Na Mary Gwera, Mahakama-Dar es Salaam
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke
kimefanya Mafunzo ya kubadilishana uzoefu kuhusiana na mashauri ya ndoa na
talaka ili kujenga uelewa wa pamoja kwenye mienendo na maamuzi ya mashauri
yanayoendeshwa katika Mahakama hiyo.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo hayo
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala
ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa aliwapongeza washiriki wote kuweza
kushiriki na kueleza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwa na uelewa wa pamoja
katika mambo ya msingi ya kuzingatia katika maamuzi ya mashauri ya ndoa kwa
kuzingatia msingi wa sheria na taratibu husika.
“Mafunzo haya ni mpango wa uongozi wa Kituo yaani
utawala wa kituo, ambapo Sekretarieti ya mafunzo hupokea maoni kutoka Majaji na
Mahakimu kuhusu maeneo yenye utata na mkanganyiko ili kujenga uelewa wa pamoja
kwenye mienendo na maamuzi,” alisema Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya
Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.
Mhe. Mnyukwa aliongeza kuwa, Mafunzo hayo hulenga kujenga uelewa wa pamoja katika uamuzi wa mashauri ya ndoa na talaka kwa mujibu wa Sheria pamoja na kupeana mbinu za utambuzi na uamuzi ili kuendana na mazingira husika ya mashauri ya ndoa.
Akitoa Mada kuhusu muongozo wa Sheria katika vipengele muhimu ambavyo Mahakimu walipendekeza kuhitaji kupata ufafanuzi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu aliwasilisha kwa kugusa vipengele muhimu ambavyo ni pamoja na Mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kuamua mgawanyo wa machumo kisheria, Taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kujaza fomu za kushindikana kwa usuluhishi wa mashauri ya ndoa kutoka katika Mabaraza ya usuluhishi wa mashauri ya ndoa.
Vipengele vingine alivyofafanua Mhe. Mkwizu ni juu ya Mamlaka ya kisheria kuhusu mashauri ya dhana ya ndoa kwa Mahakama za Mwanzo, Nyaraka zinazopaswa kuwasilishwa mahakamani wakati wa kufungua mashauri ya ndoa na dhana ya ndoa.
Kadhalika, Jaji Mkwizu alizungumzia kuhusu Uhalali wa kutoa hati ya talaka kwenye dhana ya ndoa kisheria, upokeaji wa ushahidi wa kielektroniki katika Mahakama za Mwanzo.
Baada ya Wasilisho, washiriki walipata nafasi ya majadiliano na kuazimia kuwa, Mgawanyo wa machumo uzingatie msingi wa Sheria kwa kuzingatia Mchango wa Wanandoa katika upatikanaji wa mali husika na kanuni ya usawa (fairness), Mabaraza ya Usuluhishi yanapaswa kueleza maoni yake kwenye fomu namba 3 kwa uwazi kuhusu kushindikana kwa usuluhishi.
Maazimio mengine yaliyofikiwa katika Mafunzo hayo ni kwamba, Mahakama ya mwanzo ina mamlaka ya kushughulikia mashauri ya dhana ya ndoa kwa mujibu wa Sheria kama Mahakama zingine kwakuwa Mahakama ya Mwanzo, Wilaya na Kuu zina mamlaka sawa kuhusu mashauri ya ndoa na talaka.
Mengine ni Mahakama ya Mwanzo ijikite kutumia Kanuni
za Ushahidi katika Mahakama za Mwanzo katika kupokea ushahidi na sio Sheria ya Ushahidi
hasa kwenye ushahidi wa kielektroniki na kadhalika.
Akifunga Mafunzo hayo, Jaji wa Kituo Jumuishi
cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Gladys Barthy alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa
kuandaa mafunzo hayo na vilevile alimshukuru Jaji Mkwizu kwa uwasilishaji mzuri
na kuwashukuru washiriki wote kushiriki katika Mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 03 Mei, 2024
katika Kituo hicho kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam ni moja ya mfululizo
wa mafunzo ya ndani ya Kituo hicho kwa ajili ya Majaji na Mahakimu wanaohudumu
katika Kituo hicho ambayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu (3).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni