Ijumaa, 15 Novemba 2024

MAJAJI, WASAJILI, MAHAKIMU KANDA YA DODOMA WAPIGWA MSASA KUHUSU MASHAURI YA UCHAGUZI

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amefungua mafunzo ya siku moja yanayohusu ushughulikiaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji, Wasajili pamoja na Mahakimu kutoka Wilaya mbalimbali ndani ya Kanda hiyo.

Akifungua mafunzo hayo leo tarehe 15 Novemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Mhe. Dkt. Masabo amesema mafunzo hayo yamefanyika kwa wakati muafaka kuwakuwa unakaribia uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu. 

“Ni muhimu tujijengee ujuzi na ujuzi unaohitajika ili kuhakikisha utatuzi wa haki wa migogoro ya uchaguzi unafanyika kwa wakati,” amesema Jaji Mfawidhi huyo.

Aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa, anaelewa muda hautoshi kuangazia kila kipengele cha utatuzi wa migogoro ya uchaguzi ndani ya siku moja ya mafunzo bali wana muda wa kutosha wa kushughulikia mada muhimu zaidi kuhusu utatuzi wa migogoro ya uchaguzi. 

“Kwa hiyo ninawasihi kila mmoja wenu ajishughulishe kikamilifu, ajifunze kwa bidii na kwa uangalifu na aweze kutumia ujuzi unaopatikana hapa katika kazi yako ya kila siku. Mafunzo haya yatakupa maarifa na ujuzi wa kuamua kwa haki migogoro ya uchaguzi huku ukihakikisha kwamba maadili ya msingi ya Mahakama yanalindwa,” amesisitiza Mhe. Dkt. Masabo.

Aliongeza kwa kusisitiza kwamba, Mahakama ya Tanzania ina jukumu kubwa katika kusimamia haki katika uchaguzi na kusema kuwa, “kama Majaji na Mahakimu tunabeba jukumu la kipekee la kuhakikisha kwamba ushughulikiaji wa mizozo ya uchaguzi unasalia kuwa wa haki, uwazi na wa haki. Ili kutimiza wajibu huu ni lazima tuzingatie viwango vya juu vya taaluma, uadilifu, na kutopendelea.”

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo, ambapo wawasilishaji wa mada hizo walikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe.Victoria Nongwa ambaye aliwasilisha mada yake kwa njia ya mtandao.

Mada nyingine zilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Emmanuel Ludovick Kawishe ambaye pia aliwasilisha mada yake kwa njia ya mtandao, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri.

Mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni Demokrasia za mfumo wa kisheria za uchaguzi, usimamizi wa uchaguzi na Taasisi zinazosimamia, makossa kabla ya uchaguzi, makosa baada ya uchaguzi, mashauri ya uchaguzi, nidhamu za kimahakama na uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.

Akifunga mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Edwin Kakolaki alisema ana imani kuwa kila mmoja atafanyia kazi yale aliyojifunza katika  mafunzo hayo na kwamba matarajio yake na ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla mashauri ya uchaguzi yatashughulikiwa kikamilifu katika Kanda hiyo  kwa kuwa   wamepata uelewa mzuri  kuhusu   sheria na kanuni za uchaguzi na namna bora ya kushughulikia mashauri ya uchaguzi.

 “Ninawaombeni Mahakimu wote mliobahatika kupata mafunzo haya mkawe chachu ya mabadiliko katika vituo vyenu vya kazi, naomba pia mkawe mstari wa mbele katika kuwashirikisha wenzenu yale yote mliojifunza,” amesema Mhe. Kakolaki. 

Washiriki wa mafunzo hayo wameushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wamesema yamewasaidia kuwajengea uwezo wa uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.

Mafunzo hayo maalum yameratibiwa na Masjala Kuu, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Upendo Madeha (kushoto) na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Selestine Lushasi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kushughulikia mashauri ya uchaguzi.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza kwa umakini kinachojiri katika mafunzo hayo.

 
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma. Walioketi katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Upendo Madeha na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Selestine Lushasi. Waliosimama, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan, anayefuata ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Irene Musokwa  na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa.

Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo kuhusu ushughuliakiaji wa mashauri ya uchaguzi kutoka Mahakama mbalimbali katika Mkoa wa Dodoma. Walioketi katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Upendo Madeha na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Selestine Lushasi.  

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe akiwasilisha mada kwa Mahakimu/washiriki wa mafunzo hayo.

Naibu Msajili Mahakama  Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri akiwasilisha mada kwa Mahakimu/washiriki wa mafunzo ya ushughulikiaji wa mashauri ya uchaguzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Dkt. Juliana Masabo akiwasilisha mada kwa Mahakimu /washiriki wa mafunzo hayo.

 


 Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza kwa umakini mada zilizokuwa zikitolewa katika mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni