Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Watumishi wanawake wa Makao Makuu Mahakama ya Tanzania pamoja na wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma leo tarehe 08 Machi, 2024 wameungana na wanawake wenzao kutoka Wizara mbalimbali za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika kimkoa katika viwanja vya Chamwino jijini humo.
Sherehe hizo zilipambwa na shamrashamra mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, maonesho ya ukakamavu yaliyotolewa na Askari wanawake kutoka Jeshi la Uhamiaji, mashairi na kadhalika.
Mgeni Rasmi wa Maadhimisho hayo alikuwa ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Katika hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa na Mhe. Dkt. Gwajima imesisitiza juu ya wanawake kujiunga katika Vikundi mbalimbali vya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.
“Nawasisitiza wanawake kujiunga katika vikundi mbalimbali ili kuondokana na umaskini na kujikwamua kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kwa kuzitaka Taasisi mbalimbali kuendelea kuimarisha mikakati ya kukemea vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na kuwataka wanawake/jamii kutoa taarifa za vitendo hivyo.
Mhe. Gwajima amesema kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi wakiwemo wanawake, huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, umiliki wa ardhi, upatikanaji wa haki ambapo kwa upande wa upatikanaji wa maji amesema asilimia 88 ya wananchi mjini wanapata maji.
Kwa upande wa nafasi mbalimbali za madaraka, imeelezwa kuwa idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi imezidi kuongezeka siku hadi siku huku akitoa mfano wa Majaji wanawake wa Mahakama Kuu ya Tanzania imefikia asilimia 38.1.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Jaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan amesema Mahakama inaendelea kuboresha mifumo ya utoaji haki ikiwa ni pamoja na kuweka usawa wa kijinsia.
Jaji Fatma ametoa rai kwa wanawake, kutenda kazi vizuri ili kuacha hadithi nzuri kwa vizazi na vizazi.
“Hadithi nzuri ni kutenda haki, lakini haki hii itapatikana ipasavyo endapo tu sisi wanawake ambao ndio walengwa Wakuu katika maadhimisho haya, tutashirikiana ipasavyo,” amesema Jaji Fatma.
Katika Sherehe hizo, Waziri Gwajima amezindua Sera Mpya ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 na kusisitiza kuwa kila mmoja ashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera hiyo ili kufanikisha yaliyomo katika Sera hiyo.
Mara baada ya sherehe hizo, watumishi wanawake wa Makao Makuu wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kumbukumbu za Mahakama, Bi. Agnes Bulyota walishiriki kwa pamoja kupata chakula cha mchana pamoja na kukata keki kama ishara ya kusherehekea Siku hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni