Ijumaa, 2 Februari 2024

TALECK ATOA RAI KWA WADAU WA HAKI KUSHIRIKIANA KUMUHUDUMIA MWANANCHI

Na. Hilary Lorry – Mahakama, Lindi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Zainab Telack amewaongoza watumishi,wadau na wanachi Mkoa wa Lindi katika  maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini  tarehe 1 Februari, 2024 yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.

Bi. Telack ameomba Mahakama kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja ili kuwezesha wananchi kupata haki kwa wakati.

Aidha, Bi.Telack  amesema, wadau wote wakifanya kazi kwa kushirikiana na kusikilizana wananchi watapata haki zao kwa wakati huku akitumia nafasi hiyo kuipongeza Mahakama kwa kufanya maboresho ya mifumo yake ya kusikiliza mashauri kwa njia ya kidigiti ambayo inarahisisha  utendaji kazi wa shughuli za kimahakama na upatikanaji wa haki kwa wakati.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter Singano alisema, Mahakama katika maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza juu ya lengo lake mama la utoaji haki kwa wananchi kwa kushirikiana na wadau.

Amesema, elimu ya sheria juu ya shughuli za kimahakama zimetolewa maeneo mbalimbali kama vile sokoni, vituo vya mabasi, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo pamoja na vyombo vya Habari ambapo inakadiriwa takribani watu 20,000/- wamefikiwa na elimu juu ya shughuli za kimahakama.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela alimshukuru Mgeni wa Heshima Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi.Zainab Telack kwa kutenga mda wake kushiriki nao katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya sheria.

Vilevile, Bi. Mbeyela aliwashukuru wadau wote kwa ushirikiano waliotoa kwa wakati wote hasa wiki ya sheria ambapo aliomba ushirikiano huo uendelee ili kuendelea kulisongesha gurudumu la utoaji haki.

Katika kutambua ushirikiano mzuri wa wadau kwa Mahakama uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi uliandaa vyeti kwa wadau waliojitoa zaidi kwa Mahakama kama vile Magereza Lindi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkurugenzi Manispaa ya Lindi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ofisi ya Taifa ya Mashataka, Jeshi la polisi Lindi, Redio Mashujaa FM, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lindi pamoja na Ofisi ya Misitu Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi.Zainab Telack akihutubia watumishi,wadau na wananchi mkoa wa Lindi wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya sheria nchini.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi. Mhe.Consolata Peter Singano akisoma hotuba katika kilele cha siku ya sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip.Godfrey Mbeyela akitoa neno la shukrani kwa wadau, na watumishi wa Mahakama kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi cho cha maadhimisho ya wiki ya sheria na hatimaye siku ya kilele chake.



Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi.Zainab Telack aliyevalia kitenge akipanda mti siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini.

Mwakilishi kutoka Mashujaa Redio FM akipokea zawadi  ya cheti kwa wadau na taasisi zinazojitoa Zaidi katika kufanikisha majukumu mbalimbali ya utoaji haki.

Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi wakiwa katika picha pamoja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni