Jumatatu, 16 Desemba 2024

MAHAKAMA SONGWE YASHIRIKI UZINDUZI KAMPENI MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA

 Na Iman Mzumbwe-Mahakama, Songwe

Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe juzi hivi karibuni ilishiriki katika zoezi la uzinduzi wa huduma ya kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) ili kuunga mkono juhudi za utoaji elimu kwenye masuala mbalimbali ya kisheria.

Kampeni hiyo imeandaliwa kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuongeza uelewa wa kisheria na upatikanaji wa haki, mifumo ya utoaji haki kuweka mazingira wezeshi na kulinda na kukuza haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Fraida Mguni alizinduzi Kampeni hiyo katika Viwanja vya CCM Mkoa Songwe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Daniel Chongolo. Aidha baada ya uzinduzi huo kufanyika, Bi. Farida alikagua mabanda ya Taasisi mbalimbali zinazoshikiri katika zoezi la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Moja ya Banda alilotembelea ni la Mahakama ambapo alijionea shughuli zinavyofanyika, huku Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Mbozi, Mhe. Vitalis Changwe akielezea namna ambavyo Mahakama imejipanga kutoa elimu ya kisheria kwenye maeneo ya mirathi, wosia, dhamana na makosa ya kijinai.

Bi Farida aliendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa Songwe kuchangamkia fursa hiyo ili kusaidia kupunguza na kutatua kero na migogoro iliyopo bila malipo yeyote.

Wakizungumza katika nyakati tofauti, wananchi wamesema huduma hiyo imewafurahisha na kuwapa mwanya kuwa sasa wanaweza kutatua matatizo yao ya kisheria bila gharama zozote.

Katika uzinduzi huo kulikuwa na Taasisi mbalimbali za kutoa msaada wa kisheria kama vile Wizara ya Katiba na Sheria, Wakala wa Usajili na Udhamini, Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Kujitegemea, TAWLA, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa Songwe na Mabenki.


Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgumi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na meza kuu.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgumi akisaini katika kitabu cha wageni katika banda la Mahakama Mkoa wa Songwe.

Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Mbozi, Mhe. Vitalis Changwe akimuelezea mgeni rasmi mambo mbalimbali alipotembelea  banda la Mahakama.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgumi akikagua banda la Wizara ya Katiba na Sheria.

Banda la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa Songwe.

Sehemu ya wananchi waliohudhuria katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya msaada wa kisheria.

Banda la Mahakama Mkoa wa Songwe.

Vikundi mbalimbali vikiingia katika viwanja vya uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni