Na YUSUFU AHMADI –IJA, Lushoto
Mahakimu Wakazi
wafawidhi 29 wa Mahakama za Hakimu Mkazi nchini wamepatiwa mafunzo ya uelewa na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya
mwaka 2022 (Personal Data Protection Act of 2022) kwa lengo la kuwajengea uwezo
Maafisa hao kuhusu Sheria hiyo na umuhimu wa kulinda haki za faragha za watu
binafsi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania kanda ya Tabora Mhe. Dkt. Adam Mambi kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa
Mahakama hiyo ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Siyani, tarehe 13/11/2024
katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam. Mafunzo ambayo yameandaliwa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na Jamiiforums.
Katika
hotuba yake Mhe. Dkt. Mambi amesema kuwa mapinduzi ya kidigitali yaliyoletwa na
TEHAMA, akili Mnemba na Teknolojia zingine zinazoibuka, yamebadilisha jinsi
taarifa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kusambazwa, hivyo ni muhimu taarifa za
watu binafsi, zikalindwa na kuhakikisha kuwa zinashughulikiwa kwa uadilifu na
heshima.
Pia
amesema kuwa ujio wa Sheria hiyo ya ulinzi wa taarifa binafsi unafanya sasa
ulinzi wa taarifa hizo kuwa wakisheria na sio wa kimaadili pekee jambo ambalo
litasaidia kuepusha madhara mbalimbali kwa watu binafsi, taasisi, biashara na
jamii kwa ujumla.
Vilevile, Mhe. Dkt.
Mambi amewasihi washiriki hao kuielewa vema Sheria hiyo ili waweze kuitekeleza
kwa ufanisi ili kuhakikisha jamii inakuwa na uhakika kuwa taarifa zao binafsi
ziko salama.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Mkilia amewaambia Mahakimu hao pamoja na
maafisa wengine wa Mahakama kwamba nao wana jukumu muhimu katika ulinzi wa
taarifa binafsi kwa kuwa sheria hiyo inaitambua Mahakama kama mdau muhimu
kwenye utekelezaji wa sheria hiyo.
Awali akitoa maelezo
kuhusu IJA, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu Mhe. Dkt.
Patricia Kisinda ameishukuru Tume hiyo ya ulinzi wa Taarifa binafsi kwa
kufadhili mafunzo hayo pamoja na dhamira yao ya kutoa mafunzo kwa Maafisa hao
wa Mahakama akisema kuwa yatasaidia kuimarisha ufanisi na uelewa wao juu ya
Sheria hiyo pamoja na utekelezaji wake.
Mafunzo hayo ya siku
mbili hadi tarehe 14/11/2024 yameanza kwa Mahakimu hao na baadaye yatafanyika pia
kwa makundi mengine ya Majaji na Mahakimu wa ngazi zingine.
Sheria hiyo ya ulinzi
wa taarifa binafsi maarufu PDPA ilitungwa na Serikali mwaka 2022 kwa minajili
ya kuweka mwongozo wa jinsi taarifa binafsi zinapaswa kulindwa ili zisitumike
vibaya.
Aidha mwezi uliyopita, IJA iliendesha mafunzo kwa njia ya mtandao yaliyohusu uelewa wa sheria hiyo ambayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali wa sheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora Mhe.
Dkt. Adam Mambi akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo hayo ambao
ni Mahakimu Wakazi Wafawidhi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ulinzi wa
Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia na kulia ni Mkurugenzi wa Mafunzo
ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA Mhe. Dkt. Patricia Kisinda
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora Mhe.
Dkt. Adam Mambi akihutubia kabla ya kufungua mafunzo ya uelewa na utekelezaji
wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 (Personal Data
Protection Act of 2022) Mahakimu Wakazi wafawidhi 29 wa Mahakama za Hakimu
Mkazi nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo Maafisa hao kuhusu Sheria hiyo na
umuhimu wa kulinda haki za faragha za watu binafsi. Mhe. Dkt. Mambi amefungua
mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji
Kiongozi wa Mahakama hiyo ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Siyani, leo tarehe 13/11/2024
katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akitoa neno la awali katika mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Mhe.
Dkt. Adam Mambi akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji kutoka Jamiiforums Tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi (PDPC).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni