Alhamisi, 2 Mei 2024

SERIKALI, MAHAKAMA KUSHIRIKIANA KUTATUA MIGOGORO YA WAFANYAKAZI

Na. Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Serikali mkoani hapa imeahidi kushirikiana bega kwa bega na Muhimili wa Mahakama katika kutatua migogoro inayohusu wafanyakazi.

 

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Mei 1, 2024 yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

 

Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na Viongozi mbalimbali na watumishi wa umma na sekta binafsi yalibeba kauli mbiu isemayao “Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga juu ya hali ngumu ya maisha”.

 

Mhe. Malima alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na Mhimili wa Mahakama katika kuwahudumia wananchi, huku akipongeza Viongozi wa Mahakama na watumishi wao kwa kushiriki siku muhimu ya wafanyakazi.

 

“Nashukuru sana leo tupo na Jaji Mfawidhi wa Kanda yetu na ameyapokea yaliyosemwa hapa na kuahidi kuyafanyia kazi. Sisi kama Serikali tutafanya kazi bega kwa bega na Mahakama chini ya uongozi wako ili kuhakikisha migogoro inayowahusisha wafanyakazi inatatuliwa,” alieleza.

 

Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwasihi Waajiri wote wa umma na sekta binafsi kuweka mazingira wezeshi ya kuunda vyama vya wafanyakazi katika Taasisi zao kwa kuwa ni sehemu pekee ambayo mfanyakazi anapata nafasi ya kuwasilisha changamoto zake na kujadili jinsi ya kuboresha maeneo ya kazi na maslahi.

 

 Mhe. Malima alimwagiza Afisa Kazi wa Mkoa kuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo ya kazi ili kujua hali halisi pamoja na kutatua changamoto watakazozibaini.

 

Akitoa salamau za Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor alisema kuwa Mahakama mkoani Morogoro imejipanga vizuri katika kuhakikisha inayasikiliza na kuyamaliza mashauri kwa wakati, ikiwemo mashauri yanayohusu migogoro ya wafanyakazi.

 

Mhe. Mansoor, ambaye aliongozana na watumishi kadhaa, alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Morogoro hawajawahi kuwa na mashauri ya mrundikano yanayohusu wafanyakazi, hivyo ni ishara tosha kuwa mashauri hayo yanasikilizwa na kupewa kipaumbele kwa wakati.

 

“Napenda kuwahakikishia kuwa toka imeanzishwa Mahakama Kuu hapa Morogoro hatuna shauri la mrundikano linalohusu migogoro ya watumishi ambalo lipo kwenye masjala yetu, pale tumejipanga kikamilifu kutoa huduma kwa wananchi,” alisema.

 

Alieleza pia kuwa kwa sasa Mahakama ya Tanzania imejikita katika Matumiza ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo inatumika pia katika kusajili mashauri. 

 

Mhe. Mansoor alitoa wito kwa wananchi iwapo wanakumbana na changamoto zozote wakati wa kusajili mashauri wafike katika Mahakama zilizo karibu ili wapatiwe elimu na namna ya kuutumia mfumo huo.

 

“Tuna kikao maalumu cha kusikiliza mashauri ambacho kitakaa hivi karibuni na miongoni mwa mipangilio yetu tutasikiliza mashauri sio tu ya wafanyakazi bali hata mashauri mengine. Mkakati wetu ni kumpatia mwananchi haki kwa wakati,” alisema.

 

Naye Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Morogoro (TUCTA), Bw. Nicholaus Ngowi, akisoma taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma ya Mahakama Kuu ambayo imerahisisha ushughulikiaji wa mashauri ya migogoro ya wafanyakazi

 

“Tunaishukuru Serikali kuwa sasa tuna Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, imeturahisishia ushugulikiaji wa migogoro ya watumishi. Ombi letu kuwa Serikali pia itaongoza wigo wa kuajiri watumishi wa Mahakama na kuboresha maslahi yao ili kuongeza ufanisi wakati wa ufanyaji kazi,” alisema.

 

Sherehe hizo pia ziliambatana na utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi bora, ambapo kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro na Wilaya zake walitunukiwa vyeti na zawadi.

 


 Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima (wa pili kushoto) akifuatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor wakiimba wimbo wa mshikamano.


 

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima akihutubia wakati wa Siku ya Wafanyakazi.


 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akiwasalimia wafanyakazi katika maazimisho ya siku ya wafanyakazi.


 

Miongoni mwa mtumishi bora kutoka Mahakama Kanda ya Morogoro, Bw. Joseph Madega akipokea cheti cha kuuthamini mchango wake kutoka kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Adam Malima (kushoto).


 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyevaa kofia katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi bora kutoka Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro.



 

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro (juu na picha mili chini) wakiwa katika matukio mbalimbali wakati wa maazimisho ya siku ya wafanyakazi.



 



Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa (kulia), akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni (katikati) na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ifakara wakiteta jambo katika shamra shamra za maazimisho ya siku ya wafanyakazi mkoani Morogoro.

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akicheza pamoja na kwaya iliyokuwa ikitumbuiza katika maazimisho hayo.

 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni