Na CHRISTOPHER MSAGATI –Mahakama, Manyara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Manyara Mhe. John Rugalema Kahyoza, amewaongoza watumishi wa Mahakama
Kuu Kanda hiyo, kufanya ziara ya utalii iliyofanyika jana tarehe 16 Novemba,
2024 katika Hifadhi ya Ziwa Manyara (Lake Manyara National Park) mkoani wa
Arusha.
Akizungumza na watumishi kwa nyakati tofauti
wakati wa maandalizi na hitimisho la ziara hiyo, Mhe. Kahyoza alieleleza lengo
la ziara hiyo ni kuwawezesha watumishi kuwa na uelewa na vivutio vya utalii
vilivyomo nchini ili waweze kuvitangaza kwa watu wengine.
“Kanda yetu ya Manyara ina bahati ya kuzungukwa
na Hifadhi za Taifa, mapori ya akiba pamoja na mbuga za wanyama, hivyo sisi
tuna wajibu wa kuvitambua vivutio hivyo kwa usahihi kwa sababu tumekuwa na
desturi ya kuona wageni wanaotoka mbali ndiyo wanaofika kutembelea maeneo hayo
wakati sisi wenyeji tupo karibu na hatuna uelewa wa vivutio vinavyotuzunguka.
Kwa sababu hiyo tukivielewa vizuri tutakuwa mabalozi wazuri wa kuvitangaza kwa
watu wengine wa ndani na nje ya taifa letu” alisema Mhe. Kahyoza.
Aidha, ziara hiyo iliyotanguliwa na Kikao cha
Majaji na Mahakimu Nchini Tanzania (JMAT) Tawi la Manyara kilichofanyika tarehe
15 Novemba 2024 katika eneo la Mto wa Mbu mkoani Arusha. Mwenyekiti wa JMAT
Tawi la Manyara Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora alisema
kuwa ziara hiyo ya Utalii pia ni sehemu ya kuburudika baada ya kufanya kazi
nyingi kwa muda mrefu.
“Mara nyingi tunafanya kazi hizi za kusikiliza
mashauri kwa muda mrefu na huwa muda wa kupumzika au kuburudika unakuwa mfupi
sana, watumishi wengi hupatwa na msongo wa Mawazo na matatizo mengine kwa
sababu ya kukosa muda wa kupata burudani kama hizi, ninaamini baada ya ziara
hii ya Utalii tuliyoifanya leo, kila mmoja atarejea kituoni kwake akiwa amepata
mtazamo mpya kiakili na hata kisaikolojia” alisema Mhe. Kamuzora.
Katika hatua nyingine Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Bakari Lusewa aliushukuru uongozi
wa Hifadhi ya Ziwa Manyara kwa mapokezi mazuri na kuwatembeza katika maeneo
muhimu ndani ya hifadhi hiyo.
“Kimsingi kazi zetu zina uhusiano mkubwa sana,
wakati nyinyi mnalinda hifadhi hizi, kazi yetu mojawapo kama Mahakama ni
kusikiliza mashauri yanayohusu uhalifu wowote unaotokea katika hifadhi hizi.
Kwa sababu hiyo ziara hii itazidi kuboresha mahusiano yetu na tunawashukuru
sana kwa mapokezi mazuri mliyotupa,” alisema Mhe. Lusewa.
Ziara hiyo ilijuimuisha viongozi waandamizi wa
Kanda hiyo wakiwemo Majaji Mhe. Frank Muyora Mirindo, Mhe. Nenelwa Mwihambi.
Pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama za Wilaya na
za Mwanzo zilizopo katika Wilaya za Babati, Hanang, Kiteto, Mbulu na Simanjiro.
Aidha, katika ziara hiyo, pamoja na
kuwaona Wanyama wa aina mbalimbali, watumishi
walifurahishwa kuona chemchem za maji ya moto yanayotoka ardhini lakini kubwa
zaidi ilikuwa ni kutembea katika Daraja
linalonesanesa ambalo limefungwa na kamba juu ya miti ambapo watumishi wengi
walionekana kupita kwa mashaka na hofu na msisimko japo wengi walifurahi sana
kupita mpaka mwisho bila kuanguka.
Watumishi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara wakiwa wamejipanga kwenye picha ya pamoja wakijiweka tayari kwa ajili
ya safari ya kuelekea katika Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara wakisikiliza kwa makini maelezo ya Viongozi wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe John Kahyoza akifuatiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Frank Mirindo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Frank Mirindo akipita kwenye daraja lililosukwa kwa kamba wakati wa ziara hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara wakiwa katika Daraja la Kamba lililofungwa
juu ya miti katika eneo la Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora (kushoto) akiwa na baadhi ya Waheshimuwa Mahakimu Wakazi kutoka Kanda hiyo Mhe. Neema Lazaro (katikati) na Mhe. Kuruthumu
Mkundawantu (kulia) katika eneo la Hifadhi ya Ziwa Manyara.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni