Jumapili, 25 Februari 2024

MILIONI 226 KUJENGA STUDIO YA KUTOA MAFUNZO YA MASAFA CHUO CHA MAHAKAMA

Na Tiganya Vincent-MahakamaLushoto 

 

Jumla ya shilingi milioni 226 zitatumika katika ujenzi wa studio kwa ajili ya utoaji wa mafunzo ya masafa kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

 

Hayo yamelezwa jana tarehe 24 Februari 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ujenzi na Miundombinu (HEM) wa Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Moses Luiva wakati akitoa taarifa kwa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo kwa ajili ya studio hiyo.

 

Alisema jengo hilo litakuwa na studio yenye eneo la kuandaa mada kwa njia ya picha mjongeo (Video) na sauti (Audio), eneo la kutunza data (Server room), Ofisi ya Maafisa Teknolojojia ya Habari na Mawasiliano, mapokezi na sehemu ya watu kusubiria.

 

Mhandisi Luiva alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ulioanza tarehe 18 Februari 2024 unaendelea vizuri na utakamilika tarehe 18 Mei 2024.

 

Wakati huo huo, Ujumbe wa Benki ya Dunia umeonyeshwa Mfumo wa Utoaji wa Mafunzo kwa njia ya Masafa (E -Learning) ambao umetayarishwa ya Timu ya Wataalamu kutoka Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.

 

Akizungumza mara baada ya Ujumbe wa Benki ya Dunia na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kupitishwa katika Mfumo wa Jukwaa la Mafunzo kwa Njia ya Masafa, Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alisema kukamilika kwa Jukwaa hilo hakutawalazimu wanachuo kusafiri hadi Lushoto kuhudhuria masomo.

 

Alisema Chuo kitaweza kupata Wanafunzi kutoka mbali ambao wanasoma huku wakiendelea na kazi zao za kila siku. 

 

Aliongeza kuwa Mwanachuo ataweza kujipangia kasi yake ya masomo, muda wake wa kusoma na muda atakaopenda kukamilisha somo lolote na Wahadhiri wataweza kuboresha masomo wakati wowote na kuwasiliana na Wanafunzi wakati wowote na wakiwa sehemu yoyote ile duniani. 

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema Jukwaa hilo linatoa fursa kwa IJA kuingia katika makubaliano na vyuo vingine ndani na nje ya Tanzania kutoa kozi, masomo au mafunzo ya ziada kwa Wanachuo wa Chuo cha Mahakama. 

 

Alisema jambo hilo ndio msisitizo ambao umekuwa ukitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika mikutano mbalimbali anapokutana na Watumishi wa Mahakama.

 

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema Jukwaa hilo pamoja na utoaji elimu kwa wadau wengine pia linalenga kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama katika maeneo ya taaluma zao.

 

Alisema wanatarajia kutumia rasilimali watu ambao wana ujuzi wa kutosha wakiwemo Majaji Wastaafu kuandaa mada ambazo zitatengenezwa katika studio kwa Mfumo wa picha Mjengeo(Video) na mada za sauti (Audio) ambazo zitasaidia kutoa mafunzo kwa walengwa.

 

Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour amesema mfumo huo ni kielelezo kwa Mahakama nyingine barani Afrika  katika kuwajengea uwezo watumishi wake.

 

Naye, Kiongozi Mwenza wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, ambaye pia ni Afisa Mwandamizi kutoka Benki hiyo, Bw. Benjamin Mtesigwa amepongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa hatua ya kuamua kujenga Jukwa hilo ambalo ni hatua kubwa katika utoaji wa elimu ya masafa.

 

“Niwapongeze kwa hatua kubwa hii ya kukamilisha ujenzi wa Jukwaa la Mafunzo ya Masafa. Hayni mafanikio mengine ambayo yataendelea kudhihirisha utekelezaji mzuri wa miradi ya Mahakama,” amesema Bw. Mtesigwa.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akifafanua jambo kwa Ujumbe wa Benki ya Dunia pamoja na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (hawapo katika picha) kuhusu Jengo la Studio ya Uandaaji wa Mada kupitia Jukwaa la utoaji mafunzo kwa njia ya masafa (e-learning platform) katika eneo la Chuo cha IJA Lushoto Tanga.


Baadhi ya Wajumbe kutoka Benki ya Dunia na  Mahakama ya Tanzania  wakiangalia maendeleo ya ujenzi wa studio   hiyo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.



Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ujenzi na Miundombinu cha Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Moses Luiva (aliyenyosha mkono)  akitoa taarifa kwa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo kwa ajili ya Studio ya Utoaji Mafunzo kwa njia ya Masafa.


Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akifafanua jambo kwa Ujumbe wa Benki ya Dunia(WB) pamoja na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania kuhusu Jukwaa la Utoaji Mafunzo kwa njia ya Masafa (e-learning platform).

 

 Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akimkabidhi machapisho mbalimbali Kiongozi wa Timu ya Ujumbe wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor (kushoto) mara baada ya ziara kukagua Studio hiyo.


Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA),
 Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kushoto), Kiongozi wa Timu ya Ujumbe wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor (katikati) na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Ujumbe kutoka Benki ya Dunia mara baada ya ziara kukagua Studio.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni