Na CHRISTOPHER MSAGATI- Mahakama, Manyara
Majaji
na Mahakimu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara wamepatiwa elimu ya
kuwajengea uwezo wa uandishi wa hukumu pamoja na kuendesha mashauri ya uchaguzi
jana tarehe 15 Novemba, 2024 kwa lengo kutatua migogoro itakanayo tokana na
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024 nchini.
Mafunzo
hayo yalikwenda sambamba na Kikao cha Chama Majaji na Mahakimu Nchini Tanzania
(JMAT) Tawi la Manyara na yalifanyika katika Hoteli ya Fanaka Campsite &
Lodges iliyopo katika Eneo la Mto wa Mbu, Wilayani Monduli Mkoani Arusha.
Akifungua mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe Devotha
Kamuzora aliwasisitiza Majaji na Mahakimu waliohudhuria kuzingatia mafunzo hayo
kwa kuwa ni muhimu sana katika majukumu yao ya kila siku.
“Ni
vema tukazingatia mafunzo haya kwa sababu yatatusaidia sana katika uandishi wa
hukumu za mashauri mbalimbali tunayoyasikiliza kila siku na wakati huu ambao
tunaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika siku chache zijazo,
lakini pia ni mafunzo ambayo yanatuandaa vema kwa ajili ya uchaguzi Mkuu
utakaofanyika mwaka ujao 2025” alisema Mhe. Kamuzora.
Akiongea
wakati wa Utoaji wa Mada yake ya Uandishi bora wa hukumu unaozingatia weledi,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza alisema
kuwa, hukumu zinazoandikwa huakisi sifa ya mtu na pia uadilifu wake katika
kazi.
“Hukumu
hizi ambazo tunaandika kila siku katika mashauri yetu tunayoyasikiliza, huwa
zinatutambulisha kwa wananchi na jamii yote kuwa sisi ni watu wa namna gani na
pia hututangazia sifa njema au mbaya kwa watu. Hivyo ni muhimu tukazidisha
umakini na kutanguliza weledi wakati tunaandika hukumu zetu,” alisema Mhe.
Kahyoza.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe Mariam
Lusewa wakati akitoa mada juu ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi,
aliwasisitiza wajumbe kutenda haki wakati wa usikilizaji na utoaji wa Uamuzi wa
mashauri hayo kwa sababu yana umuhimu makubwa katika mustakabali wa taifa.
“Chochote
tutakachokiamua leo, tujue kwamba kina athari hasi na Chanya kwa taifa letu
katika kipindi cha Miaka mitano ijayo. Athari hizi zinapita katika nyanja zote
za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii. Hivyo tuwe makini ili chombo chetu cha
Mahakama kisiliingize Taifa letu katika migogoro au kutokuelewana” alisema Mhe.
Lusewa.
Aidha,
mada nyingine zilizotolewa katika Mafunzo hayo ni Taratibu za Usikilizwaji wa
Mashauri ya Mirathi, Maadili kwa Watumishi wa Mahakama pamoja na masuala ya
Usawa wa Kijinsia.
Chama
cha Majaji na Mahakimu Tawi la Manyara wamekuwa na utaratibu wa kukutana mara
kwa mara kwa ajili ya vikao vya majadiliano yanayohusu Maendeleo ya Chama hicho
na kukumbushana masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa kazi za kila siku.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji na Mahakimu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara waliopata mafunzo ya uandishi wa hukumu na namna bora ya utatuzi wa migogoro inayotokana na uchaguzi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akitoa mada kwa washiriki katika mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya uandishi wa hukumu na utatuzi wa migogoro itokanayo na uchaguzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni