· Waanzisha mnyororo kabambe kudumisha ushirikiano kazini
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma amewaasa watumishi wanawake kutambua nafasi zao na kudumisha upendo, umoja na ushirikiano ili kuleta maendeleo ya kweli katika jamii.
Mhe. Maruma ametoa wito huo jana tarehe 8 Machi, 2024 katika hafla maalumu iliyoandaliwa kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam kusherekea Siku ya Wanawake Duniani.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja baadhi ya watumishi wanawake wa Mahakama kutoka Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu ya Tanzania na Masjala Kuu.
“Tuwekeze katika nafasi ya mwanamke ili tupate maendeleo katika Taifa, haya hayawezi kutendeka kama tutakuwan na upendo wa kweli, umoja na nia ya kutekeleza haya,” alisema.
Alieleza kuwa mwanamke anatakiwa kutambua haki yake na kujiamini pale anapopewa nafasi katika jamii kwani anao uwezo wa kutekeleza majukumu yake bila kuteteleka.
Jaji Mfawidhi alitolea mfano wa Viongozi wanawake ambao wanafanya vizuri kwenye maeneo ambayo wameaminiwa na hawajawahi kufikishwa mahakamani.
“Tuna Viongozi wengi ambao wanafanya kazi vizuri katika maeneo yao, ni wangapi ambao mmesikia wamepelekwa mahakamani, hakuna,” alisema na kuwaomba kutambua haki zao na kujenga ndani katika familia na kazini,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando amewaomba watumishi wenzake kusimama imara kwani wao ni nguzo muhimu katika jamii.
Alisema kuwa ingawa mwanaume ndiyo kichwa cha familia mwanamke anayo nafasi kubwa zaidi katika kuimarisha ustawi katika jamii na Taifa kwa ujumla.
“Ebu tujiulize ndugu zangu. Wanasema mwanaume ni kichwa cha familia, kwani kichwa kina viungo vingapi ukilinganisha na kiwiliwili ambayo ndiyo sehemu ya mwanamke. Kwa hiyo, sisi tunaweza na siyo lazima tuwezeshwe na mtu. Sisi wenyewe tukiamua, tunaweza,” alisema.
Hafla hiyo ilipambwa na shamra shamra za hapa pale, ikiwemo kucheza muziki, kupata similizi za kusisimua kuhusu maisha katika jamii na baadaye kupata chakula cha pamoja.
Kabla ya kuhitimisha hafla hiyo, watumishi kutoka maeneo mbalimbali waliunda mnyororo wenye lengo la kuimarisha umoja miongoni mwao, jamboa ambalo linatarajiwa kuongeza ari ya kufanya kazi na kuboresha mahusiano kazini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni