Jumapili, 10 Machi 2024

MAJAJI, MAHAKIMU WANAWAKE MUHIMU KATIKA UTAWALA WA SHERIA, UPATIKANAJI HAKI

·      Ni taa ya usawa, huruma, imani, hekima

·      Huleta meza ya mtazamo chanya, uwiano sawa wa kisheria

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika ngazi zote za uongozi na maamuzi, ikiwemo Mhimili wa Mahakama, ni mhimu katika kukuza utawala wa sheria, usawa na upatikanaji wa haki timilifu

Hayo yamebainishwa leo tarehe 10 Machi, 2024 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa anafungua Kongamano la Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake katika Ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotanna jijini Dar -es -Salaam.

“Tumeona mchango wa Majaji na Mahakimu Wanawake. Wanawake wanasimama kama walinzi wa sheria na taa ya usawa, huruma, imani na hekima. Wanaleta meza ya mtazamo chanya, ufahamu na uzoefu tofauti, uwiano wa kisheria na kukuza jamii inayoshirikishwa zaidi na yenye usawa,” amesema. 

Akimnukuu Mhe. Sandra Day O’Connor, ambaye alikuwa Jaji wa Mwanamke wa Kwanza kuteuliwa mwaka 1981 katika Mahakama ya Juu ya Marekani (Supreme Court), Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa uwepo wa Majaji Wanawake ndani ya Mhimili wa Mahakama una matokeo chanya zaidi ya idadi yao au idadi ya mashauri wanayosikiliza.

“Nawaomba Majaji na Mahakimu wanawake endeleeni kuwa mwanga unaohamasisha wanawake wengine na wasichana kutambua wana nafasi na wana mchango katika mfumo wa utoaji haki na utawala wa sheria Tanzania na Duniani kote,” Jaji Mkuu amesema. 

Amesema takwimu za Mahakama ya Tanzania kuhusu uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali inaonyesha hatua kubwa iliyofikiwa na pia safari ndefu iliyopo. Hadi tarehe 08 Machi, 2024 takwimu zinaonyesha kuwa Majaji Mahakama ya Rufani wapo 35, kati yao Wanaume ni 22, sawa na asilimia 63 na wanawake ni 13, sawa na asilimia 37.

Kwa upande wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu, jumla wapo 26, wanaume wakiwa 17, sawa na asilimia 65 na wanawake tisa, sawa na asilimia 35, huku idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ikiwa 105, wanaume ni 67, sawa na asilimia 64, huku wanawake wakiwa 38, sawa na asilimia 36.

Takwimu zinaonesha pia kuwa Naibu Wasajili jumla wapo 78, kati yao wanaume ni 40, sawa na asilimia 51 na wanawake wapo 38, sawa na asilimia 49, huku idadi ya Mahakimu Wakazi ikiwa 1,126, wanaume ni 567, sawa na asilimia 50 na wanawake wakiwa 559, sawa na asilimia 50.

Katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo, jumla ya Mahakimu wapo 229 na kati yao, 134 ni wanaume, sawa na asilimia 59 na wanawake ni 95, sawa na asilimia 41.

Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa juhudi zimeendelea kufanyika kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia unapewa kipaumbele kwa kuajiri wafanyakazi wa Mahakama katika kada nyingine.

Amesema kuwa katika majukumu ya utawala, wanawake wanachukua asilimia 14 ya nafasi za Wakurugenzi na asilimai 5ya nafasi za Wakurugenzi Wasaidizi na kushikilia uwakilishi mkubwa katika majukumu mbalimbali mengine, kama vile maafisa utumishi na maafisa tawala. 

Nawapongeza Majaji na Mahakimu Wanawake kuwa asilimia za uwepo wenu katika ngazi na nafasi mbalimbali zinatokana na uwezo wenu, na sio asilimia za upendeleo,” Mhe. Prof. Juma amesema.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA), ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake ni utekelezaji wa Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwaka 2021 kuwa kila tarehe 10 Machi ni siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.

Amebaisha kuwa lengo kuu la siku hiyo ni kusherekea na kutambua mchango mkubwa anaotoa Jaji au Hakimu mwanamke katika utawala wa sheria na usimamizi wa utoaji haki. “Siku ya leo inaashiria kuwa Mahakama zetu zinatambua na kuthamini siyo tu usawa wa kijinsia, bali pia uwakilishi wa wanawake katika utoaji haki,” amesema.

Mhe. Sehel ameeleza pia kuwa katika kusherekea na kutambua mafanikio ya mwanamke aliye kwenye nafasi ya utoaji haki ni muhimu kutafakari changamoto na ushindi ambao umeunda safari ya chama hiyo mpaka hapo walipo.

Ameeleza kuwa historia ya Tanzania inaonesha Mahakama za Tanzania zilianza kuwa na mwanamke katika nyanja ya utoaji haki mwaka 1970 baada ya Mhe. Eusebia Munuo, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani mstaafu kuteuliwa kuwa Hakimu Mkazi wa kwanza mwanamke.

“Kwa wakati huo kulikuwa na sheria maalum ambayo ilikataza wanawake kuwa Wazee wa Baraza. Kwa hiyo unaweza kujiuliza katika kipindi hicho aliwezaje kufanya kazi mpaka akafika ngazi ya juu kabisa ndani ya Mahakama,” amesema.

Mhe. Sehel ameeleza pia kuwa miaka mitatu baadaye, Mhe. Julie Manning akateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na historia inaonesha alikuwa Mwanafunzi wa kwanza mwanamke Tanganyika na pia mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kusomea Shahada ya Sheria katika Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1963.

Naye Mwakilishi wa UN Women, Bw. Peterson Magoola, ameeleza kuwa Mahakama inaweza kunufaika pakubwa kutokana na kuongezeka kwa uwepo wa majaji wanawake, kuboresha imani na uzoefu kwa wanawake na makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuachwa nyuma.

“Hadi hivi majuzi, masimulizi ya ushiriki wa wanawake katika utumishi wa umma na sekta binafsi kwa kiasi kikubwa yalilenga wanawake katika siasa, huku kukiwa na umakini mdogo kwa sekta kama vile haki,” amesema.

Bw. Magoola amesema Majaji wanawake huleta mitazamo na uzoefu tofauti, wakiongeza imani katika Mahakama kwa kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu, huku wakiakisi jamii inayowakilisha.

Hata hivyo, amesema wanawake wanaendelea kuwakilishwa kwa kiwango cha chini katika ofisi za Mahakama na taaluma ya sheria kote ulimwenguni.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa anafungua Kongamano la Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake katika Ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotanna jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Machi, 2024.


Mwakilishi wa UN Women, Bw. Peterson Magoola akifafanua jambo alipokuwa anawasilisha salamu kwenye Kongamano hilo.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (juu na chini) waliohudhuria Kongamano hilo.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu (juu na chini) na Viongozi wa Mahakama wakifuatilia kilichokuwa kinajiri.

Sehemu ya Naibu Wasajili  na Mahakimu Wakazi (juu na picha mbili) ikiwa katika Kongamano hilo. 



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea zawadi maalum iliyoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa ajili yake. Wengine wanaoshuhudia ambao ni Meza Kuu ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama ya Rufani Mstaafu, Mhe. Eusebia Munuo (wa kwanza kulia) na Mwakilishi wa UN Women, Bw. Peterson Magoola ( wa kwanza kushoto).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na Viongozi wengine wa Meza Kuu wakikata keki kuashiria ufunguzi wa maadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa TAWJA. Picha chini ikiwa katika na wajumbe wa Sekretarieti.


Wanachama wa TAWJA (juu na chini) wakijimwaga uwanjani kusherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake.










 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni