Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma
Jumla ya Wadau 64 wanahudhuria mafunzo ya siku tano ya namna ya kushughulikia mashauri ya Watoto mahakamani lengo likiwa ni kuboresha uendeshaji bora wa mashauri hayo ili hukumu zinazotolewa zizingatie ulinzi wa haki za mtoto kwa mujibu wa Sheria za Nchi na Mikataba ya Kimataifa ya haki za mtoto.
Mafunzo hayo yalifunguliwa jana tarehe 11 Machi, 2024 na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile ambaye amewataka wasimamizi wa mashauri za watoto kuzingatia haki za mtoto kulingana na sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za Watoto ambayo Serikali ya Tanzania imeridhia.
“Uendeshaji wa mashauri ya mtoto una tofauti kubwa katika uendeshaji wake ukilinganisha na mashauri mengine hivyo kumekuwa na changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau kwenda pamoja katika kusimamia mashauri hayo hasa kwa watoto wanaokinzana na sheria,” alisema Jaji Rwizile.
Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanawahusisha Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, Waendesha Mashtaka, Maafisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri, Watoa Msaada wa Sheria kutoka Taasisi mbalimbali na Wasaidizi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama.
Akizungumzia mafunzo hayo Afisa Ulinzi na Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Enna Obama alisema kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa Wadau wote katika kusimamia mashauri ya Watoto mahakamani wengi bado hawajui Sheria na taratibu za kumlinda mtoto hasa wanaofanya makosa hivyo wadau wengi wanataka watoto hao kushughulikiwa kama wahalifu wengine.
Bi. Anna aliendelea kusema kwamba, pamoja na changamoto ya kushughulikia Watoto wenye makosa bado zipo changamoto kwa kesi za Watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kwa kesi hizo kuishia Polisi bila kufika Mahakamani zinaisha katika mazingira ambayo hayatoi haki kwa mtoto inavyostahili hivyo mafunzo hao yameandaliwa kuwafundisha wadau hao kujua haki za Watoto na namna ya kusimamia mashauri kulingana na haki zao.
Naye Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashtaka mkoa Kigoma, Bw. Nestory Kulula alisema kuwa, bado changamoto ipo kwa wadau wanaofungua mashtaka dhidi ya Watoto hivyo kutaka Watoto hao kushughulikiwa kama watu wengine wakati kuna tofauti kubwa ya uendeshaji wa kesi hizo
Wakili huyo wa Serikali alisema kutokana na shinikizo kutoka kwa wadau wanaofungua mashtaka wakati mwingine imewafanya wasimamizi wa mashauri ya Watoto kutoa hukumu ambazo hazizingatii haki za kumlinda mtoto hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwajenga wadau wote kutekeleza majukumu yao kulingana na Sheria zinazomlinda mtoto.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi kutoka Kanda ya Kigoma baada ya hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo ya jinsi ya kuendesha mashauri ya Watoto. Kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na kushoto ni Mratibu wa Masuala ya Haki ya Mtoto, toka Chuo cha uongozi wa Mahakama IJA, Bi. Helena Gabriel.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitoa hotuba ya ufunguzi jana tarehe 11 Machi, 2024 kuhusu mafunzo ya jinsi ya kuendesha mashauri ya watoto yanayotolewa kwa watumishi wa Mahakama na Wadau wake katika ukumbi wa 'The Warreth' mkoani Kigoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wasaidizi wa Kumbukumbu kutoka Kanda ya Kigoma na Tabora wanaoshiriki mafunzo. Kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na kulia ni Mratibu wa Masuala ya Haki ya Mtoto kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Bi Helena Gabriel.
Afisa Ulinzi na Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Enna Obama akitoa ujumbe wake kutoka Shirika hilo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano (5) ya jinsi ya kuendesha mashauri ya watoto yanayotolewa kwa watumishi wa Mahakama na Wadau wake.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni