Jumanne, 20 Februari 2024

UJUMBE BENKI YA DUNIA WATEMBELEA CHUMBA CHA MIFUMO YA KUTOLEA TAARIFA ZA MAHAKAMA

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) leo tarehe 20 Februari, 2024 umetembelea Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room) kilichopo katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) jijini Dodoma.

Ziara fupi ya Ujumbe huo wenye takribani Maafisa watano kutoka Benki ya Dunia umeongozwa na Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha pamoja na Maafisa kadhaa wa Mhimili huo.

Mara baada ya kuwasili katika Chumba hicho, Maafisa hao walionesha kustaajabu na kufurahishwa na hatua ambayo Mahakama imepiga ya uwekaji wa chumba hicho ambacho kimesheheni taarifa nyingi za Mhimili huo.

Akitoa maelezo kuhusu Chumba hicho, Afisa TEHAMA na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza amewaeleza Maafisa hao kuwa, chumba hicho kinazalisha na kuweka taarifa za viwango vya utendaji vya kitaasisi ikiwa ni pamoja na ripoti za utendaji wa mtu binafsi na dashibodi zinazotolewa kupitia kanzi data ya utoaji taarifa ya Mahakama (Judiciary Business Intelligent (BI) Report Engine).

Amesema kwamba, Chumba hicho pia kinasimamia, kuendesha na kuhakikisha usalama na upatikanaji wa mtandao wa Mahakama sambamba na Ufuatiliaji wa Miundombinu ya Mawasiliano kwa ajili ya usimamizi mzuri wa wa rasilimali za TEHAMA.

Kazi nyingine za Chumba hicho maalum ni kuchakata na kutoa taarifa mbalimbali za kijinsia au vikundi maalum vinavyotolewa kupitia kanzi data ya Mahakama (Judiciary Business Intelligent (BI) Report Engine), kutayarisha na kutoa taarifa za Kanda za Kimahakama kwa kila ngazi ili kuwezesha shughuli za kimahakama na kazi nyingine.

Wakiwa ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama, Ujumbe huo ulipata fursa pia ya kutembelea chumba cha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Judiciary Call Centre) ambacho pia kimeambatana na Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room).

Ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya ujumbe huo, walianza kwa kuwasilishiwa taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya Kurugenzi ya TEHAMA, Kurugenzi ya Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili pamoja na Kitengo cha Usimamizi wa Majengo.

Ujumbe huo unaendelea na ziara yake ambapo wamepanga kutembelea baadhi miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi ikiwemo Geita na Simiyu na tarehe 24 Februari, 2024 watahitimisha kwa kufanya majumuisho katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akifafanua jambo kwa ujumbe wa Benki ya Dunia (WB) pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama (hawapo katika picha) kuhusu Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room) leo tarehe 20 Februari, 2024 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
 
Afisa TEHAMA na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza kushoto akitoa maelezo kwa ujumbe wa Benki ya Dunia pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama kuhusu 'screen' maalum yenye taarifa mbalimbali za Mahakama leo tarehe 20 Februari, 2024 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Muonekano wa 'screen' maalum (kushoto) iliyopo katika Chumba cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room). Bw. Ndenza akiendelea kutoa maelezo kuhusu Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room).
Afisa Mwandamizi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Benjamin Mtesigwa (wa pili kushoto) akizungumza jambo wakati yeye pamoja na Maafisa wenzake kutoka Benki ya Dunia walipotembelea 
Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room) leo tarehe 20 Februari, 2024 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Ujumbe wa Benki ya Dunia pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa kuhusu Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room).

 
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha (wa pili kulia) akitoa maelezo ya jinsi anavyotumia mifumo mbalimbali na kupata taarifa kupitia 
'screen' maalum yenye taarifa mbalimbali za Mahakama. Kushoto ni Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na wengine ni Maafisa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa nne kulia) akiwa pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Dunia na sehemu ya Watumishi wa Mahakama wakati walipotembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja (Judiciary Call Centre) kilichopo katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) jijini Dodoma.
 Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) na baadhi ya watumishi wa Mahakama wakati ujumbe kutoka Benki hiyo walipotembelea katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 20 Februari, 2024 kwa lengo la kukagua Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room).

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)








 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni