Ijumaa, 3 Mei 2024

JAJI MKUU ATETA NA UJUMBE WA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kutumia jukwaa la mkutano wa mwaka na kuwajumuisha Majaji Wafadhidhi, Naibu Wasajili na wawakilishi wa Tume waliopo nchini ili kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kupitia jukwaa hilo ili kusaidia namna bora ya kuboresha utendaji kazi.

Ameyasema hayo leo tarehe 03 Mei, 2024 alipotembelewa Ofisini kwake jijini Dar es salaam na Ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa ajili ya kujitambulisha na kuwasilisha salamu za Kamishana wa Tume hiyo.

“Nikiri tumekuwa tukikutana mara kwa mara lakini katika mwavuli wa shughuli nyingine tofauti ambazo hazitukutanishi kujadili mambo yanayohusu Mahakama na Tume hususani masuala ya utendaji kazi wetu na changamoto tunazozipitia na kuzipatia utatuzi wa kuimarisha utendaji kazi”, amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amesema ni vema Tume inakaona uwezekano wa kutumia kalenda ya kabla ya Siku ya kilele cha sheria nchini kwa maana ya wiki ya sheria kila mwaka. Tume ikaandaa mkutano wa jukwaa la wadau na kutumia fursa hiyo kujadili mambo mbalimbali ya kuboresha shughuli za Tume kutoka kwa wadau ili kuboresha utendaji kazi.

Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa, jukwaa hilo la kila mwaka linapaswa kuwa na kauli mbiu na kualika wadau kutoa mada na mawasilisho na mawasilisho mazuri yatoke hasa kwa wale wadau wanaofanya kazi na kushughulika na matatizo zaidi siyo kutumia wanataaluma wanaofanya kazi kwa nadhalia zaidi

“Nimependa sana uono wako kwamba unapozungumzia uwekezaji shughuli zenu ni muhimu sana katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na pia zinalenga kuwajengea imani wakezaji hasa pale migogoro inapotatuliwa kwa wakati na haki kutendeka”, ameongeza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu amesema uwekezaji unatengemea sehemu ambayo haina migogoro au ina utaratibu wa usuluhishi wa migogoro unaoeleweka. Mwekezaji hataki aende sehemu ambayo anajua kuna mifumo ya kutatua migogoro lakini haieleweki au kuna ucheleweshaji hayo ni maeneo ya kuyazingatia katika vipaumbele vya Tume.

Kwa upande wa eneo la teknolojia, Jaji Mkuu akachua nafsi hiyo kuipongeza Tume kwa jitihada za kusimika mifumo ya kitehama itakayowasaidia kuendesha shughuli za utatuzi wa migogoro hasa matumizi ya mkutano mtandao utakaorahisisha uzikilizaji na utatuzi wa migogoro ya kazi hata pale wasipokuwa na wawakilishi wao kwa kutumia ofisi za taasisi nyingine zenye miundombinu wezeshi.

Jaji Mkuu amesema lengo vilevile la Tume ni kupunguza mashauri ya mapitio yanayowasilishwa mahakamani kwani migogoro ikiweza kuishia kwenye ngazi ya Tume mazingira ya utatuzi wa migogoro itakuwa imeimarika zaidi, kwani mahakamani mdau anachua muda mrefu zaidi kwa wastani wa miaka mitatu hadi nne shauri kumalizika. Wakati mwingine shauri linafika hadi Mahakama ya Rufani na kuamriwa likaanze upya hali hiyo siyo nzuri kabisa hivyo Tume ikiimarisha utatuzi wa migogoro wananchi watapata nafuu kubwa.

“Nahaidi nitaendelea kuwasemea zaidi kwenye majukwaa mbalimbali kwani natambua umuhimu wa Tume ya usuluhishi na uamuzi na pia napenda sana Wizara itambue umuhimu wenu,” amesisitiza Jaji Mkuu.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Wakili Usekelege Mpulla kwa niaba ya Kamishna wa Tume hiyo pamoja na salamu amemweleza Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma kuwa hivi karibuni Tume ilisaini makubaliano ya awali na Mahakama ya kubadilishana nyaraka na kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji na kwa kupitia hiyo Tume itakuwa ikishirikishana na Mahakama kutoa taarifa muhimu na kwa uharaka ikiwemo wito wa majalada ya mashauri na mengineyo yanayofanya kuongeza ufanisi katika utendaji na Mhimili.

 “Mhe. Jaji Mkuu tumeona pia tukushirikishe mikakati ya Tume uisikie na vivile tutakuandikia ili ije kwa ajili ya maelekezo mbalimbali. Tunayo mikakati mbalimbali ya kuweza kuboresha utatuzi wa migogoro ya kikazi moja wapo ikiwa ni kuongeza kasi na ufanisi katika utatuzi wa migogoro na msisitizo wetu ikiwa ni usuluhishi ambao pia ni msisitizo wako”, ameongeza Mkurungezi Mpulla.

Mkurugenzi Mpulla amesema hivi sasa Tume inaendelea na zoezi la usimikaji wa mifumo ya kielektroniki ya utatuzi wa migogoro na usajili kwa njia ya kielektroniki na zoezi lipo katika hatua ya mwisho ya kuzinduliwa ili kuanza kufanya kazi ikiwa pamoja na kuendana na kasi ya mifumo ya uendeshaji wa mashauri ya kimahakama.

Mkakati mwingine ni kuimarisha ushirikiano na wadau ikiwa ni pamoja na Mahakama ambao ni wadau muhimu katika shughuli za utatuzi na uamuzi wa migogoro ya kazi.

Pia, Tume imesaini makubaliano ya awali na Kituo cha Uwekezaji nchini kwani Kituo hicho kazi yake kubwa ni uwashawi wawekezaji kuwekeza mitaji nchini, na wawekezaji ndiyo waajiri na ndiyo wazalishaji wa migogoro ya kikazi. Kufanya kazi na Kituo kwa pamoja kunalenga kushirikiana na kutatua kero mbalimbali za migogoro ya kazi kwa hao wawekezaji.

Aidha, Mkurungezi Mpulla amesema mkakati mwingine ni kuomba Serikali kuwezeshwa kupata magari yatayotumika kama Mahakama Inayotembea kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi wenye migogoro ya kazi hasa maeneo ya kimkakati ili kutoa huduma kwa urahisi zaidi kwa wananchi.

Vilevile maombi ya kuongezewa idadi ya wasuluhishi na waamuzi, kwa upande huo bado rasilimali watu haitoshelezi mahitaji japo Serikali imekuwa ikiongeza lakini siyo kwa kiwango cha kutosheleza mahijati ukilinganisha na migogoro inayosajiliwa ili kuamuriwa kwa wakati, ameongeza Mkurungezi Mpulla.

“Utoaji wa elimu kwa wadau wa Tume, tunatarajia kutoa elimu kwa wadu wetu kwani wakati mwingine migogoro mingine inatokana ukosefu wa elimu ya kutosha ya utatuzi wa migogoro ya kazi. Tume inatarajia kutumia vipindi vya televisheni kama inavyofanya Mahakama ili kuwafikia wadau wengi zaidi,” amesisitiza Mkurugenzi hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua mambo kadhaa wakati alipokutana na Ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Ofisini kwake jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Mei, 2024.


Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Wakili Usekelege Mpulla kwa niaba ya Kamishna wa Tume hiyo akieleza mikakati ya Tume hiyo wakati alipoongoza ujume wa Tume hiyo iliyomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Ofisini kwake.

Sehemu ya Ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi uliofika Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa ajili ya kujitambulisha na kuwasilisha salamu za Kamishna wa Tume hiyo, Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uamuzi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Wakili Vallensi Wambali na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Usuluhishi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Wakili Rodney Matalis.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimsikiliza kwa makini  Mkurungezi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Wakili Usekelege Mpulla alipokuwa akiwasilisha mipango na mikakati ya Tume hiyo kama sehemu ya kuboresha utendaji kazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo wakati wa mkutano na Ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA).

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo wakati wa mkutano na Ujumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA).


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi waandamizi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi mara baada ya kufanaya nao mazungumzo mafupi Ofisini kwake jijini Dar es salaam. 

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni