Jumatatu, 6 Mei 2024

JAJI BANZI AHIMIZA MATUMIZI YA TEHAMA

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi amewahimiza watumishi kuendeleza matumizi ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe, Banzi alitoa wito huo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama kuu Bukoba hivi karibuni.

Jaji Mfawidhi, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA yamesaidia kwenye shughuli za uendeshaji kazi za Mahakama. 

Mathalani, kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2024, mashauri 964 kwa kanda nzima yamesajiliwa kwa njia ya mtandao. Mashauri 734 yamesikilizwa kwa njia ya mtandao. Malalamiko na mawasiliano ndani na nje ya ofisi yanafanyika kwa njia ya mtandao,” alisema

Mhe. Banzi alieleza pia kuwa uwezeshaji wa kompyuta mpakato kwa Majaji na Mahakimu umesaidia hukumu zote kuchapwa na kutolewa kwa wakati.

“Viongozi na watumishi wenzangu, Mahakama ya sasa ipo kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA, tukubali mabadiliko haya ili kufanya maeneo yetu ya kazi kuwa rafiki,”alisema.

Jaji Mfawidhi amewaelekeza watumishi wote kuendelea kutumia mfumo mpya wa Usimamizi na Uendeshaji wa Mashauri (Advanced Case Management Systems (e-CMS) na pale zinapotokea changamoto ziwasilishwe mapema kwa ufumbuzi.

Awali, Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Kagera, Bi. Jean Mzena alitoa elimu juu ya umuhimu wa vyama vya wafanyakazi, mabaraza ya wafanyakazi na haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa, ambapo kupitia elimu hiyo aliwaasa watumishi na waajiri kutimiza wajibu wao.

Naye Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw.  Edward Mwashitanda ambaye pia alihudhuria kikao hicho, alielezea faida za kutumia mabaraza ya wafanyakazi katika kutatua changamoto za watumishi.

Aliwaomba watumishi kujiunga na TUGHE kwa wingi ili kuendelea kukipa chama hicho nguvu ya kuwasilisha masuala mbalimbali kwa mwajiri na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na maslahi yao

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hiyo ni Jaji wa Mahakama Kuu Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Odira Amworo na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ,Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi akitoa neno la ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda Bukoba.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ,Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi akiongoza kikao hicho. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana na kulia ni Katibu wa Baraza hilo, Bi. Febronia Serapion.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Bukoba, Bw. Lothan Simkoko akiwasilisha taarifa ya utekelezaji  wa majukumu ya Mahakama Kanda ya Bukoba kwa mwaka 2023/2024 katika Baraza la Wafanyakazi.

 Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Kagera, Bi. Jean Mzena akitoa elimu juu ya umuhimu wa vyama vya wafanyakazi, mabaraza ya wafanyakazi na haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa.

Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw. Edward Mwashitanda akitoa mada ya umuhimu wa mabaraza ya wafanyakazi. Kulia ni Afisa Kazi Mkoa wa Kagera, Bi. Jean Mzena wa pili kulia Afisa Utumishi Mahakama Kuu Bukoba, Bi. Monica Kalokola.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ,Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi (katikati walioketi) akiwa na wajumbe wa kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni