- Yajipanga kufuatia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Na RICHARD MATASHA, Mahakama-Mtwara
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara imefanya mafunzo maalum kuhusu Utatuzi wa Migogoro ya Uchaguzi ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha uwezo wa Taasisi za kisheria katika kushughulikia migogoro ya uchaguzi sambamba na kuboresha ufanisi wa mfumo wa uchaguzi nchini.
Mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) lengo likiwa ni kuimarisha uwezo wa kushughulikia migogoro ya uchaguzi kwa ufanisi, kuhakikisha kuwa haki za wapiga kura na wagombea zinahifadhiwa wakati na baada ya uchaguzi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim alisisitiza umuhimu wa uhuru wa kisheria na umahiri katika kutatua migogoro ya uchaguzi kwa haki na kwamba jinsi migogoro hiyo inavyoshughulikiwa, moja kwa moja inaathiri imani ya umma katika mfumo wa uchaguzi, jambo muhimu kwa mchakato wa kidemokrasia wa nchi.
“Mafunzo haya yatasaidia kuhakikisha kuwa wale wanaohusika na kutatua migogoro ya uchaguzi si tu kwamba wanakuwa na uelewa wa kisheria bali pia wanakuwa na ufahamu wa muktadha wa kisiasa na kijamii ambao migogoro hiyo hutokea,” alisema Jaji Ebrahim.
Mafunzo hayo yalilenga kuwapa washiriki ujuzi wa vitendo kuhusu namna ya kutatua migogoro ya uchaguzi, kuanzia ufafanuzi wa sheria za uchaguzi hadi kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kupokea na kushughulikia mashauri ya uchaguzi. Vilevile yalijikita katika mbinu za kisheria na taratibu za usikilizwaji wa mashauri pamoja na umuhimu wa kumaliza mashauri kwa haraka na kwa uwazi.
Washiriki walipata fursa ya kutathmini mifano ya mashauri maarufu ya migogoro ya chaguzi zilizopita huku wakichambua namna zilivyoshughulikiwa kisheria na matokeo yake, ili kutoa mapendekezo ya kuboresha mchakato wa kutatua migogoro ya uchaguzi siku zijazo.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Mwanga, ambaye alitoa uelewa kuhusu mfumo wa sheria na changamoto zinazoweza kutokea katika utatuzi wa migogoro ya uchaguzi.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Majaji na Mahakimu ambao wote wanachukua jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi..
Washiriki walielezea kwamba mafunzo hayo yatasaidia kuboresha uwezo wao wa kutatua migogoro ya uchaguzi kwa njia bora zaidi, huku wengi wakieleza kwamba, juhudi hizo zitasaidia kuongeza imani ya umma katika Taasisi za uchaguzi za Tanzania.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya uchaguzi. Walioketi pamoja naye wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Hamidu Mwanga ambaye ni mkufunzi wa mafunzo hayo (kushoto), wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi (kulia), wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Martha Mpaze na wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mkufunzi wa Mafunzo ya Uchaguzi yaliyotolewa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Hamidu Mwanga akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Martha Mpaze akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatiliia jambo kwa umakini katika mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni