema, hivyo kama jamii inapaswa kujiuliza kama wanatimiza majukumu hayo.

 Aidha, alibainisha kuwa Vyombo Upelelezi (Polisi, Takukuru na vinginevyo) kimsingi ndio vimeachiwa jukumu la kutafuta taarifa za uhalifu na kuzifanyia kazi na kukamata, kushitaki mtuhumiwa mahakamani wakishirikiana na Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka, hapo Mahakama ndio inasikiliza na kutoa hukumu.

“Kwakuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga nchi na jamii inayozingatia misingi ya Uhuru, Haki, Udugu, Amani na kwakuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa kwenye jamii yenye Demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe walio chaguliwa linalowakilisha wananchi na pia lenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wake wa  kutoa haki bila woga, upendeleo wowote na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu’ alisema Jaji Rwizile.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mhe. Baraka Msahuzi, akitoa salaam za Serikali, aliipongeza Mahakama Kuu Kanda hiyo kwani  Serikali  inaridhishwa na utendaji kazi wa Mahakama  hiyo na kuongeza kuwa, anawaombea kwa Mungu Majaji na Mahakimu wote pamoja na Mawakili ili waendelee na kazi ya kusimamia na kutoa haki kwa wananchi.

Aidha, Mwanasheria wa Serikali, Bw. Hemed  Mkomwa, alisema Mahakama na  wadau wanao wajibu wa kuboresha mfumo wa haki jinai, na wao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia jukumu alilonalo la kufanya tafiti na kuandaa mabadiliko ya sheria na kanuni mbalimbali watashirikiana na wadau wengine na kuwasimamia vyema Wanasheria wanaofanya kazi katika Sekta ya umma.

Sherehe hizo zilipambwa na ngoma za asili ya kabila la Waha, waliotumbuiza mbele ya Mgeni Rasmi, Mhe. Rwizile,  Wakuu wa Taasisi, wananchi, wanafunzi wa Vyuo na Sekondari, wadau wa Mahakama, Jeshi la Polisi pamoja na Waandishi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mawakili mara baada ya shughuli maadhimisho ya Siku ya Sheria katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (aliyesimama juu kulia) akipokea salaam kutoka kwa kiongozi wa kikosi maalum cha Jeshi la FFU kilichoandaliwa maalum kwa ajili ya ufunguzi wa shughuli za Mahakama katika Kanda hiyo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akikagua kikosi maalum cha Jeshi la FFU kilichoandaliwa maalum kwa ajili ya ufunguzi wa shughuli za Mahakama Kanda ya Kigoma.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (hayupo katika picha) alipokuwa akihutubia wakati wa hafla za maadhimisho ya Siku ya Sheria.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kushoto) akikagua kikosi maalum cha Jeshi la FFU kilichoandaliwa maalum kwa ajili ya ufunguzi wa shughuli za Mahakama katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma.

Tukiangazia MAHAKAMA KUU KANDA YA MANYARA, Mwakilishi wetu Christopher Msagati anaripoti kuwa;

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza amewasihi Wadau wote wa Haki Jinai kutimiza majukumu yao kwa wakati ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati.

Mhe. Kahyoza aliyasema hayo jana tarehe 01 Februari, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo kwa Kanda hiyo yaliadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Manyara. 

Mh Kahyoza alisema, “Wadau wote kwa pamoja tukiungana na tukaazimia kufanya kazi zetu kwa pamoja na kwa wakati tutasaidia sana Watanzania waweze kupata haki zao za msingi kwa wakati, mara nyingi huduma zimekuwa zikicheleweshwa kwa sababu ya baadhi ya watu kutokutimiza majukumu yao.”

Naye, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Lazaro Twange  ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Babati, aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kwa kuadhimisha Siku ya Sheria nchini na kuipongeza kwa mafanikio makubwa iliyopata Mahakama kwa kumaliza mashauri mengi hususani katika hatua ya Mahakama Kuu.

Naye, Mwendesha Mashtaka Mfawidhi wa Mkoa wa Manyara, Bi. Chema Maswi aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara. 

“Sisi sote ni kitu kimoja na tuna lengo moja, hivyo tunaahidi Mahakama kuendeleza ushirikiano ili tuweze kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote wanaofika mahakamani kila siku,” alisema Mhe. Maswi.

Naye Mwenyekiti wa Mawakili wa Kujitegemea (TLS)- Mkoa wa Manyara, Bw. Tadey Lister aliwasihi wadau wengine wa Haki Jinai kuendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika ili kusaidia Watanzania wasikwame kupata haki kwa wakati.

Ushirikiano wa wadau umesisitizwa na watu wote waliozungumza katika maadhimisho hayo kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu. Imesisistizwa kuwa ushirikiano thabiti utaleta matokeo thabiti ya haki kwa kupatikana kwa wakati. 

Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imefanya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini, ikiwa ni kilele cha Wiki ya Sheria nchini kwa mwaka 2024. Madhimisho hayo yalitanguliwa na dua na maombi kutoka kwa viongozi wa Dini na hotuba za Viongozi mbalimbali.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu wa Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza akikagua gwaride maalum lililoandaliwa kama ishara ya uzinduzi wa mwaka mpya wa Mahakama. Hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa Kanda hiyo ilifanyika jana tarehe 01 Februari, 2024 katika viwanja vya Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu wa Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza akihutubia wananchi waliofika Mahakama Kuu Manyara katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini.

Meza Kuu wakifuatilia matukio yaliyokuwa yakiendelea katika Siku ya Sheria. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Manyara, Mhe. John Kahyoza, wa kwanza kushoto ni Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. Stephemn Magoiga, wa kwanza kulia ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Frank Mirindo na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyara, Mhe. Lazaro Twange.

Baadhi ya Viongozi wa Dini waliohudhuria katika  hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini katika viwanja vya Mahakama Kuu Manyara.

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini na wadau wengine waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria. Walioketi kutoka kushoto  ni Mkuu wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe Stephen Magoiga. Wa kwanza kulia ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Frank Mirindo na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ni Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange.

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza (katikati) na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kanda hiyo baada ya hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.

Kutoka MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA MBEYA, Mwandishi wetu Mwinga Mpoli anaeleza kuwa;

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homera ameipongeza Mahakama kwa juhudi na elimu iliyotolewa kipindi cha Wiki ya Sheria na kuomba iwe jambo endelevu.

Mhe. Homera aliyasema hayo jana tarehe 01 Februari, 2024 alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini Kanda ya Mbeya.

“Ni matumaini yangu kwamba kaulimbiu ya mwaka huu ya upatikanaji wa haki jinai kwa urahisi kwa jamii yetu, kila mdau  ahakikishe anatekeleza wajibu na majukumu yake kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za miongozo mbalimbali. Niwapongeze sana Mahakama na wadau wake kwa namna ambavyo mnafanya kazi kwa weledi mkubwa tumeshuhudia namna mashauri yanavyozidi kupungua kwa kasi kubwa sana na hii inaonyesha ni jinsi gani mpo makini na mmejidhatiti na kazi” alisema Mhe. Homera

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Beda Ndunguru alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kudumisha utamaduni wa kushirikiana na Mahakama katika Siku ya Sheria kwani ni ishara njema.

“Maendeleo ya Taifa lolote yanategemea sana uwepo wa amani, usalama na utulivu pamoja na mifumo ya sheria yenye usawa, na katika kulinda vyote hivi tasnia ya utoaji haki inapaswa kuwa jumuishi katika maboresho ya sera, sheria na kanuni kwenye Sekta ya Sheria hususani mfumo wa makosa ya jinai nchini,” alisema Jaji Ndunguru.

Aidha, Mhe. Ndunguru aliwashukuru wageni wote waalikwa kutoka Taasisi mbalimbali, wadau wote wa Mahakama, Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini, watumishi wote wa Mahakama, Waandishi wa Habari na wananchi wote waliojumuika na kuwaomba waendelee kuunga mkono juhudi za Mahakama ya Tanzania katika utoaji wa haki.

Sherehe za Kilele cha Siku ya Sheria nchini mkoani Mbeya zilitanguliwa na zoezi la ukaguzi wa Gwaride katika viwanja vya Mahakama Kuu ikiwa ni kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homera akiwa katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria katika viwanja vya Mahakama Kuu Mbeya.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru akihutubia wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na Wadau wakisikiliza hotuba ya Mhe Jaji Mfawidhi (hayupo katika picha).
 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Beda Ndunguru akikagua Gwaride la uzinduzi wa mwaka mpya wa Mahakama.
Wageni mbalimbali waliohudhuria katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria Mbeya wakiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama, Vi ongozi wa Dini wa Madhehebu mbalimbali na Viongozi wa kisiasa.

(Habari hizi zimehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni