Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Uongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro hivi karibuni uliendesha mafunzo maalumu ili kuwajenga kitaaluma, kimaadili na uongozi watumishi wa kada mbalimbali, wakiwemo Mahakimu Wafawidhi Wilaya na Mahakama za Mwanzo na Wakuu wa Vitengo.
Mafunzo hayo yaliyowajumuisha washiriki zaidi ya 130 yaliyofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 3 Mei, 2024.
Wakati wa mafunzo hayo, watoa mada kutoka ndani na nje ya Mahakama waliwapitisha washiriki kwenye mambo ya msingi ya kuzingatia kwenye shughuli za utoaji haki pamoja na masuala ya kiutumishi na kijamii.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor alisema kuwa wameona umuhimu wa kukaa amoja kujifunza ili kuziba mianya ya tofauti za uelewa juu ya mambo kadha katika utekelezaji wa majukumu, hasa utoaji haki.
“Natambua juhudi mbalimbali ambazo Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi madhubuti wa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamisi Juma umeendelea kuzifanya kwenye kujenga uwezo wa Majaji na Mahakimu. Ndio maana tunafanya juhudi ndani ya Kanda yetu ili kuunga mkono jitahada hizo,” alisema.
Mhe. Mansoor alisisitiza kuwa kila mtumishi wa Mahakama anawajibu wa kuhakikisha haki sio tu kutendeka bali ionekane imetendeka na wala jukumu hilo sio la Majaji na Mahakimu pekee, bali ni la kila mtumishi.
Alisema kila mtumishi wa Mahakama anatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa usahihi na kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Khadija Kinyaka, akizungumza wakati anafunga mafunzo hayo, alisema kuwa ni vyema watumishi wakajuana kupitia kazi zao wanazozifanya.
Alisema kuwa ni imani ya waandaaji wa mafunzo hayo kuwa washiriki watakaporejea katika vituo vyao watakuwa na morali mpya ya kufanya kazi, ujuzi na wataboresha pale palipoonekana kuwa na changamoto.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyekaa katikati), kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Khadija Kinyaka wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Khadija Kinyaka akitoa nasaha wakati akifunga mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akifuatilia mafunzo.
Moja wa wawezeshaji wakitoa mada kwa washiriki.
Sehemu ya washiriki (juu na picha mbili chini) wakifuatilia mafunzo toka kwa wawezeshaji.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni