Jumapili, 10 Machi 2024

WANAWAKE WA MAHAKAMA KIGOMA WAUNGANA NA WENZAO KUSHEREHEKEA SIKU MWANAMKE DUNIANI

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye amewataka wanawake wa Mkoa huo kusimama katika  nafasi zao katika kuleta maendeleo na mafanikio  kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Andengeye aliyasema hayo tarehe 08 Machi, 2024 katika maadhimisho ya Siku Wanawake Duniani ambayo kimkoa yalifanyika katika kijiji cha Makere Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

“Wanawake wana fursa sawa na wanaume katika kipindi hiki ambacho jamii inamhitaji mwanamke kuwa kiongozi katika ngazi zote hivyo ni muhimu wanawake msimame katika nafasi zenu,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Aidha, aliwakumbusha juu malezi ya familia ili kuwa na jamii yenye maadili mema na kushiriki katika shughuli zote za kiuchumi.

 Kadhalika, aliwapongeza wanawake ambao wapo katika nafasi mbalimbali kwa jinsi ambavyo wanafanya vizuri katika kuharakisha maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla. Amewataka kuwa Viongozi wa familia ili kuondoa migogoro ya familia lakini kupunguza mateso kwa watoto wanaoteseka pale ndoa inapovunjika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kigoma, Bi. Agripina Buyogela, alisema anaishukuru Serikali kwa kuwawezesha wanawake katika nafasi mbalimbali na kuwa nguzo ya familia na Taifa kwa ujumla na kuitaka iendelee kumpa kipaumbele mwanamke ili kutimiza kaulimbiu ya Siku ya Wanawake ya mwaka huu 2024.

Watumishi wanawake wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakiongozwa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva Mushi waliungana na  wanawake wenzao Duniani katika sherehe hizo zilizopambwa na ngoma, kwaya na michezo mbalimbali kutoka kwa wasanii wa mkoani humo. 

Maadhimisho hayo yaliongozwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Wekeza kwa Mwanamke kuharakisha Maendeleo na Ustawi wa Jamii.’

 

Watumishi wanawake wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2024. Wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akitoa hotuba yake katika sherehe za Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika Kijiji cha Makere wilayani Kasulu tarehe 08 Machi, 2024.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni