Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko ameishauri
Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendelea na jitihada zake za kuwaelimisha
wananchi kuhusu uwepo wa kamati za maadili ya Maafisa Mahakama na namna ya
kuwasilisha kwa wakati malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya
Maafisa hao.
Akizungumza na watumishi wa Sekretariet ya Tume ya
Utumishi wa Mahakama jana mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Mkoa alisema wapo wanannchi
wanaoweza kuwa na malalamiko lakini hawajui ni wapi wayapeleke.
”Waelimisheni wananchi ili waweze kuwasilisha kwa wakati
malalamiko yao ndani ya muda wa miezi sita uliowekwa
na Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na
Wilaya ili wapate haki zao”, alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mafunzo waliyopatiwa na
Tume kuhusu namna ya uendeshaji wa kamati hizo yatawasaidia kujinoa zaidi na
kujiweka sawa pindi watakapopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya
Maafisa Mahakama na kuyashughulikia kwa kufuata utaratibu, Kanuni na miongozo
iliyowekwa na Tume.
”Sasa tumepata mwanga, tutakapokuwa tunaendelea kuzipitia
kanuni na mwongozo wa uendeshaji wa kamati hizo, tutaweza kutekeleza vema
jukumu hili muhimu la kisheria”, alisema.
Alisema Ofisi yake itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo
kati yake na Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania na pia
aliipongeza Tume kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za
Maadili hususan Wenyeviti na Makatibu wa Kamati hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mpanda ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya Bi. Jamila Kimaro
aliishauri Tume kuzijengea uwezo
kamati hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Alisema Ofisi yake imekuwa ikitekeleza vema takwa la
kisheria la kuitisha vikao vya kamati mara nne kwa mwaka kama inavyopaswa na
pia kutenga fedha kwa ajili ya kuendesha kamati hizo.
Naye Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
(Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya ameishauri Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya
wilaya ya Mpanda kusimamia nidhamu na maadili ya Mahakimu na kufanya jukumu la
ulezi wa Maafisa hao wanapotekeleza majukumu yao.
Aliwataka Mahakimu kuwa na weledi katika kazi yao na
kuzingatia nidhamu na maadili wanapotekeleza jukumu lao la msingi na la kikatiba
walilopewa la kutoa haki kwa wananchi.
Watumishi wa
Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa mafunzo
kwa wajumbe wa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Rukwa na
Katavi pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuziimarisha
kamati hizo.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo
katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya
Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni