Jumatatu, 18 Novemba 2024

MAHAKIMU GEITA WANOLEWA KUHUSU MASHAURI YA UCHAGUZI

Na CHARLES NGUSA-Mahakama, Geita.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, hivi karibuni iliandaa mafunzo kwa Mahakimu wote mkoani hapa ili kuwakumbusha na kuwaandaa kwenye usikilizaji na uamuzi wa mashauri ya uchaguzi ambao kwa upande wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba, 2024,huku uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ukitarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2025.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 15 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Geitayalijumuisha Mahakimu wa Wilaya ya Geita, huku wengine kutoka Wilaya za Bukombe, Chato,Mbogwe na Nyangh’wale wakishiriki kwa njia ya mtandao.

Akifungua mafunzo hayo,  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina aliwaambia washiriki kuwa mafunzo hayo ni  muhimu kwa kwao kwani yanawaandaa kwenda kuamua mashauri yenye kutoa mstakabari wa hali ya amani na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Wakati mnaendelea na mafunzo hayanaomba niwakumbushe mambo sita muhimu wakati wa kusikiliza, kutatua na kuamua mashauri ya uchaguzi. Haki ya wananchi kupiga kura na kushiriki uchaguzi, tukumbuke kuwa mamlaka ya Serikali yanatoka kwa wananchi, uchaguzi huru na wa haki,uchaguzi unaozingatia demokrasia na utawala bora, uzingatiaji wa haki za binadamu na kuangalia namna gani wananchi walivyofikiwa katika uchaguzi, alisema.

Katika mafunzo hayo, washiriki wao, kama watoa haki, walikumbushwa kushirikiana na Taasisi zingine kama Tume Huru ya Uchaguzi na wadau wengine kuhusu sheria za uchaguzi. Aidha, washiriki pia walikumbushwa kusoma maamuzi na machapisho mbalimbali ambayo yalishawahi kutolewa yanayohusu mashauri ya uchaguzi.

Katika mafunzo hayo, watoa mada mbalimbali walikuwepo ambao ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Fredrick Lukuna na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya TaboraMhe. Pamela Mazengo.

Washiriki katika mafunzo haya waliweza kupitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo iliyojikita katika kueleza kuwa ni namna gani  Mahakama inafikika kwa urahisi, utoaji wa maamuzi bila upendeleo na bila kuingiliwa na ufuataji wa taratibu kuanzia mwanzo hadi mwisho pamoja na kutoa maamuzi kwa wakati. 

Mada ilijikita katika kuwakumbusha washiriki juu ya kuzingatia taratibu za uchaguzi, mchakato wenyewe wa uchaguzi na mamlaka zinazohusika kama Tume huru ya uchaguzi, kwa upande wa Tanzania  Bara Tanzania visiwani.

Kulikuwa pia na mada iliyojikita katika kuwajengea uwezo washiriki uelewa wa pamoja juu ya haki za wapiga kura na wagombea kipindi cha uchaguzi, misingi ya maadili kipindi cha uchaguzi, makosa ambayo yanaweza kutokea kabla,wakati na baada ya uchaguzi na kuelewa mfumo mzima wa kisheria katika kutatua na kusikiliza makosa ya uchaguzi.

Mada nyingine ilijikita katika kuwajengea uwezo washiriki uelewa wa pamoja juu ya makosa ya uchaguzi,wajibu wa watoa haki katika kusikiliza mashauri ya uchaguzi, wajibu wa wapelelezi na wadau wengine pamoja na wajibu wa wasimamizi wa uchaguzi. 

Washiriki pia walipitishwa kwenye mada iloiyojikita katika kuwakumbusha kutambua athari ambazo zinaweza kuwafanya kwenda kinyume na maadili katika kutatua mashauri ya uchaguzi na pia wasipende kushiriki mijadala ya kisiasa na kuonesha mrengo wa kiitikadi wakati wa kusikiliza mashauri hayo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina (anayeonekana kwenye runinga) akifungua mafunzo hayo kwa njia ya mtandao ambapo yeye alikuwa ofisini kwake na washiriki walikuwa ukumbini.

Sehemu ya washiriki walioshiriki wakiwa ukumbini wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa.

Miongoni mwa washiriki walioshiriki kwa njia ya mtandao kutoka Mahakama ya Wilaya Nyangh’waleMhe.Robert Igogo Nyando (anayeonekana katika runinga) alipopata wasaa wa kutoa ufupisho wa mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni