Na ARAPHA RUSHEKE –Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani jana tarehe 16 Disemba, 2024 amefungua mafunzo kwa
watumishi wenye mahitaji maalumu yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) .
Akifungua
mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa OSHA jinini hapa, Mhe.
Dkt Siyani alisema anafahamu Serikali imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa
watumishi wake, lakini ni aghalabu kwa mafunzo maalumu kutolewa kwa kundi la
watumishi wenye mahitaji maalumu peke yake.
“Bila shaka
kila mtumishi wa umma, iwe ni mwenye mahitaji maalumu au laa, anao mchango
mkubwa katika ujenzi wa Taifa, kwa hiyo ni muhimu sana kwa waajiri na wadau kutambua
umuhimu wa mafunzo kwa watumishi na
kuwatengenezea mazingira salama ,” alisema.
Mhe. Dkt. Siyani aliongeza kuwa, katika
kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, Mahakama imedhamiria kushirikiana na
wadau mbalimbali, hivyo ushirikiano huo baina ya Mahakama ya Tanzania na OSHA
kwa sehemu moja ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama.
“Hivyo
mafunzo haya ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa jamii yetu na
kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi pamoja na usalama wao mahala pa kazi
zinazingatiwa na kulindwa ipasavyo,” Jaji Kiongozi alisema.
Alitumia fursa
hiyo kuwasihi wote kushiriki mafunzo hayo kikamilifu, watumie fursa hiyo
kutambua na kuelewa haki mbalimbali wanazostahili ili kuwawezesha kutimiza
majukumu yao na kuepukana na changamoto zinazoweza kutokea.
Mhe. Dkt.
Siyani alisisitiza kuwa watumishi wote ni sawa, hivyo kila mmoja anapaswa ana nafasi
ya kuchangia maendeleo.
Aliishukuru Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi na OSHA kwa kuandaa mafunzo hayo yenye dhamira ya kujenga
uelewa juu ya afya, usalama,haki na
wajibu wa wafanyakazi wenye mahitaji maalum mahala pa kazi.
“Ushirikiano wa aina hii ni muhimu kuigwa na
taasisi nyingine, kwa upande wa Mahakama milango ya ushirikiano iko wazi katika
kuhakikisha watumishi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalumu wanapatiwa fursa ya
mafunzo mbalimbali. Matumaini yangu ni kwamba waajiri na wadau wengine
wataendelea kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi,” alisema Jaji Kiongozi.
Naye, Mtendaji
Mkuu wa OSHA, Bi Hadija Mwenda aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia
fursa hiyo kujifunza vitu vingi na kwa weredi mkubwa.
Mafunzo hayo
ambayo yatatolewa kwa siku mbili kuanzia tarehe 16 Disemba ,2024 hadi 17
Disemba 2024 yamewalenga watumishi wenye uhitaji maalumu mahali pa kazi kwa
watumishi wa Mahakama na Taasisi nyingine za umma.
Meza kuu ikiongozwa na mgeni rasmi, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani(aliekaa katikati), kushoto kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Joseph Mlyambina, anaefuatia ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Fatma Khalfani, kulia kwake ni Kamishna wa kazi Tanzania Bara, Bi. Suzan Mkangwa, anaefuatia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi, Bi.Hadija Mwenda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi, Bi.Hadija Mwenda (aliesimama) akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa OSHA jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Watu Wasioona Tanzania, Bw.Omary Itambu Amasi, akitoa neno la ukaribisho kwa niaba ya washiriki wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa OSHA jijini Dodoma.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Joseph Mlyambina akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo.
Jaji kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliesimam katikati) akikabidhiwa zawadi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi, Bi.Hadija Mwenda.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni