- Asifu maboresho mahakamani, yamesaidia kupunguza msongamano
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu, leo tarehe 18 Novemba, 2024 amekutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika, ambayo yamesaidia kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Jenerali Katungu, akiwa ameongozana na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Nicodemus Menyiansumba Tenga, aliwasili ofisini kwa Jaji Mkuu iliyopo katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam majira ya saa 3.15 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake kabla ya kufanya mazungumzo mafupi.
Akizungumza baada ya kujitambulisha, Mkuu wa Jeshi la Magereza alimpongeza Jaji Mkuu binafsi na Uongozi wa Mahakama kwa ujumla kwa namna wanavyotekeleza majukumu muhimu, hasa katika utoaji wa haki.
“Yapo mengi ambayo mmefanya, mmeboresha sana shughuli za uendeshaji wa Mahakama. Suala la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa kweli mpo mbali sana. Mnafanya vizuri sana kwenye usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao na hii inaleta nafuu sana kwetu sisi…
“Hili la kuboresha utendaji kazi wa Mahakama limekuwa na mchango mkubwa sana kwetu sisi kama Magereza, hususan kwenye kupunguza msongamano wa Wafungwa na Mahabusu. Nafasi tulizonazo ni kuhifadhi wahalifu jumla 29,902 kwa nchi nzima. Lakini kwa sasa wastani wa wahalifu waliopo ni 27,000,” Jenerali Katungu amesema.
Amemweleza Jaji Mkuu kuwa idadi iliyopo haijafikia uwezo wa Magereza yote wa kuhifadhi wahalifu wote, kwa maana ya Wafungwa na Mahabusu na hilo ni dhahiri linatokana na maboresho ambayo yamefanyika, ikiwemo kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati.
Jenerali Katungu alimweleza Jaji Mkuu pia kuwa usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao umesaidia kuharakisha utoaji haki kwa wakati na umewasaidia kama Magereza kuondokana na hatari ya kuwasafirisha Wafungwa na Mahabusu kutoka magerezani kwenda mahakamani.
Amemwomba Jaji Mkuu kuendelea kushirikiana na Magereza kwenye eneo hilo na kuona namna gani ya kutumia fursa hiyo ili kuboresha utendaji kazi. Kadhalika, Jenerali Katungu aliomba maafisa wake wa TEHAMA kuja kujifunza zaidi kwa wenzao walipo mahakamani.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu, nyinyi mmepiga hatua kubwa sana kwenye matumizi ya mtandao, kasi yenu ni tofauti kidogo na yetu, tunajitahidi lakini bado hatujafika. Naomba kama kuna uwezekano wataalam wetu waje kujifunza zaidi ili na sisi tuweze kusogea na kupiga hatua,” amesema.
Jenerali Katungu pia ameomba matumizi ya adhabu mbadala kwa mujibu wa sheria kwenye makosa madogo madogo na utoaji wa dhamana kwenye makosa yanayodhaminika ili kusaidia kupunguza msongamano magerezani.
Naye Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza alimshukuru Jaji Mkuu kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na wadau wa kila namna. Alisisitiza ombi la kuangalia namna ya kutoa adhabu mbadala kwa watu wenye mahitaji maalum kwani Magereza mengi nchini haya mazingira wenzeshi kwa wafungwa wa aina hiyo.
Kwa upande wake, Mhe. Prof Juma amewashukuru wageni wake kwa kumtembelea kwani Magereza ni mdau muhimu wa Mahakama katika mchakato mzima wa utoaji haki jinai kwa wananchi.
Amesema kitu kinachoisaidia Mahakama kwa upande wa Magereza, pamoja na TEHAMA, ni kuwa na takwimu sahihi za mashauri yaliyopo, hivyo akamwagiza Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert kuwasiliana mara kwa mara na Kamishna wa Sheria wa Magereza ili kuwa na uelewa wa pamoja.
“Kila mwisho wa mwezi, Msajili wa Mahakama ya Rufani huwa ananiletea orodha ya rufaa ambazo zinasubiri kupangiwa vikao. Siyo vibaya kama Msajili atakuwa anampa Kamishna wa Sheria nakala ili kurahisisha usikilizaji wa rufaa hizo,” amesema.
Jaji Mkuu amekubali ombi la Kamishna Jenerali la wataalam wa TEHAMA kukutana na kuagiza utekezaji wa suala hilo kufanyiwa kazi mara moja na kupewa taarifa ya utekelezaji wake.
“Mnayo kila sababu maafisa wenu wa TEHAMA kuja kujifunza. Huwa nasema kama Mahakama za nchi nyingine zinakuja kujifunza, kwa nini nyinyi wadau ambao mpo nyumbani msipate hiyo nafasi.
Nadhani, wewe Msajili wa Mahakama ya Rufani, hili ni eneo la kufanyiwa kazi moja kwa moja. Mtapanga halafu mimi na Kamishna Jenerali mtatupa taarifa wewe na Kamishna wa Sheria, mmepanga lini, au mmekutana lini,” amesema.
Naye Msajili wa Mahakama ya Rufani amewahakikishia wageni hao kuwa kila jambo walilolieleza ambalo linahitaji kushikwa mkono na Mahakama ya Tanzania litafanyiwa kazi kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni