Na. Innocent Kansha – Mahakama.
Mwenyekiti
wa Kamati Kuu ya Watendaji Wakuu wa Mahakama nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika ‘SEAJAA’ na Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
amefungua Mkutano wa kamati hiyo ulifanyika leo tarehe 8 Machi, 2024 katika
ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Tifany Diamond jijini Dar es salaam.
Kamati
tendaji ya Jumuiya hiyo iliyokutana katika kikao cha siku moja jijini Dar es Salaam
kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kukuza umoja na ushirikiano baina ya nchi wananchama
na kuimarisha mifumo ya shughuli za Mahakama na hatimaye kuchangia ukuaji wa
uchumi endelevu.
“Lengo
kubwa la kukutana kwa kamati hii ni kujadili na kuangalia mambo mtambuka ambayo
nchi wanachama wanashabihiana ili tuweze kueleta mchango mkubwa katika eneo la
kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesema Mwenyekiti wa SEAJAA.
Prof.
Ole Gabriel amebainisha kuwa mkutano huo unalengo la kubadilishana uzoefu na
kujifunza kutoka kwa nchi moja wanachama hadi nyingine, kwa maana ya kutambua
fursa zilizopo katika kila nchi na kujifunza mambo mazuri ya kuendeleza nchi
wananchama.
Jumuiya
hiyo ya SEAJAA ina wanachama wa nchi13 na kwa ngazi ya Majaji Wakuu nchi
wanachama ni 16. Chama hicho cha Watendaji kinafanya kazi kwa karibu sana na
Jukwaa la Majaji Wakuu ambao pia walikuwa na mkutano wao Mkuu jijini Arusha mwaka
jana tarehe 23 Oktoba, 2023.
“Sisi
kama nchi tunanufaika kwa kiwango kikubwa sana kuandaa mikutano mikubwa kama
hii, mosi tunaendeleza masuala ya uchumi na pia masuala ya kijamii na jina la
nchi linazidi kukua zaidi,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Mwenyekiti
huyo, amesema kuwa, faraja kubwa ni kuona kwamba nchi zote hizo zinafarijika
kuona hatua ambayo imepigwa na Tanzania katika masuala ya uendeshaji wa
shughuli za utoaji haki na za Mahakama kwa ujumla.
“Kwa
mkutadha huo nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo
tunapata rasilimali watu na rasilimali fedha zinazotuheshimisha katika shughuli
za Mahakama na hata kutangaza vivutio vya utalii,” amesema Mtendaji Mkuu.
Aidha,
Prof. Ole Gabriel amesema Jumuiya ina mpango na mkakati wa kujiunga na ile
taasisi ya Kimataifa inayoitwa IACA “International Association for Court
Administrators” ili Jumuiya hiyo ya kusini na mashariki mwa Afrika izidi kukua
na kujitanua ikiwa ndiyo lengo la misingi la jumuiya hiyo.
“Tumesisitizana
masuala ya kutoa michango kutoka nchi wanachama ili taasisi hii iweze kuwa na
mafungu ya kutosha. Sababu tukiwa na
mafungu ya kutosha linakuwa ni jambo la maana katika kuratibu shughuli
mbalimbali za jumuiya kama vile mkutano huu wa leo,” ameongeza Mwenyekiti huyo.
Mwenyekeiti
ameongeza kuwa, kupitia muunganiko huo Tanzania imeendelea kusifika na
kuheshimika kwa kupiga hatua kubwa sana katika masuala ya matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani mifumo iliyojengwa na
wataalam wa ndani. Mahakama ya Tanzania itaendelea kuboresha miundombinu hiyo
ili iiendelee kuwa kisima cha maarifa kwa nchi nyingine wanachama katika kutoa
elimu hiyo.
“Kwa
sasa Mahakama ina mifumo madhubuti inayotumika kuendeshea mashauri ikiwemo
mfumo wa kielektroniki wa kuratibu mashauri e-CMS, mfumo wa kutafsiri na
unukuzi – TTS na pia mifumo mingine zaidi ya 11, alikadhalika mfumo wa kutuza
maamuzi ya kimahakama na nyaraka TanzLII ambao unashika nafasi ya kwanza kwa
kupakuliwa na watu wengi dunia hasa wale watumiaji wa maamuzi ya kimahakama,”
ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa SEAJAA na Mkurugenzi Mtendaji wa Mahakama ya
Namibia, Bw. Benhardt Kukuri amesema kama kamati wanayofuraha kubwa kuja tena
Tanzania kwa ajili ya kikao hicho cha kamati tendaji ya jumuiya hiyo.
“Tunakumbukumbu nzuri ya kushiriki mkutano wa Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu uliofanyika jijini Arusha
mwezi wa 10 mwaka jana, hivyo kurudi kwetu Tanzania ni furaha kubwa na tunashukuru
kwa kukubaliwa na wenzetu wa Mahakama ya Tanzania kufanya kikao hiki hapa
wameonyesha ukarimu wa hali ya juu,” ameongeza Katibu wa SEAJAA.
Lengo
la Jumuiya ni kuunga mkono juhudi za Mahakama za utoaji haki kwa wananchi wa taasisi
wanachama. Pia kuangalia maeneo ya ushirikiano na kujifunza au kupata ujuzi
kwenye maeneo ambayo nchi wanachama wanafanya vizuri katika utoaji haki kwa
wananchi. Jukwaa hilo litazitumia nchi hizo kama sehemu ya kujifunzia.
“Mathalani
uendeshaji wa shughuli za utoaji haki kwa njia ya TEHAMA ili kumsaidia wananchi
kupata haki bila kucheleweshwa na kumpunguzia gharama ya uendeshaji wa shauri
mahakamani. Mfano wa namna ya uendeshaji wa
mashauri, utunzaji wa kumbukumbu na yaraka za Mahakama na mawasiliano ya
kiutendaji katika shughuli za kimahakama kwa njia ya mifumo wa TEHAMA,” amesema
Bw. Kukuri.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Watendaji Wakuu wa Mahakama nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika ‘SEAJAA’ na Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya SEAJAA wakiwa wameshika tuzo mara baada ya mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni