Na Naomi Kitonka, Mahakama- Temeke
Katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani jana tarehe 08 Machi, 2024, Watumishi wanawake wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke (IJC Temeke) wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Mwanabaraka Mnyukwa waliadhimisha Siku hiyo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ndoa, mirathi na watoto ili kukuza uelewa juu ya masuala hayo.
Zoezi la utoaji elimu lilifanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuendelea kutoa elimu ya ya masuala ya kesi za ndoa, mirathi na watoto na kuwasaidia kupata haki zao kwa wakati.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi katika sherehe hizo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw. Sixtus Mapunda aliwapongeza watumishi hao kwa juhudi zao katika kutambua umuhimu wa wananchi kujua na kuelewa haki zao kwenye masuala ya ndoa, familia na mirathi.
“Mahakama imekuwa ni chombo kinachokua na kuendelea na kimefanyika kuwa mzani kwa watu wa namna zote na kwa kutambua kazi ya Mhimili huu wenye nguvu juhudi zenu za kuwaelimisha wananchi kutambua haki zao ni jambo la muhimu sana ambalo litasaidia kukuza mahusiano kati ya Mahakama na wananchi,” alisema Mhe. Mapunda.
Aidha, Mgeni maalum wa maadhimisho hayo ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi-Kituo Jumuishi cha asuala ya wa Kituo hicho, Mhe Jaji Mwanabaraka Mnyukwa alizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema ”Wekeza kwa wanawake kurahisisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii” ambapo amesisitiza kwamba katika kuhakikisha Mahakama inalinda haki za wanawake, Vituo Jumuishi vya utoaji haki vimeanzishwa kwa lengo la kuleta haki kwa haraka wakishirikiana na Wadau mbalimbali wa Sheria mfano watu wa Ustawi wa Jamii na wa Msaada wa Sheria.
Mhe. Mnyukwa alizungumzia pia athari za wananchi kukosa elimu ambapo alisema “changamoto ya wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu uelewa wa Ndoa, Mirathi na Watoto hupelekea wengi kuingia kwenye mgogoro wa kushindwa kufungua na kufunga mashauri kwa wakati na kuwazuia wengi kutokuwa na utulivu wa akili.”
Katika maadhimisho hayo pia, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Rehema Mwaisaka alitoa elimu kwa wananchi kuhusu Ndoa ambapo alizungumzia Sheria ya Ndoa na namna inavyofanya kazi, sababu zinazopelekea Mahakama kuvunja Ndoa na pia haki za wadaawa ikiwemo mgawanyo wa mali na matunzo ya watoto.
Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Orupa Mtae alisema, Mahakama hiyo inashughulikia kesi za jinai na kesi za madai ambapo kesi hizi zote zinaanzia Ustawi wa Jamii ikiwemo kesi za makazi na ulinzi wa mtoto, haki za mtoto na kuthibitisha uzazi.
Wananchi pia walipata elimu kuhusu Mirathi kutoka kwa Jaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Jaji Asina Omari ambapo alielezea kwa kina majukumu ya msimamizi wa mirathi na umuhimu wa kufungua mirathi mapema na kuacha wosia.
“Jukumu la msimamizi wa Mirathi ni kutambua na kusimamia mali za marehemu, kufuatilia na kulipa madeni ya marehemu na kusimamia ugawaji wa mali za marehemu na kwa kuwa Kifo ni hakika kwa watu wote na ndugu zetu watatakiwa kufungua Mirathi hivyo ni wajibu wetu kuacha wosia kwa ndugu zetu ili kuepusha migogoro baada ya kufariki,” alisema Jaji Asina.
Naye Mhasibu wa Kituo hicho, Bi. Sophia Sevuri alizungumzia taratibu za malipo ya Mirathi na aliwasisitiza wananchi kuwa mtu yoyote asiwadanganye kuwa anao uwezo wa kurahisisha na kuharakisha malipo ya Mirathi na Malipo yote yanafanyika kwenye mifumo ya Serikali.
Aidha, Watumishi hao walianza shamrashamra kwa Maadhimisho ya Siku hiyo katika ukumbi wa mikutano kituoni hapo kabla ya kuhamia katika viwanja vya Mbagala Zhakhiem ambapo wanawake wote pamoja na watumishi wengine wa Mahakama walipata nafasi ya kujifunza na kukumbushana mambo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na uwekaji wa akiba katika mifuko ya jamii kutoka kwa mwezeshaji kutoka UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga pamoja na mbinu za kujiamini kutoka kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Upendo Kapama.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwezeshaji kutoka ‘UTT AMIS’ alisema, “ili ufanikiwe katika masoko ya mitaji ni muhimu kama mwekezaji aanze mapema na kuweka kiasi cha fedha mara kwa mara na kuweka mipango ya uwekezaji huku ukijua hatari za uwekezaji itasaidia kuwa vizuri zaidi.”
Naye, Jaji wa Kituo hicho, Mhe. Sharmillah Sarwatt alipewa nafasi ya kushirikisha wanawake alipopitia kwenye utumishi wake mpaka sasa ambapo alisema, “Mwanamke ni moja kati ya watu wachache wenye majukumu mengi sana ambao wamepewa uwezo wa kuyafanya hayo yote na mwanamke wa namna hiyo ana akili sana na katika miaka yote ya kufanya kazi mahakamani nimegundua kuwa Mawingu ni mwanzo tu wa mafanikio na siyo mwisho kama wanavyosema hivyo wanawake msiache kutumia fursa yoyote hata kama ni ndogo katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.”
Sherehe hiyo ilipambwa na matukio kadhaa ikiwemo utoaji zawadi kwa Wanawake Hodari, ukataji wa keki, muziki na kushiriki chakula kwa pamoja.
Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyeketi katikati) pamoja na Majaji wengine wa Kituo hicho wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi Wanawake wa Kituo hicho wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2024.
Mwezeshaji kutoka Shirika la UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga akitoa elimu ya uwekezaji kwa watumishi wanawake wa IJC Temeke.
Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akitoa zawadi ya cheti kwa mwanamke hodari, Bi. Queen Mwakubombaki.
Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Jaji Mwanabaraka Mnyukwa (katikati) pamoja na wenzake wakifurahia jambo pamoja na Majaji wenzake na Naibu Msajili wa Kituo hicho. Wa kwanza kulia ni Mhe. Jaji Sharmilla Sarwatt, wa pili kulia ni Mhe. Asina Omari, wa pili kushoto ni Mhe. GladysNancy Barthy na wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Evodia Kyaruzi.
Jaji wa Mahakama Kuu kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Jaji Asina Omari akijibu swali kutoka kwa mwanachi (Hayupo pichani) katika siku ya Maadhimisho ya Wanawake katika viwanja vya Mbagala Zakhiem.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni