Alhamisi, 7 Machi 2024

JAJI MKUU AWASILI NCHINI BAADA YA KUSHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA UGANDA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 7 Machi, 2024 amewasili nchini akitokea Uganda kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa unaozihusisha Mahakama Afrika kujadili njia mbadala ya utatuzi wa migogoro, ikiwemo njia ya usuluhishi.

Mhe. Prof. Juma na ujumbe wake waliagwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Entebe na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Patience Rubagumya majira ya saa 10.45 jioni kabla ya kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Uganda kuja Tanzania.

Ushiriki wa ujumbe wa Mahakama ya Tanzania katika Mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa kufuatia mada mbalimbali zilizowasilishwa na kupata uzoefu wa Mahakama nyingine katika Bara la Afrika namna wanavyochukulia kwa uzito suala la utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, ikiwemo usuluhishi.

Katika Mkutano huo wa siku mbili ulioanza tarehe 5 Machi, 2024, Jaji Mkuu aliongozana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kituo hicho, Mhe. Isaya Arufani.

Viongozi wengine wa Mahakama wanaohudhuria Mkutano huo wa siku mbili ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando na Afisa Itifaki, Bw. Juma Mshana.

Ujumbe huo wa Mahakama ya Tanzania ulihudhuria Mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Mestil jijini Kampala kufuatia mwaliko alioutoa Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo.

Mkutano huo uliandaliwa na Mahakama ya Uganda kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Pepperdine kilichopo California Marekani. Kauli mbiu ya Mkutano huo ilikuwa Kurekebisha Utawala wa Haki katika Bara la Afrika.

Wakati wa Mkutano huo washiriki walijadili mada mbalimbali kulingana na tafakari kwamba kile kinachoainishwa leo kama Utatuzi Mbadala wa Migogoro ndio msingi wa falsafa na utaratibu wa utatuzi wa migogoro barani Afrika.

Mkutano huo uliwawaleta pamoja Majaji, Wahusika Sekta Binafsi, Mawakili wa Kujitegemea, Wasomi na Waendesha Mashtakana kutoa fursa kwa Mahakama na watendaji wengine wa haki barani Afrika kufikiria upya upatanishi na uwekaji wa Utatuzi Mbadala wa Migogoro kama njia kuu, kama sio njia ya msingi ya kusuluhisha migogoro katika robo ijayo ya karne ya 21.

Zaidi ya hayo, Mkutano huo uliangazia pia mwelekeo unaoibuka, maendeleo na ubunifu kwenye Utatuzi Mbadala wa Migogoro katika kuimarisha upatikanaji wa haki na utatuzi wa haraka wa migogoro.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili patika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Uganda kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa. Picha chini akiwa aameongozana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Uganda, Det. Pius Bigirimana.


Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, ambaye aliambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Mkutano huo akiwasili chini.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe aliokuwa ameongozana nao kwenye Mkutano huo. Kwenye Ujumbe huo alikuwepo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kituo hicho, Mhe. Isaya Arufani (wa tatu kulia), Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi (wa kwanza kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando (wa kwanza kulia) na Afisa Itifaki, Bw. Juma Mshana ( wa pili kulia).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni