Na Paul Pascal, Mahakama Moshi
Viongozi na watumishi wanawake wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Lilian Mongella waliadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea Kituo cha wazee wasiojiweza kilichopo Kata ya Njoro Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Zoezi hilo lililofanyika tarehe 08 Machi, 2024 liliongozwa na Jaji Dkt. Lilian Mongella kwa kutembelea Kituo hicho cha wazee wasiojiweza Njoro chenye jumla ya wazee 18 ambapo 12 kati yao ni wanaume na 6 ni wanawake.
Akizungumza katika Kituo hicho, Jaji Mongella alisema, “sisi kama wanawake tunao wajibu wa kuwajali wazee wetu kwani wazee ni hazina ya Taifa letu niwasisitize na kuwaasa wanawake wenzangu tuwe na utamaduni wa kile kidogo tunachokipata kuwakumbuka wazee wetu haswa wazee wasiojiweza kama tunalivyofanya leo.”
Alisema kama wanawake wana wajibu wa kuwatunza wazee katika jamii na kuwasihi kujiwekea utaratibu endelevu wa kuwajulia hali, kuwapatia mahitaji muhimu kadri wanavyojaaliwa ili nao waone furaha ya kuwa katika ulimwengu huu.
Naye, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe alipongeza uratibu uliofanyika wa kufanikisha jambo hilo na kusema kuwa, wamechagua fungu lililo jema.
“Napongeza uratibu wa zoezi hili, kwakweli tumechagua fungu lililo bora kwa kuwapa faraja wazee wetu kwa hiki tulichojaaliwa, niushukuru Uongozi wa Kituo hiki kwa juhudi zao za kuwahudumia wazee hawa wasiojiweza pia niombe zoezi hili liwe endelevu,” alisema Mhe. Simfukwe.
Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje alisema kuwajali na kuwatunza wazee ni ibada na kusema kuwa wao wamefanya hivyo, ameomba jambo wanapaswa kulienzi na kulitekeleza mara kwa mara kila wanapojaaliwa chochote.
Naye, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala alibainisha kuwa, katika siku hiyo, walifanikiwa kuwapatia wazee wa Kituo cha Njoro vifaa vya matumizi ya kila siku pamoja na nafaka kwa ajili ya vyakula vyao vyote hivyo vikiwa vimepatikana kupitia michango ya wanawake wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni