Ijumaa, 23 Februari 2024

UJUMBE BENKI YA DUNIA WATEMBELEA UJENZI WA KITUO JUMUISHI SIMIYU

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Ujumbe wa Benki ya Dunia ambao upo nchini kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Benki hiyo jana tarehe 22 Februari, 2024 uliangalia maendeleo ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Simiyu.

Wawakilishi hao kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor na Bw. Benjamin Mtesigwa walitemebela mradi huo wakiwa umeambatana na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na Viongozi wengine wa Mahakama.

Viongozi wengine walioambatana na Ujumbe huo ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ujenzi na Miundombinu, Bw. Moses Luiva pamoja na timu nzima inayohusiana na mradi huo kutoka makao makuu ya Mahakama.

 

Mhe. Dkt. Rumisha, ambaye alikuwa Mwenyekiti, aliongoza kikao cha tathmini ya mradi huku akimtaka Mhandisi Mshauri, Bw. Athuman Ikungu kuwasilisha taarifa ili kujua maendeleo yaliyofikiwa na kufahamu kama bado Mkandarasi yupo ndani ya muda aliopewa. 

 

Taarifa ya Mhandisi Mshauri ilionyesha Mkandarasi yupo nyuma kwa asilimia nne, hatua iliyomlazimu Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bi. Christine kumtaka Mhandisi Mshauri kufidia asilimia hizo ndani ya wiki moja ili kwenda na muda aliopewa kukamilisha mradi huo.

 

Katika kikao hicho, Mwenyekiti pia alimtaka Mkandarasi kujenga kisima haraka iwezekanavyo ili kurahisisha utendaji kazi na kutekeleza makubaliano ya mkataba ulivyo elekeza.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti na timu nzima iliridhishwa na maendeleo ya mradi na kumtaka Mkandarasi azidi kuongeza juhudi ili aweze kukamilisha mradi huo kwa wakati.



Kulia ni Mhe. Dkt. Angelo Rumisha ambaye alikua Mwenyekiti wa kikao. Kushoto ni mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor.  


Pichani ni wajumbe waliohudhuria kikao cha maendeleo ya mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Simiyu.


Picha ya mradi ulipofikia.
 
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni