Ijumaa, 3 Mei 2024

NGUZO NAMBA MBILI YA MKAKATI WA MAHAKAMA YATEKELEZEKA KWA VITENDO PWANI

Na Mary Gwera, Mahakama - Pwani 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imefanikiwa kutekeleza nguzo namba mbili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa Mwaka 2020/2021 – 2024/2025 kwa kusikiliza na kuamua jumla ya mashauri 9,760 kwa mwaka 2023 ikiwa ni sawa asilimia 105.6 ya utekelezaji. 

Hayo yalibainishwa Mei 02, 2024 na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga, akifanya mahojiano maalum na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami. 

“Katika kutekeleza na kuzingatia, nguzo namba mbili (2) ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania jitihada kubwa za Mahakama mkoani Pwani zinafanyika katika kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa mahakamani yanafanyiwa kazi kwa kuzingatia miongozo iliyopo na viwango vilivyowekwa,” amesema Bw. Minga. 

Amefafanua kuwa, kati ya mashauri yaliyosajiliwa, ni mashauri 118 yaliyomalizika katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi/ Mkoa, mashauri 2,890 katika Mahakama za Wilaya na mashauri 6,752 katika Mahakama za Mwanzo. 

Ameongeza kuwa, mashauri yaliyobaki kufikia Desemba, 2023 katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi yalikuwa 32, katika Mahakama ya Wilaya yalikuwa 519 na katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo yalikuwa mashauri 278. 

“Takwimu hizo zinaonesha kuwa, Mahakama ya Mkoa iliweza kufikia kiwango cha umalizaji mashauri (clearance rate) kwa asilimia 92.3 kuwa na wastani wa kasi ya uondoshaji wa mashauri kwa asilimia 78.6, kasi ya umalizaji wa mashauri kwa Mahakama za Wilaya ilikuwa asilimi 83.3 na katika Mahakama za Mwanzo kwa kasi ya asilimia 100,” amefafanua Bw. Minga. 

Akizungumzia mafanikio mengine ya Mahakama hiyo, Mtendaji huyo amesema, imefanikiwa kufanya ukaguzi wa Mahakama za chini kama ilivyopangwa kwa kila robo ya mwaka wa fedha kuendana na taratibu zinavyoelekeza. 

Akizungumza mara baada ya mahojiano yake na Mtendaji huyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami, ameeleza kuwa pamoja na kufahamu mafanikio ya Mahakama hiyo  malengo mengine ya ziara yake katika Mahakama hiyo na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) ambavyo atatembelea ni kufahamu kiwango cha mridhiko na imani ya wanufaika katika upokeaji wa huduma za Mahakama/ Vituo hivyo ikiwa ni pamoja na idadi ya mahudhurio yao katika huduma hizo na manufaa yake kwa Taifa. 

Pamoja na hilo Mkuu huyo wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Mahakama ya Tanzania, alisisitiza kufanyika kwa uhamasishaji wa Watumishi na Wananchi katika kutemebelea kurasa rasmi za Mahakama ya Tanzania katika Mitandao ya Jamii zikiwemo Tovuti (www.judiciary.go.tz)  na Blogu (tanzaniajudiciary.blogspot.com) na kurasa za Mitandao ya Kijamii ya Mahakama, ili kupata elimu ya huduma zitolewazo pamoja na taarifa mbalimbali za Mahakama. 

Mpaka sasa Mkuu huyo wa Kitengo tayari ametembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kwa Wananchi Mkoani Dodoma, Morogoro, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani pamoja na eneo ambapo kitajengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoani Pwani ambacho hadi sasa kibali cha ujenzi wake tayari kimepatikana anasubiriwa mkandarasi kuanza kazi. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (kulia) akizungumza jambo na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami alipotembelea Mahakama hiyo jana tarehe 02 Mei, 2024.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami akisaini kitabu cha wageni alipofika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga.
Mahojiano kati ya Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga (aliyeketi mbele) na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami yakiendelea. Kulia ni Afisa Tawala Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bi. Stumai Hoza.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga (wa pili kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami (wa pili kulia) na sehemu ya Maafisa wengine kutoka Mahakama hiyo.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga (wa kwanza kushoto) akimuonesha Bw. Gerard Chami (wa pili kulia) kiwanja itakapojengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Pwani.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni