Alhamisi, 22 Februari 2024

MKUU WA MKOA MARA AMTEMBELEA JAJI MFAWIDHI MUSOMA

 Na Francisca Swai – Mahakama Musoma.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda  jana  tarehe 21 Februari 2024 alimtembelea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma ,Mhe. Fahamu Mtulya, kwa lengo la kuyafahamu mazingira ya Mahakama Kuu Musoma pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya kiutendaji baina ya Ofsi hizo mbili.

Katika salamu na mazungumzo yake Mhe. Fahamu Mtulya alimueleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Mahakama inajitahidi kutekeleza jukumu lake la utoaji haki kwa weledi na kwa wakati kama inavyotakiwa ambapo kwa sasa Mahakama Kuu Musoma peke yake kila Mhe.Jaji anasikiliza zaidi ya mashauri yapatayo 200 kwa mwaka.

Mhe Mtulya alisema wingi huu wa mashauri unatokana na wananchi kusogezewa huduma ya Mahakama Kuu Mkoani Mara tofauti na ilivyokuwa kwa miaka mitano ya nyuma ambapo wananchi walilazimika kwenda Mwanza kufuata huduma hiyo. Na kutokana na umbali na gharama za nauli, chakula na malazi wananchi wengi waliacha haki zao zipotee kwakuwa hawakuweza kumudu gharama hizo.

Aidha, katika mazungumzo hayo Mhe. Mtulya alisema Kanda ya Musoma ina jumla ya Mahakama Kuu moja, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya sita (Musoma, Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya) Mahakama za Mwanzo 32 na zote zinafanyakazi.

Mhe. Mtulya pia alimshukuru Mkuu wa Mkoa na kamati za maadili za maafisa wa Mahakama kwa namna zinavyofanya kazi kuhakikisha Maafisa wa Mahakama wanazingatia maadili ya kitaaluma katika kutekeleza majukumu yao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda Mtanda ambaye pia kwa nafasi yake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwa Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa, alishukuru kwa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Mahakama na Ofisi nyingine za kiserikali ndani ya Mkoa jambo linaloziwezesha ofisi hizo kushirikiana kwa karibu katika kutatua changamoto za wananchi na kuleta amani. 

Katika ziara hiyo fupi pamoja na mipango mbalimbali ya kiutendaji iliyojadiliwa, Mkuu wa Mkoa huyo, alitembelea mazingira ya Mahakama Kuu Musoma pamoja na wenyeji wake Jaji Mtulya akiongozana na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha na Monica Ndyekobora pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya.


Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (wa pili kulia) akisaini katika kitabu cha wageni Ofisini kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (aliyesimama) akiongea jambo katika kikao hicho cha viongozi wa Mahakama Kuu Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara.




Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (wa pili kulia) aliyemtembelea ofisini kwake. Wengine ni Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa kwanza kushoto) na Monica Ndyekobora (wa kwanza kulia) pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa pili kushoto).


Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (wa pili kulia) akiongea jambo katika kikao kifupi cha viongozi wa Mahakama Kuu Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara kilichofanyika Ofisini kwa Mhe. Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (kulia) Ofisini kwa Mhe. Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (wa kwanza kulia) akikagua na kujioneautunzaji wa mazingira ya Mahakama Kuu Musoma akiwa na wenyeji wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (aliyeko kulia kwa Jaji Mfawidhi) pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (mwenye mtandio wa rangi nyekundu) na Monica Ndyekobora (kulia kwa Mhe. Mshasha).
 Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda (katikati) akiwa na wenyeji wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto) Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa kwanza kushoto) na Monica Ndyekobora (wa pili kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa kwanza kulia).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni