Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Levira amewaomba wadau wote wa maendeleo kuwekeza zaidi kwa wanawake kwani wao ni nguzo katika jamii inayochochea uharakishaji wa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
Mhe. Dkt. Levira ametoa rai hiyo leo tarehe 8 Machi, 2024 alipokuwa anazungumza na watumishi wanawake wa Mahakama ya Rufani kama Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
“…. kama ilivyo dhamira ya kuiletea nchi yetu maendeleo ya haraka na ustawi wa jamii, ni wakati muafaka sasa wa kuwekeza kwa wanawake kwani tumeweza kujipambanua kuwa tunaweza,” amesema.Kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka 2024 inasema: “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.”
Mhe. Levira amebainisha kuwa tunapozungumzia uwekezaji kwa wanawake, tunamaanisha kuwa, ili mwanamke aweze kuleta faida inayotarajiwa kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii, ni lazima wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla waone umuhimu, pamoja na mambo mengine, kuwaelimisha, kuwashirikisha, kuwafanya wajiamini na kuwapatia mitaji au kumwezesha wanawake kiuchumi.
“Pengine niseme kwa kifupi kuwa, wanamke wa nyakati tulizonazo wanahitaji kupata taarifa sahihi za mambo mbalimbali zitakayomwezesha kusimama katika nafasi zao na kutimiza majukumu yao ili kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii. Kwani ni jambo lisilo na ubishani kuwa wanawake anachangia nafasi iliyo kubwa kiustawi na maendeleo kuanzia katika ngazi ya familia, jamii, Taifa na hata kimataifa,” amesema.
Jaji Levira ameeleza kuwa jambo hilo siyo geni kwani kuna wanawake wengi ambao, bila shaka, mchango wao ni mkubwa kwa Taifa. Akamtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anafanya mambo makubwa ya maendeleo na ustawi wa Nchi.
Amewataja pia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Pindi Chana, Wasajili wanawake, Mahakimu na watumishi wanawake katika ngazi mbalimbali za utumishi mahakamani na katika Serikali ambao matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa kwao kutokana na kazi zao yanaonekana.
“Mifano michache ya wanawake niliyotoa itoshe kuonyesha kuwa kama ilivyo dhamira ya kuiletea Nchi yetu maendeleo ya haraka na ustawi wa jamii, ni wakati muafaka sasa wa kuwekeza kwa wanawake kwani tumeweza kujipambanua kuwa tunaweza,” Mhe. Levira amesema.
Akabainisha pia kuwa Dunia inakwenda kwa kasi katika maendeleo ya sayansi na teknologia, hivyo wanawake wote hawana budi kutumia fursa hiyo adhimu kujiwekea mazingira ya utayari ili kuruhusu uwekezaji wenye tija kwao kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
“Kwamwe maendeleo haya yasitupeleke katika kutafuta na kudai mambo yasiyo na faida kwa maendeleo yetu binafsi na jamii kwa ujumla,” Mhe. Levira akasisitiza.
Maadhimisho hayo ambayo yalihudhuriwa na Majaji Wanaume kadhaa wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Mhe. Zepharene Galeba na Mhe. Sam Rumanyika pamoja na Kaimu Msajili Mkuu, Mhe. Silvester Kainda na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Emmanuel Mrangu, yalipambwa na shamra shamra za hapa na pale huku washiriki wote wakijimwaga uwanjani kusherehesha siku hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni