Jumamosi, 9 Machi 2024

WATUMISHI WANAWAKE MAHAKAMA PWANI WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Watumishi wanawake wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani wameongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce Mkhoi kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani. 

Akizungumza wakati mgeni rasmi alipotembelea banda la Mahakama, Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Felister Ng’hwelo ambaye alikua msemaji katika banda hilo amebainisha namna Mahakama ilivyopiga hatua kwa kuwa matumizi ya mtandao tangu shauri linaposajiliwa, linaposikilizwa mpaka hukumu hutoka kwa njia ya mtandao.

“Hakuna muda tena wa kusubiri nakala au mwenendo mpaka uchapwe bali kesi inapomalizwa kusikilizwa nakala inatoka kwa wakati kutokana na mfumo unavyoratibu masuala hayo, hivyo hakuna tena ucheleweshaji wa nakala ya  hukumu  wala mwenendo kwa maana kesi inapoisha tu ndio nakala zote zinapatikana,” alisema Mhe. Ng’hwelo.

Sherehe hizo za siku ya wanawake zilifanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya Kibaha katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani Mlandizi, na Mgeni Rasmi katika sherehe hizo alikuwa ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Naser. 

Katika maneno yake ya utangulizi amesema wanawake Mkoa wa Pwani wameazimia kutomuacha mtu yoyote katika mchakato wa maendeleo.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema ‘Wekeza kwa wanawake kurahisisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii’ amesisitiza uwekezaji wa fursa za elimu, uongozi, uwezo wa kiuchumi na umiliki ili kufikia lengo la tano la maendeleo endelevu la usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote kufikia malengo.

Ametoa rai kwa wanawake wote kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali zinazojitokeza.

Akinukuu hotuba ya Mkuu wa Mkoa alisema, “Sisi wanaume tuko nanyi bega kwa bega katika kuhakikisha kwamba, haki zenu za msingi zinapatikana.”

Katika sherehe hizo Mkoa wa Pwani umetoa huduma kwa wazee na pia kulikuwa na michezo mbalimbali iliyofanyika yote ikilenga kuwaleta pamoja wanawake pamoja na kushirikishana fursa.

Watumishi wanawake wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani wakijiandaa kuelekea Mlandizi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Watumishi wanawake wa Mahakama Pwani wakiwa katika maandamano kuingia kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani jana tarehe 08 Machi, 2024.

Watumishi wanawake wa Mahakama Pwani wakipita mbele ya Mgeni rasmi (hayupo katika picha).


Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha (Pwani), Mhe. Joyce Mkhoi (kulia) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai (kushotO wakiwa katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mlandizi.

Watumishi wanawawake Mahakama Kibaha wakimpokea Mgeni Rasmi wakati wa maonesho ya Siku ya Wanawake yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mlandizi.

 Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Felister Ng’hwelo akimueleza Mgeni Rasmi (hayupo katika picha) kuhusu shughuli za Mahakama wakati alipotembelea banda la Mahakama katika Maonesho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya Mkuranga, Mhe. Khadija Nasir akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni