· Mafanikio lukuki yabainishwa
· Hakuna mlundikano wa mashauri
· Mahusiano mema na Wadau ni dhahiri
Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma
Mahakama Kuu Musoma pamoja na wadau wake washeherekea miaka mitano ya kazi ya Mahakama hiyo kwa furaha na shangwe kuu.
Mahakama Kuu Musoma ilianzishwa rasmi kwa tangazo la Gazeti la Serikali namba 112 la tarehe 01/02/2019. Tangazo hili lileta nyuso za furaha kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambao, kabla ya hapo walikuwa wakifuata huduma ya Mahakama Kuu, katika Mkoa wa Mwanza umbali wa Kilomita 223 kutoka Musoma.
Mahakama Kuu Musoma ilianza kazi chini ya uongozi wa Jaji Mfawidhi, Mhe. John Kahyoza, akisaidiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa, Mhe. Zephrine Galeba.
Viongozi wengine waanzilishi ni Naibu Msajili, Mhe. Mary Moyo na Afisa Utumishi, Bi. Francisca Swai, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mtendaji wa Mahakama kuanzia mwezi Aprili 2019 hadi Novemba 2019. Walikuwepo pia watumishi wa kada nyingine mbalimbali ambao kwa jumla wao walikuwa wanane.
Mahakama Kuu Musoma ilianza kazi zake rasmi mwezi Aprili 2019 katika jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na baadae mwezi Desemba 2019 ilihamia katika jengo lake la Mahakama Kuu lililopo eneo la Bweri, umbali wa Kilomita nane kutoka Musoma Mjini.
Kwa sasa Mahakama Kuu Musoma iko chini ya uongozi wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akisaidiana na Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Marlin Komba na Mhe. Kamazima Idd.
Viongozi wengine waliopo kwa sasa ni Naibu Msajili Mhe. Salome Mshasha na Mhe. Monica Ndyekobora, Mtendaji wa Mahakama Bw. Festo Chonya pamoja na watumishi wa kada nyingine jumla yao wote wakiwa watumishi 37.
Kwa kipindi cha miaka mitano Mahakama hiyo inajivunia mambo mbalimbali ikiwemo kasi nzuri ya usikilizaji wa mashauri. Kwa miaka hiyo imesajili mashauri 4,689 na kumaliza mashauri 4,327.
Mafanikio mengine ni kutokuwa na mashauri mlundikano, kuimarisha ushirikiano mzuri kati ya Mahakama na wadau wake, uhifadhi mzuri wa mazingira ya ndani na nje ya jengo na kuwa na umoja, upendo na ushirikiano kati ya Viongozi watumishi.
Kadhalika, tangu kuanzishwa kwa Kanda ya Mahakama Kuu Musoma kumechagiza uwepo wa mafanikio yanayogusa nyanja ya miundombinu ambapo maboresho makubwa yamefanyika kwa baadhi ya Mahakama za Mwanzo kwa kufanyiwa ukarabati mkubwa na nyingine kujengwa upya kupitia fedha za ndani.
Miongoni mwa Mahakama hizo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mahakama za Mwanzo Nansimo, Kenkombyo, Bunda Mjini, Ngoreme, Mtana, Kinesi, Kukirango, Shirati, Kiagata na Musoma Mjini.
Aidha, katika kipindi hicho Mahakama Kanda ya Musoma imefanikiwa kupata jumla ya hati 21 za viwanja vya Mahakama, Mahakama zote zina miundombinu ya vyoo na jumla ya Mahakama za Mwanzo 30 zina umeme.
Katika kipindi husika hakuna Mahakama iliyofungwa, Mahakama zote za Mwanzo 32 zinafanya kazi na upandaji wa miti umefikia miche 10,000 kuzunguka mipaka na maeneo ya Mahakama ndani ya Kanda.
Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mahakama kupitia Afisa wake, Bw. Simon Lyova imefanikiwa kuanzisha mfusha mpya wa kuita mashauri kwa kutumia simu ya mkononi na kompyuta mpakato badala ya kutumia vipaza sauti.
Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya zote pamoja na Magereza yote ndani ya Kanda yamenunuliwa simu na laini za simu na kuwezeshwa vifurushi vya kila mwezi kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya ‘Teleconference.’ Jumla ya mashauri 336 kwa mwaka 2023 yamesikilizwa kwa njia hii ndani ya kanda nzima.
Uwepo wa Mahakama Kuu Musoma umekuwa na faida kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa haki kwa karibu na kwa wakati, hivyo kuwapunguzia gharama za muda na nauli zilizokuwa zikitumika kufuata huduma za Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Mahakama hii pia imesogeza kwa karibu huduma za Mahakama ya Rufani kwa wananchi katika Mkoa wa Mara.
Katika kipindi hicho, huduma ya Mahakama imesogezwa karibu zaidi kwa wananchi kupitia uanzishwaji wa Mahakama mpya, ikiwemo Mahakama za Wilaya Rorya na Butiama na Mahakama za Mwanzo Mukendo iliyoko Musoma Mjini na Ingri iliyoko Rorya.
Baadhi ya Viongozi waliowahi kufanya kazi katika Mahakama Kanda ya Musoma Majaji wakiwemo Mhe. Ephery Kisanya, Mhe. Awamu Mbagwa, Mhe. Frank Mahimbali, Naibu Wasajili Mhe. Mary Moyo na Mhe. Frank Moshi.
Katika kusheherekea miaka hiyo mitano, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma pamoja na wadau wake walisherehekea kwa kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu katika maeneo tofauti tofauti pamoja na magereza na kutoa misadaa mbalimbali kwa makundi hayo.
Akizungumza katika hafla fupi iliyojumuisha Watumishi wa Mahakama na Wadau wake, Mhe. Mtulya alisema miaka hii mitano imekuwa ya mafanikio makubwa kwa Kanda ya Musoma.
Mahakama ya Mwanzo Ngoreme iliyoko Serengeti kabla na baada ya ukarabati.
Mahakama ya Mwanzo Mtana iliyoko Tarime kabla na baada ya ukarabati.
Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo iliyoko Bunda kabla na baada ya ukarabati.
Pichani ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa tatu kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Mhe. Erick Marley (wa tatu kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bunda Mhe. Mulokozi Kamuntu (wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo Mhe. Victoria Gambalama (wa pili kushoto), Afisa Utumishi Mahakama ya Wilaya Bunda Bi. Rose Millinga na Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo Bi. Tabu Ungura (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo baada ya ukarabati mkubwa kufanyika.
Mahakama ya Mwanzo Kiagata iliyoko Butiama kabla na baada ya ukarabati.
Pichani ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa tatu kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Mhe. Erick Marley (wa tatu kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Butiama Mhe. Judith Semkiwa (wa pili kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Kiagata Mhe. Kennedy Mwaikambo (wa kwanza kushoto), Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Butiama Bi. Teckla Patrick na Mlinzi wa Mahakama ya Mwanzo Kiagata Bw. Boniphace Kanukanu (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Kiagata baada ya ukarabati mkubwa kufanyika.
Mahakama ya Mwanzo Nansimo iliyoko Bunda kabla na baada ya ukarabati.
Watumishi wa Mahakama na Wadau wakitoa misaada kwa Magereza Musoma, Bunda na Tarime (juu na picha mili chini).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni