Jumamosi, 4 Mei 2024

MAHAKAMA MOSHI YAMFARIJI MTUMISHI ALIYEATHIRIKA KWA MAFURIKO

Na Paul Pascal-Mahakama, Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Dkt. Lillian Mongella ameungana na baadhi ya watumishi wa Mahakama kumjulia hali na kumfariji mtumishi mwenzao aliyepatwa na janga la mafuriko mnamo usiku wa kuamkia tarehe 25 Aprili, 2024 nyumbani kwake mtaa wa Langoni kata ya Mji Mpya Wilaya ya Moshi.

Mtumishi huyo Bw. Mussa Mssekeni ambaye ni Mlinzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi anayeishi katika mtaa wa Langoni Kata ya Mji Mpya Wilaya ya Moshi alikumbwa na mafuriko hayo kutokana na mvua kubwa iliyopelekea kujaa kwa mto Rau na kuacha familia nyingi katika Kata hiyo bila makazi na mahitaji ya kibinadamu.

Akizungumza wakati wa kumfariji mtumishi huyo Mhe. Dkt. Mongella alisema, anamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai aliowajalia hadi kufikia siku ya hiyo maana janga hilo limeagharimu maisha ya watu, akamuomba mtumishi huyo kuwa na subra katika kipindi hicho anachokwenda kuanza kuijenga familia upya hasa akizingatia anaanza kujitafutia upya mahitaji kwa ajili ya maisha ya kila siku ya familia.

“Msifadhaike kwa kupoteza vitu katika makazi yenu sisi ni sehemu ya familia hii. Ndiyo maana leo tumefika hapa na mkono wa pole ili maisha yaweze kuendelea. Yatupasa pia kuchukua taadhari pale tunapoona hali sio shwari kwa muktadha wa maisha yetu, kama Kanda tunawapa pole sana kwa kadhia ya mafuriko”, alisema Mhe. Dkt. Mongella

Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Bw. Paul Mushi alieleza kuwa vitu mbalimbali vilivyowasilishwa kwa mtumishi huyo ni ishara ya umoja na upendo uliopo baina ya Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.

“Ni utaratibu tuliojijengea kusaidiana pale anapotokea mmoja wa watumishi anapatwa na tatizo hivyo kwa siku ya leo kupitia michango ya watumishi wa Kanda hii tumeweza kuwasilisha kwa mwenzetu vitu vya nyumbani kama Godoro, jiko, vyombo vya kulia chakula, nguo za watoto, blaketi, sabuni pamoja na vyakula kama mchele, unga, mafuta na sukari niwashukuru watumishi wenzangu kwa ushirikiano huu mliouonyesha,” alisema Kaimu Mtendaji huyo.

Kaimu Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Bw Paul Mushi (katikati mwenye t-shirt nyeupe) akitoa salamu za pole wakati wa tukio la kumfariji mtumishi mussa msekeni aliyekumbwa na mafuriko nyumbani kwake kata ya mji mpya moshi 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Mhe. Dkt. Lillian Mongella akimkabidhi vifaa mbalimbali vya matumizi ya nyumbani na chakula kwa mtumishi mussa msekeni aliyekumbwa na mafuriiko.

Sehemu ya watumishi wakiwa wamebeba vifaa vya matumizi ya nyumbani kuelekea kumfariji mtumishi mwenzao aliekumbwa na mafuriko nyumbani kwake mji mpya moshi

Sehemu ya watumishi wakiwa wamebeba vifaa vya matumizi ya nyumbani kuelekea kumfariji mtumishi mwenzao aliekumbwa na mafuriko nyumbani kwake mji mpya moshi


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Mhe. Dkt. Lillian Mongella akimkabidhi mkono wa pole mtumishi Mussa Msekeni aliekumbwa na mafuriko.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama) 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni