Na. Ahmedi Yusufu na Innocent kansha.
Mahakama ya Tanzania imeanza kutoa
mafunzo ya matumizi ya msingi ya stadi za kidigiti (Basic Digital skills) kwa
Watumishi wake 1,829 ambapo 1,324 ni Wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama na 505
ni Waandishi Waendesha ofisi.
Mafunzo hayo ya wiki saba yameanza
kutolewa tarehe 19 Februari, 2024 katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma
na yamefunguliwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere
kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole
Gabriel.
Pia mafunzo haya yamefunguliwa kwa
pamoja ambapo Dar es Salaam yanafanyika katika ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa
Fedha (IFM), Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Ukumbi wa Makumbusho ya
Taifa na Dodoma ni katika Ukumbi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania.
Akihutubia katika mafunzo haya, Bw.
Kategere ambaye alizungumza kwa njia ya mtandao na washiriki waliopo Dar es
Salaam huku yeye akiwa jijini Dodoma, amewataka washiriki wahakikishe wanatoka
kwenye mafunzo hayo wakiwa na dhamira ya dhati ya kwenda kutumia mifumo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanya kazi.
Pia, amewaambia washiriki hao:
"Wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama na Waandishi waendesha ofisi ni wadau
muhimu katika matumizi ya mifumo kama e-case Management na e-office. Hivyo
haitarajiwi msaidizi wa kumbukumbu kwa vyovyote kutoa kisingizio cha kutokujua
kutumia mifumo hiyo."
Mafunzo haya yanatolewa na Mahakama
ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na yanaendeshwa
na wataalamu kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC).
Akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanzania,
Bi. Patricia Ngungulu alianza kwa kutoa, historia fupi ya kwanini mafunzo hayo
yanafanyika.
“Mwaka 2021/22, Mahakama ilifanya
zoezi la kutathmini Utayari wa Watumishi wa Mahakama katika kutumia TEHAMA na
Vifaa vya TEHAMA. Zoezi lilibaini uwepo wa miundombinu pamoja na uwepo wa
watumishi wanaopenda kutumia TEHAMA katika kazi zao. Hata hivyo, changamoto
kubwa ilikuwa ni ukosefu wa maarifa na ujuzi miongoni mwa watumishi wa Mahakama
likiwemo kundi hili”, amesema Bi. Ngungulu
Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha
kuwa, wakati wa Baraza la Wafanyakazi la mwaka 2023 lililofanyika Mei, 2023
jijini Dodoma, suala la kujenga uwezo katika matumizi ya digitali yalijadiliwa
na kuelekezwa kuwa suala hili lifanyike kwa watumishi wote hasa wakati huu
ambao Mahakama inaelekea kwenye Mahakama Mtandao. Hivyo, maandalizi kwa ajili
ya mafunzo haya yakaanza mara moja na leo tumeanza kazi ya kuwawezesha
watumishi katika eneo hilo.
Bi. Ngungulu ameongeza kuwa, mafunzo
hayo yenye idadi kubwa ya washiriki, ni mradi mkubwa kuwahi kufanyika na ambao
utagharimu takribani 2.5 Bilioni, ambapo matokeo ya mafunzo haya, yataweka njia
kwa makundi mengine ya watumishi kuwezeshwa kwenye mafunzo kama hayo.
“Nitoe rai kwa washiriki kuzingatia
mafunzo haya na kuhakikisha kuwa maarifa na ujuzi utakaopatikana kutokana na
mafunzo, unatumika vizuri katika kuharakisha utoaji huduma na wenye tija kwa
ujumla kwenye maeneo yao”, amesisitiza Mkurugenzi Msaidiszi huyo.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mkuu na
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama (IJA) Mhe. Dkt. Patricia Kisinda
akizungumza akiwa Dar es Salaam, amewaomba washiriki kutumia vizuri mafunzo
hayo ili kuboresha maarifa yao katika matumizi ya TEHAMA.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa
Umma (TPSC) jijini Dar es salaam, Dkt. Ernest Mabonesho amesema kuwa kwa sasa
Utumishi wa umma unahitaji mtu mwenye ujuzi wa matumizi ya TEHAMA ili kuweza
kutenda kazi zake kwa urahisi na kuzaa matokeo bora.
Miongoni mwa malengo ya mafunzo haya
ni kuwapatia na kukuza maarifa na ujuzi wa washiriki ili kuweza kutumia mifumo
ya kidigiti katika kazi zao za Kimahakama, ikizingatiwa kuwa kwa sasa utendaji
kazi wa Mahakama unaelekea zaidi mtandaoni (e-judiciary).
Haya ni mafunzo ya awali baada ya
mtaala kuandaliwa na IJA na kupitishwa na Mahakama ya Tanzania na yanafadhiliwa
na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia ikiwa ni utekelezaji wa
Awamu ya Pili ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere akihutubia wakati wa ufunguzi wa mafumzo ya matumizi ya msingi ya stadi za kidigiti (Basic Digital skills) kwa Wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama na Waandishi Waendesha ofisi. Amefungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, katika ukumbi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma tarehe 19 Feberuari, 2024.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akitoa neno la ukaribisho kabla ya uzinduzi wa mafunzo hayo jijini Dar es salaam.
Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama (IJA) Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza wakati wa kutoa salamu fupi za Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kabla ya uzinduzi wa mafunzo hayo.
Mashauri mwelekezi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
(TPSC), Bw. Charles Magaya akiwezesha mada katika Mafunzo
ya matumizi ya msingi ya stadi za kidigiti (Basic Digital skills) ambayo
yanatolewa kwa Wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama na Waandishi Waendesha
ofisi jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni