Na EUNICE LUGIANA & BROWN MTIMBA, Mahakama-Kinondoni
Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni wamepatiwa mafunzo kuhusu uwepo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPA) na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).
Akifungua mafunzo hayo jana tarehe 18 Novemba, 2024 Kituoni hapo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mhe. Is-haq Kuppa aliwajulisha watumishi hao kwamba amelazimika kutoa elimu hiyo baada ya kuona umuhimu wa watumishi hao kupata mafunzo hayo.
“Nimelazimika kuwapitisha katika mafunzo haya baada ya mimi nikiwa ni miongoni mwa watumishi wachache wa Mahakama ya Tanzania kupatiwa mafunzo hayo tarehe 13 na 14 Novemba, 2024 kutoka kwa Wawezeshaji kutoka Tume hiyo wakishirikiana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe.Prof. Ubena John Agatho,” alisema Mhe. Kuppa.
Mhe. Kuppa alisema Sheria hiyo ya mwaka 2022 imeanza rasmi kutumika tarehe 01 Mei, 2023 imefafanua vizuri juu ya uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) katika kifungu cha 6 (1) cha Sheria hiyo pamoja na majukumu ya Tume kama yalivyoorodheshwa katika kifungu cha 7 (a-h) kinahusika na ufuatiliaji wa Sheria husika, kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko kuhusu madai ya ukiukwaji wa ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu.
Vilevile, inachunguza na kuchukua hatua dhidi ya jambo lolote ambalo Tume itaona linaathiri ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu.
Pamoja na mambo mengine watumishi hao walifahamishwa kwamba, kufuatia uanzishwaji wa Sheria hiyo, usajili wa wakusanyaji taarifa, malalamiko yote ya kimadai yanashughulikiwa na Tume ambayo ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kwa kutoa tuzo ikiachia makosa ya kijinai kama yanavyoonekana katika vifungu vya 60, 61, 62 na 63 vya Sheria husika ambayo ndio yatasikilizwa katika Mahakama.
Mfawidhi huyo, aliwasisitiza Mahakimu waliohudhuria mafunzo hayo kuwa, kwa sasa Mahakama nchini hazina mamlaka ya usikilizaji na kuamua malalamiko ya kimadai dhidi ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Watumishi hao walisisitizwa pia kuisoma Sheria hiyo pamoja na kanuni zake ili waweze kupata uelewa zaidi na kuchukua tahadhari zote za kutotenda makosa kama yalivyofafanuliwa katika Sheria hiyo.
Akichangia mada katika mafunzo hayo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Jacqueline Rugemarila amewaasa watumishi wawe makini juu ya taarifa binafsi na faragha za watu kwa kutoshiriki kwa namna yoyote ya usambazaji kwa kuwa Sheria sasa ipo na itachukua mkondo wake kwao kwa kuwa hakuna aliye juu ya Sheria.
Naye, Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Bi. Aisha Kaungu alimshukuru Mwezeshaji na kumuomba afanye utaratibu wa kila mtumishi kupata nakala laini ya Sheria husika na kanuni zake kwa urahisi ya rejea.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mhe. Is-haq Kuppa (aliyesimama mbele) akitoa elimu kwa watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni